Yaliyoandikwa magazetini Ujerumani hii leo
8 Februari 2006
Wanasiasa wa vyama vyote vya Ujerumani wameelezea hofu zao kutokana na kuzidi makali maandamano katika ulimwengu wa kiislam dhidi ya makatuni yanayomdhalilisha Mtume Mohammad. Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya mambo ya nchi za nje,serikali kuu ya Ujerumani inataka watu wajiepushe na kila linaloweza kupandisha mori.Magazeti ya Ujerumani hii leo yanajaribu kukichambua kizungumkuti hiki.
Gazeti la “Der NORDKURIER “ la mjini Neubrandenburg linaandika:
„Vipi wimbi hili la machafuko linaweza kuzuwiliwa?Kansela Angela Merkel ameshauri watu wazungumze.Na hajakosea kushauri hivyo.Guido Westerwelle,amekuja na fikra iliyokosolewa na washirika katika serikali ya muungano wa vyama vikuu aliposhauri misaada ya fedha isitishwe.Hakukawia kukosolewa anataka kujipendekeza tuu-bila ya kufikiria kwamba hali hiyo inaweza kuzidisha makali.Lakini na yeye pia, kiongozi huyo wa FDP, hajakosea.Utayarifu wa kuketi na kuzungumza pamoja na kunyosheyana mikono kwaajili ya amani ni jambo moja na misaada nono ya fedha ni jambo jengine.Jirani anapofanya fujo na kutishia atauwa,watu wanafanya tahadhari na kuanza kujisalimisha.Haimaanishi lakini kwamba watu hawataaendesha juhudi za kutaka kusuluhu .Lakini yeyote yule anaetishia kuangamiza maisha ya wengine,hastahiki hata akidogo kupewa bahashishi ya fedha ambazo pengine atazitumia kununulia silaha.“
Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG linaandika:
„Kususiwa rasmi bidhaa za Danemark inamaanisha kuzidi makali mzozo;kwasababu kwanza kamisheni kuu ya Umoja wa ulaya mjini Brussels katika juhudi za kutaka kutuliza mambo,ilikwisha onya dhidi ya hatua kama hiyo.Na sababu ya pili ni kwamba Iran kwa kufanya hivyo inataka kuutia kishindo umoja wa ulaya ili kujipiga kifua baadae kujifakharisha.Ni sawa kabisa kuwaona wanasiasa wa ulaya ,kutokana na“ wimbi la malalamiko“ wakitoa mwito watu wafanye busara na kujadiliana.Lakini kama mwito huo haujaitikwa je ,itakuaje?“
Gazeti la EßLINGER ZEITUNG linashauri ifuatavyo:Gazeti linaandika:
„Hakuna misingi ya pamoja kati ya Ukristo na Uislam linapohusika suala la haki ya binaadam alihoji mwaka 1996 mtaalam wa masuala ya kisiasa wa Marekani Huntington.Kuishi pamoja waislam na wakristo katika nchi za magharibi ni ushahidi timamu kwamba hoja zake hazina msingi,licha ya matatizo yote yanayokutikana katika juhudi za kuishi pamoja wageni na wenyeji wao.Watu wakitaka kweli kuepukana na balaa la mapambano ya Utamaduni,basi watu wanaoishi katika „dunia moja“watalazimika kulipatia jibu suala la „uhuru wa matumizi ya nguvu na utayarifu wa kujadiliana.Na wale wanaofuata misimamo ya wastani katika ulimwengu wa kiarabu ndio wanaobidi kuchangia zaidi katika kulipatia jibu suala hilo.“