Yaliyoandikwa magazetini nchini Ujerumani
8 Machi 2006Tuanze lakini na uwezekano wa kutumwa wanajeshi wa Umoja wa ulaya katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.Gazeti la AUGSBURGER ALLGEMEINE linashuku mpango huo,na linaandika:
„Hata kama dhamiri na nia ni nzuri,lakini tume ya Umoja wa Ulaya ya wanajeshi wasiozidi 1500,kila mmoja anaibisha.Kwa sababu tume hiyo ni ndogo mno kuweza kusimamia amani katika nchi kubwa kama hiyo inayosumbuliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.Badala ya kutumwa wanajeshi wa kizungu,ingekua bora kama Umoja wa Afrika ungewajibika kulinda amani.“
Gazeti la mjini Bonn,General Anzeiger linajiuliza:
„Watawezaje wanajeshi wasiozidi 1500 ,watakaowekwa katika mji mkuu tuu wa nchi hiyo iliyofilisika na kuteketezwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe ,kudhamini utulivu na nidhamu miezi minne tuu kabla ya uchaguzi?
Muhali,haiwezekani hasa kama vikosi hivyo vinabidi vitumwe wiki chache kuitoka sasa na hadi dakika hii hakuna ajuaye nchi gani itachangia wanajeshi wangapi , vikosi hivyo vya umoja wa ulaya vitaongozwa na nani,vinakwenda wapi na kufanya nini.“
Gazeti la MÄRKISCHEN ODERZEITUNG linazungumzia uwezekano wa kushirikishwa jeshi la shirikisho Bundeswehr.Gazeti linaandika:
„Bundeswehr haiwezi kuingilia kila mahali-kinyume na vile madhamana wa kisiasa mjini Berlin wanavyoamini.Umoja wa Ulaya unabidi utathmini vyema uwezo wake.Bila ya Marekani hakuna lolote litakalotendeka katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo-lakini wao wameshakataa.Kimoja ni dhahiri, opereshini inayotajwa eti ya kusimamia uchaguzi,haiwezi kuzuwia mauwaji .“
Gazeti la mjini Cologne,Kölnsiche Rundschau linahisi:
„Hajakosea waziri wa ulinzi wa Ujerumani anapolizungumzia kwa tahadhari suala hilo.Tangu miaka kadhaa hivi sasa jeshi la shirikisho Bundeswehr limekua likitumika mtindo mmoja katika eneo la Balkan,pembe ya Afrika na Afghanistan.
Kimoja lakini hakijadhukuriwa hapo jana:Kikosi kidogo kama hicho,kitakachowekwa katika mji mkuu tuu,hakiwezi kuleta amani katika nchi kama hiyo iliyoteketea.Hakuna la ziada isipokua pengine ushahidi kwamba Ulaya haikulisahau bara la Afrika.
Gazeti linalochapishwa mjini Ulm, SÜDWEST PRESSE linahisi:
„Ni changamoto kubwa hii na wanasiasa wa Ulaya hawajakosea wanaposita sita.Hata hivyo lakini,sote tunajikuta tukihuzunika tunapoona yanayotokea katika nchi hiyo ya Afrika kati,na sio tuu kwasababu za kiutu.
Hatima ya wanaotaabika tunakabiliana nayo moja kwa moja wanapoanza kupiga hodi katika ngome za Ulaya huko Lampedusa,Mellila au Ceuta.Umoja wa ulaya kwa hivyo utafanya la maana ukijiunga na juhudi za kusaka ufumbuzi.
Mada ya pili magazetini inahusu bima ya uzeeni.
Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linaandika:
„Mjadala kuhusu malipo ya uzeeni umegubikwa na hofu za kila aina.Hofu hizo lakini utakuta mara nyingi ni za kubuni na hazina msingi.Watu wanahofia umasikini wakiwa wazee.Lakini ukweli wa mambo ni mwengine kabisa:Watu wengi waliostaafu humu nchini hali zao za maisha si mbaya-hayo yamedhihirika kutokana na uchunguzi uliofanywa.
Umaskini wa uzeeni ni nadra sana kushuhudiwa nchini Ujerumani,ikilinganishwa na Uengereza kwa mfano inayosifiwa kama mfano mzuri wa kuigizwa.Nchini humo wanaojikuta zaidi katika hali ya umasikini ni vijana;wanawake wanaolazimika kuwalea watoto wao peke yao,wanaume ambao hawana ajira au vijana ambao hawakupata mafunzo ya kazi.
Gazeti la NEUE RUHR/NEUE RHEIN-ZEITUNG la mjini Essen linaandika:
„Franz Müntefering atakapotangaza ripoti yake ya mwaka hii leo,umri wa kustaafu hautakua tena siri,kila mmoja anajua tangu muda sasa kwamba mtu atastaafu akiwa na umri wa miaka 67 na sio tena miaka 65.Watu wameingiwa na wasi wasi na kuzusha lawama hata ndani ya chama chake cha SPD.Mjadala unabidi uanze tangu sasa hasa kuhusu mustakbal wa ajira na malipo ya uzeeni.