yaliyoandikwa na magazeti ya Ujerumani hii leo
7 Februari 2006
Mgomo mkubwa kabisa uliotishwa na chama cha wafanyakazi cha VERDI pamoja na machafuko yaliyosababishwa na kuchorwa makatuni ya Mtume Mohammed ndizo mada zilizopewa umuhimu mkubwa na magazeti ya Ujerumani hii leo.
Mgomo mkubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa katika idara za huduma za jamii umeanza jana humu nchini.Maelfu ya wafanyakazi wa serikali za miji na mitaa hawajenda makazini mwao wakilalamika dhidi ya kurefushwa muda wa kufanya kazi toka masaa 38.5 na kufikia masaa 40 kwa wiki,pamoja pia na kupunguzwa mishahara yao.Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani yanatofautiana katika suala hilo.
Gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN kwa mfano limeandika:
„Hata kama Verdi itafanikiwa na waajiri kuridhia,litakua suala la wakati tuu hadi muda wa kufanya kazi utakapoenea hadi katika serikali za miji .Sio tuu katika shughuli za kiuchumi-hata katika huduma za jamii,watumishi wa serikali,wafanyakazi wepya au wale walipanda vyeo,suala hilo limeshakua la kawaida sasa.Kwa vyovyote vile iwavyo:Verdi imetereka katika mapambano bila ya kinga. Waajiri wana nguvu zaidi na wanaweza pia kuachilia mbali mipango yao,lakini Verdi inajikuta ikizidi kutiwa kishindo kila siku zinapopita.
Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG linaandika:
“Mapambano haya ya wafanyakazi ni yenye madhara,hayana mshikamano na hayana pia faida-achilia mbali kichekesho kwamba Verdi inataka sasa kulazimisha makubaliano ya kazi yatumike katika majimbo ,licha ya kushindwa katika serikali za miji.Migomo ina madhara,kwasababu inazifanya shughuli za kiuchumi zipooze na kuzorotesha ukuaji wa kiuchumi.Na kutokana na hali tete ya ukuaji wa kiuchumi,Ujerumani haiwezi kumudu balaa kama hilo.Mgomo hauna maana kwasababu makasha ya seerikali ni matupu na kila kitu kinastahiki kutiwa njiani ili kupunguza gharama.“
Gazeti la NEUE DEUTSCHLAND lina maoni tofauti na hayo.Gazeti linaandika:
„Ikiwa hakutazuka maajabu,basi sekta ya huduma za jamii nchini Ujerumani itajikuta ikitumbukia katika mzozo mkubwa wa kupimana nguvu.Sababu ya yote hayo,inakutikana bila ya shaka upande wa waajiri.Kwanza mawaziri wa fedha wa serikali za majimbo waliamua kujitoa katika majadiliano ya kuyafanyia marekebisho makubaliano kati ya waajiri na waajiriwa,wakaamua watumishi wa serikali za miji katika majimbo matatu ya shirikisho-waendeleze utaratibu uliofikiwa baada ya majadiliano makali-uamuzi ambao haukuleta tija yoyote na utaratibu wa kurefushwa muda wa kufanya kazi ukapingwa na serikali za miji.Jambo moja lakini ni dhahir katika mashindano haya ya kupimana nguvu:Kinyume na hali namna inavyokua katika soko huru la kiuchumi,hakuna yeyote anaeamini eti nafasi zaidi za kazi zitabuniwa kwa kurefushwa muda wa kufanya kazi katika sekta ya shughuli za serikali za miji na huduma za jamii.
Gazeti la OSTSEE-ZEITUNG la mjini Rostock linahisi:
„Serikali nyingi za miji na mitaa zinakabwa na shida.Mikopo iliyopindukia,nishati ghali kupita kiasi,na gharama zinazozidi za kuwahudumia jamii zinayafanya matumizi yazidi kua makubwa-katika wakati ambapo mapato yamepungua kutokana na idadi kubwa ya watu wasiokua na ajira na wakati huo huo mashirika kupunguziwa kodi za mapato .Pengo kati ya ufukara katika shughuli za huduma za jamii na utajiri wa mashirika ya kibinafsi linazidi kukua.Na madhamana wanabidi kulishughulikia suala hilo.Mgomo hautasaidia kulipatia jibu suala hilo.
Mada ya pili magazetini inahusu makatuni ya Mtume Mohammad yaliyochorwa katika magazeti ya Ulaya na kuzusha hasira katika ulimwengu wa kiislam.Mjini Teheran waandamanaji walioingiwa na ghadhabu walizishambulia kwa mawe na moto ofisi za ubalozi za Danemark na Austria.Mzozo huu umekua ukichambuliwa takriban kila siku na magazeti ya Ujerumani.
Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linahisi:
„Nchi za magharibi zitafanya vyema ikiwa hazitang’ang’ania hoja kwamba wao ndio wenye haki-hiyo isimaanishe kwamba hawana haki, hasha,bali tuu kwasababu kua na haki katika ulimwengu wa leo ,haisaidii kitu.La muhimu zaidi ni kujaribu kuendeleza msimamo wa wastani na kutuliza mambo.Na zaidi ya hayo mipango ya kuwajumuisha wageni katika maisha ya jamii katika nchi za magharibi,inahitaji pia kutangulizwa mbele.
Gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG linaandika:
„Kuvunjwa miko ni jambo lililokua likitokea kwa miongo kadhaa katika nchi za kidemokrasia za magharibi.Lengo lilikua kulifanya taifa lijikomboe toka taasisi za jamii zenye maguvu kupita kiasi.Upande huo watu wamefanikiwa.Na hiyo ndio maana nchini Danemark,hakuna aliyefikiria vyengine makatuni ya Mtume Mohammed yalipochorwa na kuchapishwa.Ulimwengu wa kiislam lakini haujaingia katika daraja ya ulimwengu wa kimambo leo.Maendeleo ya teknolojia ambayo ulimwengu wa magharibi unajivunia,yanaangaliwa kwa jicho jengine katika ulimwengu wa kiislam.