Yaliyoandikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo
24 Novemba 2005Kuhusu ziara ya kansela Angela Merkel mijini Paris na Brussels limeandika gazeti la mjini Düsseldorff kama ifuatavyo:
„Bibi kansela Angela Merkel-hapo watu watabidi kwanza wazoee kusema hivyo,na sio tuu humu nchini,bali pia nchi za nje.Watu watafuatilizia kwa makini tena bila ya kupepesa kila kitu wakati wa ziara hiyo ya kwanza ya kiongozi mpya wa serikali ya Ujerumani-lilitishia gazeti la kihafidhina la Ufaransa „Le Figaro“ kabla ya ziara ya kansela Markel.Lakini kile ambacho wafaransa hawajakiona licha ya kukitegemea ni busu juu ya shavu na kukumbatiana kama ilivyokua ikishuhudiwa kati ya Gerhard Schröder na Jacques Chirac ambapo hata watazamaji wa televisheni walikua wakiduwaa.Kansela wakike mtu hawezi kumbusu seuze kumkumbatia.Amejitokeza lakini akiwa makini na mwenye bashasha,kiongozi anaejiamini mwenye kutetea masilahi ya Ujerumani.“
Gazeti la Die Welt la mjini Berlin linaamini:
„Katika wakati ambapo rais Jacques Chirac anazungumzia juu ya mhimili wa Ujerumani na Ufaransa,kansela Angela Merkel ameonolea bora kuzungumzia juu ya urafiki.Kwa namna hiyo ameukwepa uhusiano wa aina pekee ulioanzishwa na Gerhard Schröder uliotuwama mahala pamoja tuu.Kansela huyu wa kike anataka kurejea katika enzi za siasa ya nje ya kawaida,kama ilivyokua ikifuatwa tangu enzi za Konrad Adenauer-akitengwa Gerhard Schröder.Siasa hiyo imejengeka chini ya misingi ya kutilia maanani„kote“,ikimaanisha uhusiano wa dhati pamoja na Paris lakini bila ya kuzitenga nchi nyengine za ulaya.Kuutunza uhusiano wa Ujerumani na Ufaransa lakini bila ya kuiudhi Marekani.
Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung linahisi:
„Fikra ya Chirac na Schröder ya kutaka kuupanua mhimili hadi Moscow lilikua kosa:Washington iliiangalia fikra hiyo kama jaribio la kushindana nayo na ndio maana haikuchelea kuipinga ;ushahidi upo, unakutikana katika kushindwa juhudi za Ujerumani za kupigania kiti cha kudumu katika baraza la usalama la umoja wa mataifa;Na miongoni mwa wanachama wepya wa Umoja wa Ulaya kutoka ulaya ya kati na mashariki,fikra hiyo ilizidisha dhana wanatumiwa tuu kwa masilahi ya kisiasa ya wengine.Kama dalili za enzi mpya zimechomoza,bila ya kusababisha madhara ya kidiplomasia mjini Paris na Moscow,si suala litakalotegemea pekee werevu na mbinu za bibi Angela Merkel.“
Mhariri wa gazeti la BERLINER ZEITUNG anahisi:
„Katika muida mfupi unaotukabili tutashuhudia mchanganyiko wa utaratibu uliokua ukiendelezwa wakati wa enzi za Helmut Kohl kuhakikisha na mataifa madogo pia ya umoja wa ulaya yanatunzwa na hali ya kujiamini na kuwajibika Ujerumani katika majukwaa ya kimataifa kama ilivyokua katika enzi za Gerhard Schröder .Kwa namna hiyo pia inaweza kujitokeza Ujerumani inayofuata msimamo wa wastani.“
Tuigeukie mada ya pili sasa:Kashfa ya nyama iliyooza inazidi kuenea nchini Ujerumani.Mnamo siku za hivi karibuni tuu,tani mia kadhaa za nyama iliyooza zimegunduliwa utafiti ulipofanywa katika mashirika kadhaa katika majimbo chungu nzima ya Ujerumani.Gazeti linalosomwa na wengi mitaani mjini Cologne-EXPRESS limehamakishwa sana na kashfa hiyo na linaandika:
„Nyama iliyooza inayonuka-inauzwa kama nyama iliyotoka machinjoni hii leo!Si hasha pengine watu wameila.Loo!Vitimbi vya baadhi ya mashirika katika sekta hiyo ya faida vinaekezeka kwa neno moja tuu:uhalifu.Lakini pia hakuna haja kuanzia sasa watu kuamua kula mboga mboga tuu.Kwasababu,licha ya yote hayo,ni mashirika machache yaliyosubutu kujitaajirisha kwa nyama iliyooza.Wakuonewa huruma hapo ni wakaguzi pia.
Gazeti la MANNHEIMER MORGEN linaandika:
„Mashindano makali ya kibiashara-hakuna kokote barani Ulaya ambako bei za vyakula ziko chini kama Ujerumani-hali hii inawafanya malaghai na wahalifu wafike hadi ya kuwauzia wananchi bidhaa zilizooza.Ni kitandawili kikubwa hichi,watu wanajiuliza kwanini madhamana hawaviandami kwa nguvu zaidi visa hivi vya uhalifu.Katika nchi ambako kila skurubu inayouzwa dukani na vipimo vyake vinachambuliwa,imekwenda kwendaje hata nyama iliyooza,nyama inayonuka uvundo ikafika katika meza ya vyakula „kama tunaweza kuviita safi.“Na inapogunduliwa,wanunuzi wanatulizwa nyoyo na kuhakikishiwa eti nyama hizo zilizooza hazina madhara kwa afya.Haya basi kitutamkie.