Yaliyoandikwa magazetini nchini Ujerumani hii leo
27 Aprili 2006Duru ya nane ya mazungumzo ya serikali kati ya Ujerumani na Urusi inaendelea katika mji wa Tomsk,katika jimbo la Urusi la Syberia.Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamechambua mazungumzo hayo na kumulika uhusiano kati ya nchi hizi mbili.Mada nyengine magazetini hii leo ni kuhusu mashtaka ya jiji la Berlin mbele ya korti kuu ya katiba,kudai ipatiwe fedha zaidi kutoka serikali kuu.
Gazeti la WIESBADENER KURIER linahisi washirika hawako sawa katika mazungumzo ya Tomsk kati ya Ujerumani na Urusi .Gazeti linaandika:
“Urusi imepata nguvu chini ya uongozi wa Putin;haijiangalii hata kidogo kua mshirika wa kimkakati,au mshirika pekee wa Ujerumani na Ulaya.Moscow inajilinganisha zaidi na dola kuu,linalostahiki kutetea kwa kila hali masilahi yake .Ujerumani hapo ni karata mojawapo tuu japo kama ni muhimu,kutokana na nguvu zake za kiuchumi.”
Gazeti la Frankfurter Rundschau linachambua:
„Juhudi hizi mpya za kuimarisha uhusiano kati ya Ujerumani na Urusi zinastahiki kupaliliwa kwa dhati na ikihitajika basi chini ya misingi ya kuambiana ukweli.Putin, hasa katika suala la mashariki ya kati na Iran,haepukiki.
Suala juu ya muelekeo mpya wa siasa ya dunia,litategemea kwa sehemu kubwa mkondo wa mambo nchini Urusi.Na licha ya taharuki zilizosababishwa na kishindo cha gesi:maadhimisho ya miaka 20 ya msiba wa Tschernobyl,hayatakosa kushawishi mazungumzo ya Tomsk.Usalama wa nishati ni sababu inayoifanya Ujerumani ivutiwe zaidi na Urusi inayofuata utaratibu wa kidemokrasi.“
Gazeti la OST-THÜRINGER la mjini Gera linaandika:
„Merkel anabidi ajaribu kumjingelea rais Vladimir Putin mfano katika suala la mzozo wa Iran.Watu wasijidanganye.Urusi ni dola kuu.Sawa na Uchina,Urusi pia inapendele kufuata njia ya aina nyengine.Wao ni washirika wa Ulaya.Lakini wanapokukumbatiwa hukawii kujikuta na mabalanga.“
Gazeti la NEUE RUHR/NEUE RHEIN-ZEITUNG la mjini Essen linaandika:
„Uhusiano wa kisiasa pamoja na Urusi unatuwama katika fani ya diplomasia ya kiuchumi.Hesabu tuu ndizo zinazotiliwa maanani.Biashara ya pande mbili kwa mwaka uliopita wa 2005 ilifikia yuro bilioni 39 ,ikiongezeka kwa asili mia 24.
Hatuwezi kumudu kuitenga Urusi na hata kisiasa lisingekua jambo la busara.Gerhard Schröder amejitahidi kuonyesha hata chui anaweza kufugwa.Kansela Angela Merkel amejichagulia njia nyengine-Ushirikiano wa kimkakati.Ushirikiano-hapo tutakua tunatia chunvi,pengine usawa,hata kama bado haujafikiwa.“
Mada ya pili magazetini inahusu mashitaka wa diwani wa jiji la Berlin Klaus Wowereit mbele ya mahakama kuu ya katiba mjini Karlsruhe,akidai wapatiwe fedha zaidi kutoka serikali kuu.Maoni ya wahariri yanatofautiana katika suala hilo.
„Gazeti la LANDSHUTER ZEITUNG linakumbusha misaada ya serikali kuu kwa majimbo mengine,haikuleta tija iliyokusudiwa.Gazeti linaandika:
„ Kwa kutuma mashtaka mbele ya korti kuu ya katiba mjini Karlsruhe, Berlin imeitaja misaada ya fedha iliyowahi kutolewa na serikali kuu kuzisaidia Bremen na Saarland.Lakini fedha hizo,yuro bilioni 15 zilitolewa katika wakati ambapo bajeti ya serikali kuu haikua duni kama hivi sasa.Na zaidi ya hayo shabaha zilizokuwa zimewekwa,hazijafikiwa.Bremen inadaiwa zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote mwengine.
Ikiwa mabilioni yatatolewa kwaajili ya kuisaidia Berlin,lazma yafungamanishwe na masharti magumu.Kama vile kwa mfano kupatiwa serikali kuu usemi pia katika suala la maamuzi ya fedha ya Berlin na kadhalika.