Yaliyochambuliwa na wahariri wa Ujerumani hii leo
29 Juni 2005
Kuhusu kura ya imani kwa kansela Gerhard Schröder,gazeti la mjini München,SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limeandika:
“Aliwahi kuahidi wakati mmoja ,”hatobadilisha yote,lakini mengi yatakua bora.”Sasa kansela Gerhard Schröder anafanya yale yale ambayo kansela Kohl aliyatenda mwaka 1982.Kura ya imani,atakayoizusha ijumaa ijayo ,ni ya hadaa,sawa na ile iliyoitishwa na Kohl wakati ule…Tofauti ndogo ya kisiasa iliyopo ni kwamba wakati ule Kohl alijiamini na chaguzi za kabla ya wakati hazikumbwaga.Schröder ametangaza mbinu yake bila ya matumaini makubwa kama anachokitaka atakipata.Kwa maneno mengine amejibwaga tuu ,akijiambia “tusubiri tuone matokeo yatakua ya aina gani.”Hadi sasa lakini mambo yanazidi kumharibikia.Hawajakosea wanaposema “mkamia maji hayanywi.”
Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linalalamika na kuandika:
“Rais wa kawaida anaweza kutofautisha kati ya kura ya imani na kura ya kutokua na imani.Katika uwanja wa kisiasa lakini kila siku tunapewa uchambuzi mpya wa maneno haya mawili ambayo tafsiri yake ni bayana.Kipa umbele ni kimoja tuu,nacho ni hila kuhakikisha kura ya maoni inashindwa na wakati huo huo watu wakijiandaa kwa kampeni za uchaguzi.”
Gazeti la MANNHEIMER MORGEN linachambua”
“Kansela na mwenyekiti wa chama wa chama cha SPD wanalazimika kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kura ya imani inashindwa.Wanambabaisha rais wa shirikisho na pengine hata kuilaghai korti kuu ya katiba.Kwa ufupi yanayotendeka si chengine isipokua dharau.
Gazeti la mjini Berlin NEUES DEUTSCHLAND linazungumzia shauri la mwenyekiti wa chama cha SPD,FRANZ MÜNTERFERING aliewataka wabunge wa chama chake wajizuwie kupiga kura.Gazeti limeandika:
“Sio wote walioelewa.Pengine kuna huyu au yule ambae hajahudhuria mafunzo ya lahaja,lakini kwamba wasiwe na imani na kansela ,kwa maneno mengine waunge mkono kura ya kutokua na imani,hakuna ambae hajauelewa usemi huo.”
Gazeti la ESSLINGER Zeitung linazungumzia juu ya wajib wa rais wa shirikisho na kusema:
“Köhler amebakiwa na njia mbili “ anaweza kuitisha uchaguzi wa kabla ya wakati ,akijiambatanisha na vifungu vya katiba au kukataa kulivunja bunge kwa sababu hiyo hiyo.Si uamuzi rahisi,lakini chaguo la pili lina auzito mkubwa zaidi.Akiruhusu uchaguzi mpya kuitishwa,kuna hatari,korti kuu huenda ikaingilia kati wakati kampeni za uchaguzi zinaendelea na kuutaja utarativbu mzima kua kinyume na sheria.Madhara yake ni makubwa kupita kiasi.Njia moja ambayo ni bora kuliko zote,Schröder anaweza kuitumia nayo ni kujiuzulu.Kwanini lakini hataki kujiuzulu? Hakuna ajuaye.
Mada nyengine iliyochambuliwa na magazeti hii leo inahusu hotuba ya rais George W. Bush wa Irak.Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linahisi:
“Kushindwa jeshi la Marekani kukomesha mataumizi ya nguvu kumemdhoofisha sana rais Bush.Wapiga kura wamemchagua tena kwasababu walijiwekea matumaini uongozi wake ni bora zaidi katika enzi hizi za vita kuliko wa mpinzani wake.Na sasa anashindwa kule kule ambako wananchi walikua wakitarajia angefaulu-tuachilie mbali ukweli kwamba hivi sasasio wengi wanaomuanini.Haitakua rahisi kuubadilisha mkondo wa mambo.Na mkondo wa mambo katika sera za serikali kuelekea Irak si suala la kujadiliwa.Kwa maneno mengine,sera zile zile za zamani zitaendelezwa kwa jina jipya.
Mada ya mwisho inahusu uamuzi wa kuruhusiwa Ufaransa ijenge mtambo mkubwa wa utafiti wa nishati ya mchanganyiko ITER.Gazeti la mjini Berlin Die Welt linahisi:
“Uamuzi wa kujengwa mtambo wa ITER nchini Ufaransa ni uamuzi wa maana kwa mahitaji ya baadae.Teknolojia hiyo ya kimambo leo inaashiria uwezekano wa kumtoa binaadamu toka shida ya ukosefu wa nishati,mamoja katika nchi za viwanda au katika nchi zinazoinukia.Nchini Ujerumani kuna sauti zinazopazwa kuukosoa mradi huo eti utafiti huo ni fedha za bure.Si uongo kwasababu hakuna ajuae bado vipi mtambo huo utaweza kufanya kazi kiufundi.Kwa vyovyote vile lakini watu wanabidi wajaribu.Pengine utaleta tija.