Xi na Kim waahidi kuimarisha uhusiano katika kikao Beijing
4 Septemba 2025Rais wa China Xi Jinping na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un wamekutana mjini Beijing na kuahidi kuimarisha urafiki wa jadi na ushirikiano kati ya nchi zao.
Mazungumzo hayo yalifanyika kando ya sherehe za kumbukumbu ya miaka 80 tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha serikali CCTV.
Xi alisisitiza kwamba urafiki kati ya Beijing na Pyongyang ni wa muda mrefu na hautabadilika licha ya mabadiliko ya hali ya kimataifa. Aliahidi kuimarisha ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi na kuendeleza mshikamano kati ya nchi hizo jirani.
Kim Jong Un, ambaye hajawahi kufanya ziara rasmi nchini China kwa kipindi cha miaka sita, aliwasili Beijing akiwa na binti yake mdogo, hatua iliyoongeza uvumi kwamba anajiandaa kumrithisha uongozi.
Hii pia ilikuwa mara ya kwanza tangu achukue madaraka mwaka 2011 kushiriki kwenye hafla kubwa ya kimataifa pamoja na viongozi 26 wa dunia.
Ushirikiano wa kijeshi na Urusi
Mazungumzo haya yamefanyika siku moja baada ya Kim kushiriki gwaride la kijeshi la China sambamba na Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Putin alimpongeza Kim kwa ujasiri wa wanajeshi wa Korea Kaskazini wanaoshiriki katika vita vya Ukraine, ambapo Pyongyang imesambaza silaha na wanajeshi kuisaidia Moscow.
Uchumi wa Korea Kaskazini umedorora kutokana na vikwazo vikali vya Marekani vinavyohusiana na mpango wake wa silaha za nyuklia.
Wachambuzi wanasema ziara ya Kim Beijing inalenga pia kuongeza nguvu katika mazungumzo yanayoweza kufufuliwa na Rais Donald Trump, ambaye mara kadhaa ameonyesha nia ya kurejesha diplomasia na Pyongyang.
China, ambayo ndiyo mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara na mfadhili mkuu wa Korea Kaskazini, inataka jirani yake huyo kurejea mezani kwa mazungumzo na kusitisha kabisa mpango wake wa nyuklia.
Hata hivyo, uhusiano wa karibu kati ya Pyongyang na Moscow umeibua wasiwasi Beijing, ambayo imekuwa ikijitambulisha kama msuluhishi wa kimataifa.
Kuwepo pamoja kwa Xi, Kim na Putin katika gwaride hilo kumezua hisia kwamba kuna mpango wa ushirikiano wa pamoja wa kupinga shinikizo la Marekani.
Rais Trump alieleza wazi kupitia mitandao ya kijamii, akimtaka Xi kufikisha salamu zake kwa Kim na Putin "wanapopanga njama dhidi ya Marekani.”
Majibu ya Putin na mtazamo wa baadae
Putin, akizungumza na waandishi wa habari mjini Beijing, alipuuza madai hayo, akisema hakuna kiongozi yeyote aliyezungumza vibaya kuhusu serikali ya Trump katika mikutano yake.
Aliongeza kuwa Rais wa Marekani pia ana kipaji cha ucheshi, akionesha kutochukulia kwa uzito madai hayo.
Wachambuzi wanasema bado hakuna ishara kwamba kuna umoja wa wazi wa mataifa matatu haya.
Kwa mujibu wa Profesa Zhu Feng wa Chuo Kikuu cha Nanjing, "ushirikiano wa wazi na Korea Kaskazini unaweza kuharibu taswira ya China kimataifa, kwa sababu Korea Kaskazini inabaki kuwa taifa lililofungwa na lenye mamlaka ya kiimla zaidi duniani.”
Wakati Pyongyang ikitafuta msaada wa kiuchumi na Beijing ikitaka kuendeleza ushawishi wake, wachambuzi wanabashiri kuwa ushirikiano huu utabaki katika kiwango cha tahadhari.
Hata hivyo, ahadi za Xi na Kim kwamba urafiki wao hautabadilika, zinatoa ishara kwamba mustakabali wa uhusiano kati ya China na Korea Kaskazini bado utabaki kuwa nguzo muhimu katika siasa za Asia Mashariki.
Chanzo: AP