Yaliyoandikwa na wahariri wa Ujerumani hii leo
30 Agosti 2006
Bila ya kujali maoni ya wananchi yakoje kuelekea serikali ya muungano wa vyama vikuu,kansela Angela Merkel na makamo wake Franz Müntefering wanaonyesha wamepania kuendeleza mkondo wa mageuzi.Walichokisema katika mkutano pamoja na waandishi habari mjini Berlin-“Tuendelee vivyo hivyo” kinakosolewa sana na wahariri wa humu nchini.Gazeti la MANNHEIMER MORGEN linahisi:
“Mwenye kuitembeza siasa yake namna hiyo hata kumshinda Gerhard Schröder na agenda 2010-hajitokezi kama walivyokua Angela Merkel na Franz Müntefering.Kujitokeza kwao namna ile ni mbiu tuu za kuficha mvutano wa kina ambao ni shida kuufumbua.Linapohusika suala la mageuzi ya mfumo wa afya kwa mfano,chama cha Social Democratic kinahisi kimejipatia fursa ya kuvuruga mfumo wa bima ya kibinafsi uliokua hadi sasa ukipendwa na kutetewa na wahafidhina wa CDU/CSU.
Katika suala la kufanyiwa marekebisho mfumo wa malipo ya kodi kwa waajiri,,licha ya kuongezeka michango iliyokusanywa toka kodi za mapato mwaka huu,wanatafuta njia ambayo kusema kweli hataitawarahisihia mambo waajiri.Vipi serikali ya muungano wa vyama vikuu itaweza kukabiliana na vizinbgiti hivi,yadhihirika hata kansela mwenyewe bado hajui vipi.”
Gazeti la OSTSEE-ZEITUNG la mjini Rostock linahisi:
“Vyama vya rangi nyeusi na nyekundu vinajaribu kuvuta wakati linapohusika suala la kutia njiani mageuzi tete.
Mageuzi ya mfumo wa afya ni ya lazima-lakini yana machungu.Kuna makosa katika mfumo wa malipo wa wakosa ajira wa muda mrefu maarufu kwa jina la Hertz nambari nne.Na walakini katika mageuzi ya mfumo wa kodi ya mapato ambayo ni shida kwa mtu kuweza kutambua kama yataleta faida au kama ni upuuzi mtupu tuu.
Kwa upande mmoja mashirika ya kiuchumi yatafaidika yakipunguziwa mzigo wa malipo ya kodi kwa upande wa pili ni shida kuwatanabahisha watu kwanini watu walazimishwe kulipa viwango vya juu vya kodi ya mauzo kama michango ya kodi za mapato imepindukia kiwango kilichokadiriwa na kufikia yuro bilioni 20?Serikali ya muungano wa vyama vikuu inaangaliwa kwa namna hiyo kama muungano wa usumbufu mkubwa.Kwa waajiriwa, kwa wasiokua na ajira na hata kwa watu waliostaafu.”
Gazeti la KÖLNISCHE RUNDSCHAU linajiuliza:
„Tunaelekea wapi?Falsafa msingi ya serikali hii ya muungano ni ya aina gani kama inazungumzia kwa upande mmoja juu ya kupunguza matumizi lakini wakati huo huo inawakamua wananchi.Inabidi angalao ifafanue mkondo gani wa kufuatwa-Ujumbe unaabidi uwe lawama na kupungua imani ya wananchi si mambo mazuri na sio kama ilivyosemwa jana:tuendelee vivyo hivyo na kugusia mara hapa mara pale ,na tukishindwa ,tuwachilie mbali.“
Mada ya pili magazetini ni kuhusu mzozo uliosababishwa na mradi wa kinuklea wa Iran.Muda mfupi kabla ya kumalizika muda uliowekwa na baraza la usalama la umoja wa mataifa ,rais Mahmoud Ahmadinedjad anapinga kwa mara nyengine tena kusitisha mipango ya nchi yake ya kurutubisha maadini ya uranium.
Kwa maoni ya gazeti la Die Welt,rais wa Iran anafuata mkakati maalum.Gazeti linaendelea kuandika:
„Ahmadinedjad anategemea zaidi hitilafu za maoni ndani ya baraza la usalama na kutaraji ukorofi utatokea huko huko ndani ya umoja wa mataifa.Shida kubwa zaidi itakua kuzishawishi Urusi na China zikubali kufuata msimamo wa pamoja.Kinyume na afikirivyo rais wa Iran,kizingiti hicho lakini kinaweza kukiukwa.Si kwa masilahi ya Moscow kama nchi jirani ya Iran inamiliki silaha za kinuklea.Kwa hivyo vikwazo haviko mbali dhidi ya Iran.Na ikilazimika watu wasichelee kutumia kitisho cha kuzuka vita ikiwa kitasaidia.Ahmadinedjad anabidi atanabahi kiu cha Iran cha kumiliki nguvu za kinuklea kiitawadhuru wenyewe.“