Yaliyoandikwa katika magazeti ya Ujerumani hii leo
5 Septemba 2005Nani amewatanabahisha zaidi wapiga kura katika mjadala wa jana usiku kwa njia ya televisheni kati ya kansela Gerhard Schröder na mpinzani wake bibi Angela Merkel? Fadhaa za madhamana wa Marekani katika kushughulikia maafa ya kimbunga Katrina na mkutano mkuu wa chama cha CSU ambapo Edmund Stoiber amechaguliwa kwa asili mia 93 “tuu” aendelee na wadhifa wake,ndizo mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.
Tuanze lakini na mjadala wa jana usiku kati ya kansela Gerhard Schröder na mpinzani wake Angela Merkel.Gazeti la RHEINISCHE POST la mjini Düsseldorf linahisi mshindi aliyetokana na mjadala huo ni wapiga kura.Gazeti linaandika:
“Haya,ndio ulivyomalizika hivyo kwa hivyo mjadala uliokua ukisubiriwa kwa hamu kati ya watetezi wawili wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.Kansela Gerhard Schröder na mpinzani wake Angela Merkel hawakufanyiana mzaha.Takwimu zimetolewa,mambo hakika yaliyotendeka yametajwa, lakini zaidi kuliko yote ilikua kuonyesha nani hasa amewatanabahisha zaidi mamilioni waliokua wakiangalia televisheni.Kwasababu,kwa vyovyote vile ,katika demokrasia ya vyombo vya habari,kinachotangulizwa mbele sio kile kilichosemwa bali jinsi kilivyosemwa.Na ingekua sio hivyo basi Schröder asingekua kansela.Jana kwa hivyo tumejionea awamu ya mwanzo.Ya pili itafuata September 18.Na japo kama maoni ya umma yanatofautiana siku hadi siku-hayawezi lakini kutosha kumuwezesha Schröder aendelee madarakani.Seuze tena ameshaahidi, kamwe hatokua tayari kuiongoza serikali ya muungano ya SPD-walinzi wa mazingira na mrengo wa shoto.Na Angela Merkel jee?Amejionesha kua bibi mkakamavu anaeweza kukabiliana na hali ngumu.Baadhi ya wakati akifika hadi ya kutabasamu.Lakini nani hasa ameibuka na ushindi kati yao? Bila shaka wapiga kura,waliojipatia maelezo wanayoyahitaji kuweza kuamua, licha ya yote yaliyoshuhudiwa katika televisheni.
Gazeti la Berliner Zeitung linahisi ni mamoja nani kashinda katika mjadala huo wa mabishano kwa njia ya televisheni kati ya Gerhard Schröder na Angela Merkel..Walioshindwa jana usiku linasema Berliner zeitung ,wanajulikana tangu mwanzo nao ni wapiga kura-raia waliolazimika kuondoka patupu,waliogeuzwa wanunuzi,watazamaji na kadhalika.Kusema kweli hakujakua na neno hata moja,sentensi wala fikra ambayo wapinzani hao wote wawili hawajaitamka mara dazeni kadhaa kama si mara mia kadhaa-limeandika gazeti la Berliner Zeitung.
Gazeti la Frankfurter Allegemeine linasema:
Hakuna atakaesubutu kusema wajerumani hawakujua nini na nani anasimama katika uchaguzi wa september 18 ijayo.Ni kansela ambae,kama alivyotamka mwenyewe,kundi lake halitaki tena kumfuata,lakini anataka kwa kila hali kuliongoza kundi hilo hilo,na ndio maana anapigania aruhusiwe kutawala tena.Kwa upande mwengine anakutikana mtetezi wa kike ambae kwa ukakamavu na werevu amefanikiwa kujiimarisha chamani.Kipi kitaamua hatima ya uchaguzi, hakuna asiyekijua na wapiga kura hawatokubali kusalitiwa.
Mada ya pili inahusika na maafa ya kimbunga Katrina.Gazeti la SCHWERINER VOLKSZEITUNG linaandika:
Tangu wiki sasa ulimwengu umejipatia sura mpya ya Marekani:Vurumai,vifo na uporaji mali.Binaadam waliokata tama,wanaosubiri wasaidiwe.Polisi wasiojua nini cha kufanya,jeshi lililoduwaa likitumbuliana macho na madhamana wasiokua na maarifa hata kidogo.Imani gani inaweza kujipatia serikali ambayo makadirio yake mabaya yameshagharimu maisha nchini Iraq ,serikali ambayo hata hivi sasa imedhihirisha, hata pakitokea maafa,inashindwa kuachana na umangi meza-kwasababu kinakosekana kile mbacho nchini Marekani kinajulikana kama “Leadership” au uongozi.”
Gazeti la LANDESZEITUNG la mjini Lüneburg linaongezea.
Ingekua suala hapo lilikua kuporomosha mabomu mahala Osama Ben Laden alikojificha,basi ikulu ya Marekani ingehitaji dakika tuu kuamua.Maguvu yote inayoyaonyesha ulimwenguni,nyumbani imedhihirika haina nguvu zozote.Baada ya kuzama New-Orlean,dola hilo lenye madaraka yaliyopindukia,linabidi sasa lijiulize,utulifu gani unaweza kuwepo katika taifa ambalo ingawa wengi wa wananchi wake wanaruhusiwa kumiliki silaha,lakini wengi pia wanashindwa kupata elimu na huduma za afya?
Tumalizie yaliyoandikwa magazetini hii leo kwa mkutano mkuu wa chama cha CSU mjini Nürmberg ambapo kama magazeti yanavyosema, kiongozi wa chama hicho,waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Edmund Stoiber amechaguliwa kwa asili mia 93 tuu aendelee kukiongoza chama hicho.Gazeti la MAIN-ECHO linaandika:
“Si uasi dhidi ya Stoiber,lakini bila shaka ni onyo.Kongozi huyo na kundi lake lote katika halmashauri ya uongozi hawana tena raha.Watu wanaonya hata chama cha CSU chenyewe kiko hatarini.Wanasiasa wa mabaraza ya miji wanahisi wanatiwa kishindo na wenzao wa mjini München.Manung’uniko kuna kwa mfano “Wanasiasa wa hali ya juu “ au hata “wanasiasa wa tabaka maalum” yameenea miongoni mwa wanachama wa kawaida.Na hakuna anaefurahia hali hiyo.