Yaliyochambuliwa na wahariri wa Ujerumani
21 Juni 2006
Mvutano umezuka bungeni kati ya upande wa upinzani na serikali kuhusu bajeti ya mwaka 2006.Bajeti hiyo inakadiria matumizi ya serikali yatafikia yuro bilioni 261,pakihitajika mkopo wa yuro bilioni 38.Wahariri kadhaa wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha na suala hilo,sawa na walivyomulika mtihani aliokabiliana nao kansela Angela Merkel katika “siku ya viwanda nchini Ujerumani.
Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE linahisi mkopo mwengine wa kukidhi matumizi ya serikali,ni mtihani mkubwa.Gazeti linaendelea kuandika:
“Ikiwa Ujerumani inahitaji kupigwa jeki kama kansela Angela Merkel anavyosema-basi hatua za kuziba nyufa hazitasaidia kitu.Waziri wa fedha Steinbrück anatetea umuhimu wa mkopo huo katika kuupa msukumo ukuaji wa kiuchumi utakaochangia kuimarisha bajeti.Lakini nakisi kubwa kubwa sizo zitakazoinua ukuaji wa kiuchumi seuze kupelekea kuongezeka idadi ya waajiriwa.”
Hata gazeti la mjini Mainz Allgemeine Zeitung linavikosoa vyama vinavyoundea serikali ya muungano mjini Berlin.Gazeti linaendelea kuandika.
“Kiroja hapa lakini ni kwamba kile dhaifu kinachowafungamanisha washirika wa serikali ya muungano wa vyama vikuu,kinatuwama katika ukweli kwamba,hata mapato yajayo,yanayokadiriwa kukukusanywa toka nyongeza za kodi,yameshajumuishwa katika hesabu zao.Zaidi ya hayo,shirikisho la jamhuri ya Ujerumani imepitisha kwa mara nyengine tena bajeti ambayo mtu anaweza kusema haiambatani na muongozo wa katiba.
Ni jambo la kusikitisha sana,kwamba serikali ya muungano wa rangi nyeusi na nyekundu haijaweza kuutumia ipasavyo wingi wao wa viti bungeni kupitisha hatua ya kijasiri.”
Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linaamini upande wa upinzani ndio ulioondolewa patupu katika mjadala huo wa bajeti.Gazeti linaadika:
“Wapige makelele watakavyo bungeni wana FDP,walinzi wa mazingira-Die Grüne na wawakilishi wa chama cha mrengo wa shoto-Linkspartei,lakini katika enzi za muungano wa vyama vikuu,malumbano ya kweli hayawi kati ya serikali na upande wa upinzani,bali kati ya wawakilishi wenyewe kwa wenyewe wa serikali ya muungano wa vyama vikuu.
Hayo yamedhihirika sio tuu katika mijadala ya mageuzi ya sekta ya afya na kodi ya makampuni,hata katika mijadala ya bajeti-vuta nikuvute kati ya vyama ndugu vya CDU/CSU na SPD imetosha kusababisha mivutano.Lawama wanazotupiana washirika katika serikali ya muungano sio tuu zinabainisha mfarakano uliopo kati yao bali pia unabainisha hata wenyewe hawajaridhika na waliyoyafanya hadi sasa.”
Mada ya pili magazetini inahusu siku ya viwanda nchini Ujerumani.Wahariri wanahisi kansela Angela Merkel hakuranda katika uwanja wa nyumbani.Mwenyekiti wa shirikisho la viwanda vya Ujerumani-BDI ,Jürgen Thumann ameitaka serikali iharakishe kutia njiani mageuzi.Wahariri wengi wamemulika jinsi kansela alivyokua katika maadhimisho ya siku ya viwanda nchini Ujerumani.
Gazeti la MÜNCHENER MERKUR linahisi mwisho wa hali ya usuhuba unakurubia.
Nalo gazeti la Die Welt la mjini Berlin linaamini lawama za wanaviwanda hazitaishia vivi hivi tuu.
Gazeti la OSTSEE-ZEITUNG la mjini Rostock lakini linamsifu kansela Angela Merkel na kusema,ingawa ni mhafidhina,mwenye kuwapendelea zaidi wana viwanda,lakini zawadi nono nono za kodi ya mapato wasitaraji angalao kwa sasa kuzipata wanaviwanda.