Yaliyoandikwa magazetini hii leo nchini Ujerumani
28 Septemba 2005
Walinzi wa mazingira wanaingia katika bunge lijalo wakiwa na viongozi wawili wepya:Renate Künast na Fritz Kuhn ndio watakaoongoza kundi la wawakilishi wa walinzi wa mazingira bungeni.Wote wawili wameshasema ,wanataka chama chao kiwe mbele kabisa miongoni mwa vyama vya upande wa upinzani bungeni.
Kuhusu mada hiyo gazeti la FRNKFURTER RUNDSCHAU linaashiria:
“Yatakua mapambano ya kukinusuru chama chao kisipoteze umuhimu wake.Kwakua watajikuta wanabanwa kila upande,walinzi wa mazingira Die Grüne wanabidi wajihakikishie nafasi yao katika upande wa upinzani.Joschka Fischer aliwika huko wakati mmoja.Wateule wepya ambao mtu anaweza kusema ni warithi wake wataweza tuu kujipiga kifua wakifanikiwa kukirejesha chama chao katika zile enzi za zamani za ulimi mkali .Kwa namna hiyo hata washirika wao wa zamani katika serikali ya muungano ya nyekundu na kijani,watakua wapinzani wao.Hata wao hawatowajali,sawa na vile ambavyo hawatomjali Joschka Fischer.
Gazeti la OSTTHÜRINGER ZEITUNG la mjini GERA linahisi hata ndani chamani walinzi wa mazingira wanakumbwa na mtihani.Gazeti linaandika:
“Tokea hapo chama hicho hakipendelei sana makubwa”.Ndio maana,baada ya enzi za Joschka Fischer,watu wametanguliza mbele haiba ya Künast .Lakini amewekewa Kuhn,ili kuhakikisha mambo yanakwenda barabara.Si hasha kuwaona wakuu wa chama Roth na Bütikofer wakishusha pumzi.Kwasababu angeshindwa katika kundi la wabunge,basi Künast bila shaka angejaribu bahati yake katika uongozi wa chama.Katika upande wa upinzani ambako hakuna mengi ya kugawana,kinachohitajika zaidi ni kusimama kidete na kushirikiana.Na sifa hizo wanazo Kuhn na Künast pia.Waziri wa mazingira Jürgen Trittin ameamua kukaa kando.Matokeo ya upigaji kura yamedhihirisha wenye nguvu ni nani.
Gazeti la Kölner Stadt Anzeiger linahisi siku za mbele kuna uwezekano mzuri wa kuundwa serikali ya muungano wa Nyesui na kijani.Gazeti linaandika:
“Sio lazma walinzi wa mazingira wabuni mkakati mpya,wanabidi wajiambatanishe tuu na hali mpya.Nyingi kati ya mada zao zitaendelea kuwepo.Miaka sabaa ya serikali ya muungano wa Nyekundu na kijani inawapa fursa walinzi wa mazingira kutafakari na kupima kama wakati haujawadia wa kushirikiana pia na wahafidhina wa CDU/CSU.Mada kama kwa mfano kuhifadhiwa maumbile,akiba,taifa salama,usafi wa mazingira ni miongoni mwa mada zinazowaleta pamoja walinzi wa mazingira na wahafidhina.Jaribio la kwanza la kuunda serikali ya muungano wa nyeusi na kijani,pengine litashuhudiwa katika jimbo la Baden-Württemberg ambako uchaguzi wa bunge unapangwa kuitishwa mwakani.Huko,itafaa akusema hapa,ndiko Fritz Kühn alikowahi mwaka 1990,kuzungumzia uwezekano wa kuunda serikali kama hiyo.”
Gazeti la WESTDEUTSCHE ZEITUNG la mjini Düsseldorff ,mtu anaweza kusema linashangiria hasa kukiona chama cha walinzi wa mazingira kikikalia viti vya upande wa upinzani na linaashiria pia uwezekano mzuri wa kushirikiana siku moja wahafidhina na walinzi wa mazingira.Gazeti linaandika:
“Ushirikiano wa nyekundu na kijani umeshapita.Lakini walinzi wa mazingira wanaweza kufufuka kama kura ya jana ilivyodhihirisha.Matumaini ya kuibuka toka upande wa upinzani na kugeuka nguzo muhimu ya serikali nchini Ujerumani ni makubwa.Mdhamini wa matumaini hayo ni Renate Künast.Jukumu lake kubwa litakua,mbali na kupigania masuala ya usafi wa mazingira,ni kushadidia pia huduma za jamii na hivyo kujiandaa kuingia katika serikali ya kwanza ya muungano wa nyeusi na kijuani katika historia ya majimbo ya Ujerumani.
Kuhusu serikali ya muungano katika daraja ya shirikisho,kati ya vyama vya kihafidhina na wasocial Democratic,gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limeandika:
“Kila kwa mara pande hizi mbili zimekua zikisema kiini cha muongozo wa serikali hakitakua sababu ya kushindwa kundwa serikali kuu.Matamshi makali yaliyokua yakitolewa wakati wa kampeni za uchaguzi,yanasahauliwa na kutangulizwa mbele uwiano.Si ndo ilivyokua hivyo katika kuufanyia marekebisho mfumo wa bima ya afya,hata maridhiano yakapatikana au vipi?Na katika mkutano wa kilele wa kubuni nafasi zaidi za kazi,si kuna pia masikilizano funali yanayoweza kusaidia?Pande zote mbili zimeahidi kufanaya busara.SPD kidogo kidogo inaanza kuregeza kamba linapohusika suala la kiti cha kansela.Sasa tutaona kama wahafidhina wataendelea kumng’ang’ania Angela Merkel,vita vya madaraka vitakapomalizika.