Xi na Putin waikosoa vikali mitazamo ya Magharibi
2 Septemba 2025Xi Jinping amewahutubia viongozi akiwemo Rais wa Belarus Alexander Lukashenko na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, akisema kuwa mfumo wa sasa wa uendeshaji wa dunia "unazidi kuwa wenye utata" akionyesha wasiwasi kuhusu mwelekeo wa mahusiano ya kimataifa yanayoongozwa na misingi ya upande mmoja.
Kiongozi huyo wa China amesisitiza kuwa dunia inakabiliwa na misukosuko na mageuzi makubwa, hivyo kuna haja ya kuendeleza ushirikiano wa pande nyingi unaozingatia usawa, kuheshimiana, na maendeleo ya pamoja.
Pia amekosoa kile alichokiita "tabia za uonevu" kutoka kwa baadhi ya mataifa—akimaanisha Marekani kwa njia ya mafumbo—na kusisitiza umuhimu wa kufuata mwelekeo wa SCO ili kuhakikisha amani na maendeleo ya kikanda.
Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin alitumia jukwaa hilo kutetea operesheni ya kijeshi ya Urusi nchini Ukraine, akizitupia lawama nchi za Magharibi kwa kuchochea mgogoro huo.
Mkutano huo wa kilele uliofanyika katika mji wa bandari kaskazini mwa China Tianjin umewaleta pamoja viongozi wa Urusi, China, India, Kazakhstan, Pakistan, Iran, Belarus, Tajikistan, Uzbekistan na Kyrgyzstan.
Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai SCO inalenga kukuza ushirikiano wa kiusalama, kiuchumi na kisiasa bila kuongozwa na misingi ya Kimagharibi.