Yaliyoandikwa magazetini nchini Ujerumani
15 Februari 2006
Makampuni kadhaa ya gesi nchini Ujerumani yanataka kuwarahishia wateja, kuanzia April mosi ijayo waweze kufunga mikataba na wahudumu wengine wa gesi wakitaka.Uamuzi huo umepitishwa na makampuni sabaa ya gesi.Maoni ya wahariri yanatofautiana lakini.
Gazeti la NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG linaandika:
„Kuregeza kamba kwa ghafla makampuni hayo ni hatua moja mbele kuelekea mashindano zaidi ya kibiashara na ni ushindi pia,japo haba kwa wanunuzi.Ni wa pili lakini,baada ya wahudumu, wiki kama mbili hivi zilizopita,kukubaliana na taasisi zinazoshughulikia biashara ya gesi , raia wa kawaida wawe huru kujitafutia mashirika yanayouza gesi kwa bei rahisi kuanzia october.Kwa hivyo hivi sasa wanaweza kujitafutia mashirika hayo mapema zaidi.
Gazeti la SCHWARZWÄLDER BOTE la mjini Oberndorf linauangalia kwa jicho la hofu uamuzi huo.Gazeti linaandika:
„Matumaini ya kupatikana bei hafifu zaidi yako mbali kufikiwa.Kwasababu bado biashara ya gesi inadhibitiwa na taasisi maalum-na bila ya shaka kuna mzigo wa ada zinazobidi kulipwa na ambazo taasisi hizo zisingetaka kuubeba.Shirika la gesi la E.ON halijakawia kudai eti faida iliyopata haijapindukia asili mia moja.“
Hata gazeti la Allgemeine la Mainz linashuku kama kweli bei zitashuka na linajaribu kulinganisha,na kuandika:
„Ukitupia jicho soko la nishati tuu unatosheka.Soko hilo limefungua milango yake tangu muda mrefu uliopita,lakini raia wa kawaida hawakufaidika.Kwa muda wote ambao mabwana wanaodhibiti biashara hiyo wataendelea kushikilia bei na masharti yasiyovutia,kwa muda wote ambao mashirika machache yatakua yakipeyana biashara hiyo,hakuna kitakachobadilika.
Gazeti la mjini Cologne,Kölnische Rundschau linahisi:
„Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya makampuni ya mafuta Ulf Böge na mkuu wa taasisi ya shirikisho inayosimamia masuala ya nishati Matthias Kurth wanajitahidi kuona bei ya gesi inapungua.Hakuna anaeweza kubisha.Hata hivyo mkondo wa mambo katika soko la gesi hautabadilika haraka hivyo,sio April na wala si october.Pande zote mbili zitabidi kwanza ziendeleze majadiliano pamoja na makampuni yanayouza nishati hiyo,juu ya namna ya kusimamiwa gharama na ada zinazotokana na biashara hiyo.
Mada ya pili magazetini inahusu kutuwama shughuli za kiuchumi katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho ya mwaka 2005.Pato la ndani kwa kipindi hicho halijabadilika ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka mmoja kabla.Idara kuu ya takwimu inahisi hakuna haja ya kutia chunvi.Lakini wahariri wa magazeti wanaitumia hali hiyo kuitia kishindo serikali kuu.
Gazeti la PFORZHEIMER ZEITUNG linaandika:
„“Eti uchumi umeanza kukua baada ya uchaguzi mkuu-hakuna chochote!“Kinyume na matarajio ya wengi na matumaini , baada ya kushindwa serikali ya rangi Nyekundu na Kijani,hali ya kiuchumi ingeanza kunawiri,matumaini hayo yamefifiishwa na takwimu za robo ya mwisho ya mwaka jana.Lakini cha kustaajabisha kipi kama watu bado wanaigeuza senti mara mbili kabla ya kuamua kuitumia?Hakuna.Hata serikali ya rangi Nyeusi na Nyekundu haijafanikiwa hadi sasa kuwaondoshea wasi wasi wananchi.
Mhariri wa gazeti la FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND ana maoni tofauti na hayo.Anaandika:
„Mwanzo,ukiziangalia takwimu hizo utahisi kweli hazilingani na makadirio ya kutia moyo ya wiki zilizopita.Lakini takwimu za robo mwaka za pato la ndani pekee hazitoshi kupima mkondo wa ukuaji wa kiuchumi.Takwimu hizo zinapingana na hali jumla inayoashiria matumaini mema ya kiuchumi.
Gazeti la MITTELBAYERISCHE ZEITUNG linahisi:
„Yote kenda,kumi itagonga mwaka 2007.Hapo ndipo itakapodhihirika kama makadirio ya ukuaji wa kiuchumi yatapata nguvu na kuimarika au yatafifia.Kwasababu pekee kodi ziada itakapopandishwa-wanunuzi watapungukiwa na Euro bilioni 20 mifukono mwao.