Yaliyoandikwa magazetini Ujerumani
14 Desemba 2005Uamuzi wa kutekeleza adhabu ya kifo dhidi ya Tookie Williams huko California umezusha lawama katika kila pembe ya dunia.Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanaiangalia adhabu ya kifo kua ni utaratibu wa kale,usioambatana na ubinaadam,hasa kwa kuzingatia kadhia ya Williams.Mbali na hayo wahariri wametupia jicho uamuzi wa mahakama kuzuwia mgomo uliopangwa kuitishwa na madaktari humu nchini.
Gazeti la BERLINER KURIER linahisi taifa la kistaarabu kuliko yote mengine ulimwenguni linafuata mtindo wa kale kabisa wa kutoa roho.Gazeti linaandika:
„Katika suala hili Marekani inajikuta kundi moja na yale mataifa ambayo viongozi wa mjini Washington wanapenda kuyaita mataifa ya „mhimili wa maovu.“Si jamii ya kuvutia.Schwazenegger amewaridhisha wale wanaounga mkono adhabu ya kifo jimboni mwake.Lakini Williams amebadilika na kuwa mtu mwengine kabisa baada ya miaka 24 katika chumba cha jela cha kusubiri mauti.Kwa mantiki hiyo ,kuuliwa kwake ni sawa na mauwaji ya kiikatili yaliyoshawishiwa kisiasa.“
Kwa maoni ya OFFENBACH-POST adhabu hiyo ya kifo ni kinyume na sifa inayojipagaza Marekani.Gazeti linaandika:
„Ndio adhabu ya kifo ni kinyume na ubinaadam,ni ushenzi-sawa na mauwaji.Dola lakini linalotanguliza mbele adhabu hiyo wakati huo huo lakini likijinata kama muasisi wa haki za binaadam na kujigamba linapigania yaliyo mema kote ulimwenguni,haliwezi kamwe kuaminika.Kama tujuavyo hoja kwamba adhabu ya kifo itachangia kuwatisha watu wajiepushe na matumizi ya nguvu,hakuna anaeziamini.Kwa hivyo adhabu hiyo ya kifo haiwezi kuangaliwa kama adhabu inayostahiki –badala yake mtu anaweza kuilinganisha na kitendo cha kikatili kabisa cha kulipiza kisasi.“
Gazeti la mjini München TZ linasema adhabu hiyo ya kifo haikua na maana yoyote.Gazeti linaandika:
„Historia ya Tookie Williams pekee ni funuzo dhidi ya adhabu ya kifo.Alikamatwa akiwa na miaka 26,na kubadilika moja kwa moja katika kipindi cha miaka 25 aliyokua akisubiri kuuliwa.Asili mia moja tuu ya waliouwa ndio wanaohukumiwa adhabu ya kifo-na mara nyingi wahusika ni watu masikini na weusi;na kati ya watu elfu moja na mmoja waliouliwa kufuatia adhabu hiyo, 450 kama si zaidi imekuja gunduliwa baadae haweakua na hatia.
Gazeti la LANDESZEITUNG la Lüneburg linaleta uwiano kati ya adhabu hiyo ya kifo na kushikiliwa katika jela za siri za CIA magaidi watuhumiwa.Gazeti linaandika:
„Tabu na shida alizokumbana nazo Stanley Williams alipokua akipambana na mauti na dhana zinazozidi kupata nguvu za kuwepo utaratibu na vituo vya mateso vya CIA-ni pande mbili za medali moja tuu.Dola kuu la Marekani linajitenganisha na maadili ya nchi za magharibi.Ikiwa huko Texas,mkono wa mhalifu utapunguswa kwa dawa kabla ya kudungwa sindano ya sumu,hicho si chochote chengine isipokua dhihaka tuu.Ukweli ni kwamba marekani inajiweka mstari mmoja na nchi kama China na Saud Arabia zisizochelea kuwapiga risasi au kuwanyonga watu hadharani.