Yaliyoandikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo
1 Septemba 2005
Maoni hayo yamejitokeza pia katika uhariri wa gazeti la mjini Cologne, Kölner Stadt Anzeiger.Gazeti linaandika:
“Bila shaka hakufanya makusudi kansela Schröder,alipobainisha walakini iliyoko katika kampeni ya uchaguzi ya chama cha SPD.Chama hakina mkakati unaostahiki watu kuuvalia njuga.Ingawa hachoki Schröder kushadidia umuhimu wa kuendelezwa mageuzi.Lakini zaidi ya kutetea haja ya kuimarishwa matumizi ya aina mpya ya nishati na bima ya wananchi katika mfumo wa afya,SPD hawana jengine la kulitetea.
“Hata gazeti la München SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linahisi SPD wanashindwa kuona mbali. Gazeti linaandika:
“Gerhard Schröder alionekana akitoa hotuba kali kabisa,alishambulia ingawa kindani ndani hotuba hiyo ilikua ya kujitetea.Amechambua maovu ambayo SPD itazuwia yasitokee pindi wakishinda uchaguzi mkuu.Nini hasa wanapanga badala yake kufanya,hakusema.Na panapohusika na hali ya ndani chamani, basi jana ilikua mara ya kwanza watu kumuona kansela akivinjari kama vile mjini Berlin.”
Gazeti la Aachener Zeitung linajiuliza:
“Eti tangu lini mtu akazungumzia kitu ambacho hata wenzake chamani hawakiamini?Eti chama chao kiwe na nguvu zaidi na eti serikali ya muungano ya Nyekundu na Kijani iendelee kuwepo madarakani.Bila ya shaka hawatakosa kusema hivyo-kwasababu hawana njia nyengine.Kuzungumzia aina nyengine ya muungano ambao unaingia akilini ni miko kwa wasocial Democrats.Wasocial Democrats na walinzi wa mazingira Die Grüne wataweza tuu kuunda serikali kwa ushirikiano pamoja na chama kipya cha mrengo wa shoto.Oh,Oooo-Wala usikitaje hicho!Na muungano wa vyama vikubwa,yaani CDU/CSU na SPD,unawezekana lakini bila ya Gerhard Schröder.Balaa kubwa hilo kwa SPD:”
Gazeti la TAZ la mjini Berlin linaandika:
“Ni kichekesho kujidai kila kitu ni bam bam.Inadhihirisha zaidi wapi linakutikana tatizo lao kubwa ambalo hakuna yeyote chamani anaesubutu kulizungumzia kinaga ubaga.Ingawa Schröder bado anajivunia imani ya wananchi,lakini si mtetezi anaefaa kwa kampeni isiyofaa na mkakati usiofaa wa SPD.Wasocial Democrats hawakupaza sauti,Schröder alipowageuza mahabusi may 22 iliyopita .Wasocial Democrat wangependelea sana kuamini kile kilichokusudiwa katika mbinu hii mpya ya kansela :Mbinu hiyo iliyolenga kusababisha maajabu na kuyafanya yasiyowezekana yawezekane.Lakini mbinu hiyo imemgeukia na kudhihirisha kisiasa amefeli.Wananchi wameshaitambua hali hiyo na wanachofanya hivi sasa si chengine isipokua kuwapa wasacial Democrat kile wanachostahiki kupewa.Hakuna miujiza yoyote itakayoweza kuzuwia ukweli huo wa mambo usitokee.
“Gazeti la OSTSEE-ZEITUNG la mjini Rostock limeandika:
“Manung’uniko ya wasocial Democratic dhidi ya muongozo wa kampeni ya uchaguzi na muungano wa baada ya uchaguzi mkuu,hayeshi.Schröder ambae anashindwa kuwatanabahisha watu, si kwa sifa ya uongozi wake na wala si kwa sera zake za kutaka amani,anakabiliwa na kazi ngumu katika kampeni hii ya uchaguzi.Kampeni yake inalenga zaidi kuuwashambulia na kuwakosoa wa CDU/CSU na waliberali na kuashiria mabaya ya kutisha yatakayotokea pindi wakiingia madarakani.”
Gazeti la MITTELBAYERISCHE ZEITUNG la mjini Regensburg linasema:
“Tatizo kubwa katika hotuba hiyo kali iliyoshangiriwa ya Schröder sio pale anaposhambulia bali pale anapotoa picha ya kutisha ya mtetezi wa CDU/CSU bibi Angela Merkel.Kansela huyo mwenye bashasha na stadi anapozungumza na waandishi habari ,pengine amefanikiwa kuonyesha picha” afadhali zimwi likujualo.”Kansela amewakosha wafuasi wa chama chake.Lakini kama hali hiyo itaitikwa pia na wapiga kura ni suala jengine.”