yalioandikwa katika magazeti ya Ujerumani hii leo
10 Mei 2005Kuhusiana na kumbukumbu za mjini Moscow,gazeti linalochapishwa mjini München-Tageszeitung limeandika:
„Jinsi vyombo vya habari vilivyoripoti kumbu kumbu za miaka 60 baada ya vita kumalizika,mtu alihisi kana kwamba ya zamani yanajiri upya.Ni vizuri,kwamba hata baada ya kupita miongo sita,hakuna kilichosahauliwa kuhusiana na miaka 12 ya kiza katika historia yetu.Kumbu kumbu na maadhimisho ni fursa ya kuanzishwa mijadala kati ya wazee na vijana kuhusu mambo ya ndani kabisa ya kifamilia ,sawa na masuala ya siasa muhimu za dunia.“
Gazeti la „Die Welt“ linahisi kuna utata na linaandika:
„Kwa upande mmoja ni jambo la kusisimua, kusikia watu wakishadidia uhusiano uliojengeka chini ya misingi ya suluhu kati ya wajerumani na warusi ,miongo sita tuu baada ya vita kumalizika.Kwa upande mwengine picha chungu nzimas za Stalin zinazoonyesha majisifu ya kile wakiitacho „zama za fakhari“ zinamfanya mtu awe na shaka shaka.Putin anakua na kigeu geu katika suala la yaliyotokea.Kwa upande mmoja anavunja miko na kujitokeza kwa madaha na ucheshi akisifu uhusiano mzuri uliopo pamoja na Ujerumani na kufika hadi ya kuutaja kua wa kirafiki.Lakini anapokabiliana na raia wenzake halai inakua nyengine kabisa.“
Gazeti la mjini Berlin,“NEUES DEUTSCHLAND“ linahisi maadhimisho ya mjini Moscow yanaashiria kweli suluhu.Gazeti linaandika:
„Kuporomoka umoja wa jamhuri za Usovieti,ni zahma ya karne kwa Putin na kwa wapinzani wake ni neema.Ingawa wananchi wa Umoja wa Usovieti ndio waliovuruga mikakati ya kivita ya Hitler.Ingawa idadi ya wahanga na mchango wa Soviet Union katika kuushinda nguvu ufashisti hauna mfano.Licha ya yote hayo lakini hakuna anaemini anaweza kufuga madubu wa Rashia,hata rais wa Marekani hawezi.
Kuhusu mchango wa Marekani ,gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limeandika:
„Marekani ni muanzilishi wa Ulaya,kwasababu ukombozi na utaratibu wa kueneza demokrasi barani Ulaya usingewezekana bila ya Marekani.Kwa hivyo shaka shaka juu ya mchango wa Marekani barani Ulaya,mamoja zinatokea Washington au Berlin,ni za hatari kwasababu zinadhuru umoja barani Ulaya.Funzo linalotokana na kushindwa pamoja na miaka nenda miaka rudi ya vita baridi ni kwamba Ulaya hawezi kuchagua mmoja kati ya wawili,kati ya Rashia na Marekani.“
Tugeukie mada nyengine sasa.Gazeti la Frankfurter Rundschau limejishughulisha na hofu pengine fedha zinazomiminwa na walipa kodi zitakua haba na hivyo kupelekea kuwepo kasoro katika bajeti ya serikali.Gazeti la Frankfurter Rundschau linaandika.
„Kwa kuchanganya katika chungu kimoja hatua za kupunguza kodi na kupunguza matumizi,serikali ilifikiria kuupa msukumo uchumi.Ufanisi lakini haujapaatikana.Serikali inaelekea kujibebesha mzigo mwengine wa madeni,ingawa gharama zilikua haba kuliko hali namna ilivyokua miaka mitano iliyopita.KInachotisha zaidi ni jinsi vitega uchumi vinavyozidi kupungua katika sekta za huduma za jamii.Hata marekebisho katika sekta hizo hayakusaidia kitu.Kitu kimoja kimejitokeza nacho ni kwamba serikali sio tuu inakumbwa na tatizo la kugharimia kama inavyodai mara nyingi,bali pia katika kujikusanyia fedha pia ni tatizo.“
Gazeti la COBURGER TAGEBLATT lina maoni tofauti na hayo,linaandika:
„Ikiwa mapato ya Hans Eichel hayatoshi,basi bopra apunguze matumizi.Katika kitita cha euro bilioni 250,kuna njia ya kutenga vijibilioni bila ya kupiga upatu.Yeyote atakaetaka kufunika kawa na kumwachia mwanaharamu apite, anajiharibia mwenyewe.“
Na hatimae mapigano yaliyoripuka upya nchini Afghanistan.Gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE linaandika:
„Kwamba Afghanistan haigongi vichwa vya habari magazetini kila kukicha,sababu ni moja tuu nayo ni kwamba mashambulio ya Irak yanagharimu maisha ya walio wengi zaidi kuliko huko.Lakini na huko pia hakuna ishara kwamba hali itaimarika. Marekani inakubaliana na rais Hamid Karzai hakuna njia nyengine isipokua vikosi vya kigeni kuendelea kuwepo nchini humo.Na zaidi ya hayo Afghanistan inasalia kua kituo cha masilahi ya Marekani kuelekea nchi kama vile Iran,Pakistan na katika eneo la kaskazini yanakokutikana mataifa tajiri kwa mafuta ,mataifa ya Usovieti ya zamani.Hakuna lakini chochote kinachoashiria ahadi ya ujenzi mpya wa nchi hiyo.