Xi aonya dhidi ya vita vya kibiashara na Marekani
14 Aprili 2025Rais wa China Xi Jinpingameonya dhidi ya ulinzi wa kibiashara na vita vya ushuru, akisema havina mshindi na havisaidii maendeleo, wakati akianza ziara ya mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia.
Ziara hiyo, ya kwanza ya Xi nje ya nchi mwaka huu, inampeleka Vietnam, Malaysia na Cambodia, ikilenga kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kupunguza athari za ushuru mkubwa uliowekwa na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Soma pia:Trump atishia ushuru zaidi kwa China
Xi ameandika makala nchini Vietnam akisisitiza umuhimu wa kulinda mfumo wa biashara wa kimataifa na minyororo thabiti ya usambazaji.
Vietnam na China zina uhusiano wa karibu wa kiuchumi, lakini pia tofauti kuhusu Bahari ya Kusini ya China, ambapo Xi amesema migogoro inaweza kutatuliwa kwa mazungumzo.
Baada ya Vietnam, Xi atatembelea Malaysia na kisha Cambodia, ambayo ni mmoja wa washirika wakubwa wa China katika kanda ya Kusini-Mashariki mwa Asia, ambako Beijing imetanua ushawishi wake katika miaka ya karibuni.