Yaliyochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo
28 Novemba 2005Waziri mpya wa mambo ya nchi za nje wa serikali kuu ya Ujerumani Frank-Walter Steinemeier anakwenda Washington kwa ziara yake ya kwanza nchini Marekani.Kabla ya hapo ripoti kuhusu kusafirishwa kwa siri wafungwa na idara ya upelelezi ya Marekani CIA,zilipandisha mori miongoni mwa jamii.Magazeti ya Ujerumani hii leo yanachambua ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje mjini Washington.Die SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linampima waziri wa mambo ya nchi za nje kwa mtazamo wa Marekani na kuandika:
„Bila shaka,serikali ya Marekani ingependelea kumuona mwasiasa mwengine akimrithi Joschka Fischer,badala ya mshirika wa dhati wa kansela wa zamani Gerhard Schröder.Mpinzani huyo wa vita vya Irak hakuna hata mmoja mjini Washington anaemsikitikia.Lakini yote hayo ni bure kwasababu,kwanza watu wa Bush hawatoulizwa maoni yao na pili hofu zao kwamba ndege aliyeambukizwa virusi vya Schröder anaingia tunduni mwao,hazitakawia kufifia.Na tatu,na hiyo ni sawa kwa wote-wanalazimika kumkubali yeyote aliyechaguliwa.Kashfa za ndani na hasa masaibu ya Irak yanamfanya rais asiwe na njia n yengine isipokua kujihami.“
Gazeti la MANNHEIMER MORGEN linaandika:
„Frank-Walter Szeinmeier hatoweza hata kidogo kuripuuza ripoti kuhusiana na safari za ndege za udanganyifu za idara ya upelelezi ya Marekani CIA.Tangu september 11,serikali ya Washington, inajichukulia kile ambacho mtu anaweza kukiita hatua za dharura ambazo haziambatani hata kidogo na misingi ya sheria za kimataifa, kuendeleza mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa.Si jukumu la serikali ya Ujerumani kuikosoa hali hiyo hadharani.Lakini pia haiwezi kunyamaza kimya au hata kuvumilia viwanja vya ndege vya kijeshi katika ardhi ya Ujerumani vinapotumiwa kuendeleza mambo ambayo pengine yanakwenda kinyume na msinghi ya haki za abinaadam.Dola huru,sio tuu lina haki bali pia lina jukumu na wajibu wa kudai ufafanuzi.Uhusiano wa pande hizi mbili hautotetereka eti kwasababu Ujerumani haiko tayari kusabilia maadili yake.
Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE linahisi:
„Ya kurekebishwa yako tena mengi tuu katika uhusiano kati ya Ujerumani na Marekani.Lakini hali namna ilivyo haionyeshi kua ni ya kawaida hii leo waziri wa mambo ya nchi za nje Steinmeier anapoanza ziara yake ya kwanza nchini Marekani.Si jambo la kustaajabisha mtuhumiwa akiandamwa na baadae kupelekwa mahala kokote kule kuhojiwa.Lakini ikiwa mfungwa atateswa,mamoja wapi na nani,hapo watu hawastahiki kuvumilia.Hapa sasa serikali ya Marekani imejipatia fursa ya kurekebisha baadhi ya mambo.“
Gazeti la KÖLNER STADT Anzeiger linachambua uhusiano namna ulivyo kati ya Marekani na Ujerumani.Gazeti linaandika:
„Jamii ya watu katika nchi za magharibi pengine ingeiachia Marekani nafasi ya kutosha kuwaandama na kupambana na magaidi,ingekua serikali ya Marekani mjini Washingon na idara zake za upelelezi zinaaminiwa.Lakini hali ni nyengine kabisa.Baada ya september 11,Marekani imejikuta katika mtihani na kulazimika kuihami misingi ya sheria zake wenyewe…. visa vya kinyama kujibiwa isivyostahiki.Lakini kwa kuitolea mhanga misingi ya kisheria,sifa za dola ya kidemokrasi zinachafuliwa.
Mada nyengine iliyochambuliwa magazetini ni azma ya waziri wa mambo ya ndani Wolfgang Schäuble ya kutumia data zilizokusanywa na madareva wa malori ili kuwafichua magaidi na wahalifu wengine..Gazeti la SAABRÜCKER ZEITUNG linahisi fikra si mbaya lakini ina walakin.Gazeti linaandika:
„Kwa mtazamo wa kijuu juu,hoja zake si mbaya.Linapohusika suala la kuzuwia uhalifu au wahalifu kuandamwa,hakuna pingamizi.Na hapo waziri mpya wa mambo ya ndani Wolfgang Schäuble hajakosea hata kisogo,ana haki sawa na aliyemtangulia Otto Schilly.Lakini fikra ya Schäuble ndio yenye walakini hasa kwa upande wa kuhifadhiwa data.