Yaliyoandikwa magazetini hii leo nchini Ujerumani
20 Desemba 2005Gazeti la Berliner Zeitung linahisi:
„Kamati maalum iliyoundwa kukishughulikia kisa cha kutekwa nyara Susanne Osthoff na madalali waliendesha shughuli zao kisiri siri wakilenga zaidi kile walichokikusudia..Serikali ya kansela Angela Merkel imeutatua mtihani wake wa mwanzo kistadi kabisa…Susanne Osthoff,bibi mwenye kumiliki paspoti ya kijerumani,amepatiwa huduma zote anazozihitaji na hata zaidi kutoka kwa madhamana wa ofisi ya ubalozi wa Ujerumani.Ni jambo la kutia moyo kujua kuna chombo madhubuti kinachoweza kumsaidia mtu anapohitaji msaada-hata kama ni mtu mmoja,bila ya kujali jambo gani limemtumbukiza katika balaa hilo.Hakuna anaeweza kusema,kamwe balaa kama hilo halitomfika.Maisha yana mikasa,kuna yale ambayo mtu hakuyategemeya,ya kusisimua na mengine ya kusikitisha pia.
Gazeti la Berliner Kurier lina hoja sawa na hizo,Linaandika.
„Mtu hakua akisikia sana seuze mengi kuhusu kamati hiyo maalum ya kushughulikia mzozo iliyofanya kila la kufanya ili Susanne Osthoff aachiwe huru.Baada ya wiki tatu kupita,mabibi na mabwana wa kamati hiyo wamefanikiwa na habusi amesalimika.Wamefanya kazi nzuri kupita kiasi tena bila ya kuhanikiza.Hawakuendesha shughuli zao kwa fujo wala kujionyesha.Ni mashujaa wasiopenda makubwa.Hata kama baadhi ya wakati palihitajika maelezo kuhusu hali ya mambo namna ilivyo,lakini muhimu zaidi sio jibu la suala imekwenda kwendaje,bali kujua hatimae mtaalamu huyo ameachiwa huru.“
Gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG lina shaka ashaka na kuandika:
„Bado si dhahiri nani wa kushukuriwa.Jee balozi wa Ujerumani mjini Baghdad ndie aliyechangia kutokana werevu wake wa kujadiliana,kuachiliwa huru Susanne Osthoff? Jee mawasiliano pamoja na wateka nyara yamewezekana kupitia ukoo wa familia ya mtalaka wake?Na wamarekani jee,wamechangia kwa namna yoyote ile au vipi?Baadhi ya masuala haya pengine hayataweza abadan kujibiwa kwa uhakika.Kilicho dhahir ni kwamba serikali ya kansela Angela Merkel imefanikiwa kwa fahari kuufumbua mtihani wake wa kwanza na mgumu kupita kiasi.Waziri wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinmeier amedhirika kama stadi wa kuitatua mizozo.Kamati aliyoiunda imefanya kazi ipasavyo.Sifa hizo zimemjilia Steinmeier wakati muwafak kabisa.Zinafunika angalao kwasasa madhambi ya siku za nyuma.
Na gazeti la ABENDZEITUNG la München linaandika:
„Kuna kimoja kinachotofautisha mada hii ya sasa na zote zile zilizopita:Nacho ni kwamba juhudi za kutaka aachiliwe huru Susanne Osthoff na dereva wake zimepata uungaji mkono mkubwa hasa katika ulimwengu wa kiislam.Hali hii inatufanya tufikirie upya,mtu anapotaka kutuhadaa eti dini ya kiislam na ulimwengu wa magharibi ni kambi mbili zinazohitilafiana.Pengine kisa cha Susanne Osthoff kimesaidia kuufanya upeo wa macho kuona mbali zaidi katika suala hili.“
Tuigeukie mada nyengine sasa.Magazeti mengi ya humu nchini yamejishughulisha na hotuba ya hivi karibuni ya rais George W. Bush kuhusu siasa yake kuelekea Irak.
Gazeti la NORDKURIER linalochapishwa NEUBRANDENBURGE linaandika:
„Niaminini“! George W. Bush heshi siku hizi kuwaomba wamarekani,kile ambacho yadhihirika hawako tayari kumkubalia.Niaminini,ni muhimu kweli kusalia Irak hadi ushindi kamili utakapopatikana.Niaminini,vituo vya siri vya CIA na mitindo ya kutatanisha ya watu kuhojiwa,ni njia ya kujikinga dhidi ya magaidi.Niaminini,ile sheria inayoruhusu raia wa nchi hii kuchunguzwa kisiri siri na shirika la upelelezi la NSA ni muhimu katika kuwaandama watuhumiwa .Hata ndani ya chama chake mwenyewe,kuna wanaoshuku kama George W. Bush anastahiki kweli kuaminiwa.
Na hatimae gazeti la Handelsblatt la mjini Dusselsdorf linajiuliza juu ya matokeo ya uchaguzi wa bunge la Irak kwa siasa za Ujerumani.Gazeti linaandika:
„Kwa kuchaguliwa bunge jipya mjini Baghdad,linazidi pia kupata nguvu suala la misaada ya Ujerumani kwa Irak.Na hasa pale serikali huru ya Irak itakapotoa maombi kama hayo ya kupatiwa misaada.Ikiwa makadirio ya mwanzo mwanzo toka vituo vya upigaji kura ni ya kuaminika basi hatakosea mtu akisema bunge jipya la Irak litawakilisha jamii zote za nchi hiyo.Ikiwa serikali mpya mjini Baghdad itakua kama hivyo,hapo serikali ya Ujerumani italazimika kufikiria upya jinsi ya kuiangalia serikali halali kama hiyo.Angela Merkel atalazimika kuitumia kila fursa itakayopatikana na kuwajibika ,bila ya kuutia ila msimamo wa Ujerumani unaopinga vita nchini Irak…