WTO yalenga mageuzi kwa biashara huru na maamuzi rahisi
17 Julai 2025Shirika la Biashara Duniani (WTO) limeanza juhudi mpya za kuondoa mkwamo wa muda mrefu katika mazungumzo ya kibiashara ya kimataifa, ambayo yamepuuzwa kwa kiasi kikubwa tangu kurejea madarakani kwa Rais Donald Trump.
Hali hiyo imeongeza hofu kuwa shirika hilo linaweza kupoteza umuhimu wake, kulingana na nyaraka za ndani za WTO zilizoonekana na shirika la habari la Reuters.
Katika mazingira ambako ushuru wa Trump ulilazimisha mataifa kuingia kwenye mikataba ya pande mbili na Marekani, badala ya mfumo wa kimataifa wa pande nyingi, WTO imekuwa ikikumbwa na changamoto ya kufikia maamuzi kwa mujibu wa sheria ya makubaliano ya wanachama wote 166. Diplomasia ya sasa inalenga kuondoa hali ambapo mwanachama mmoja anaweza kuzima uamuzi wa wote.
"Uharaka wa hali hii unahisiwa na kuna mtazamo mpana kuwa hakuna njia mbadala ya kweli zaidi ya kufanya mageuzi,” alisema Balozi wa Norway katika WTO, Peter Olberg, aliyeteuliwa kuratibu mazungumzo hayo ya mageuzi.
WTO inafuata kanuni ya kimsingi ya "Most Favored Nation (MFN)” – inayohitaji wanachama wote kutendewa kwa usawa – lakini nchi zinazoendelea, zikiwemo China na India, zimepewa upendeleo maalum kusaidia ushindani wao wa kiuchumi. Trump aliwahi kupinga upendeleo huo akidai nchi hizo tayari ni mataifa yenye nguvu kiuchumi yanayoweza kujitegemea.
Moja ya nyaraka inaonesha kuwa wanachama wa WTO wanalenga kurahisisha mchakato wa maamuzi, kuhimiza sera za viwanda zenye usawa zaidi (ikiwemo ruzuku), na kupitia upya upendeleo wa nchi zinazoendelea.
Mvutano wa Marekani, China na India wajitokeza
Mapendekezo haya yanachochea mashauriano yatakayodumu hadi mwishoni mwa mwaka huu, kwa lengo la kutoa mwelekeo kwa Mkutano Mkuu wa Mawaziri wa WTO unaotarajiwa kufanyika Cameroon mwezi Machi. Mzunguko mpya wa mashauriano unaendelea wiki hii mjini Geneva.
Miongoni mwa mapendekezo ni kile kinachoitwa "Pareto improvement”, ambapo mjumbe mmoja mwandamizi kutoka China alisema kuwa ni pendekezo lao. Hatua hiyo itawalazimu wanachama wanaopinga pendekezo lolote kutoa ushahidi wa wazi na wa msingi wa madhara.
Mapendekezo mengine yanajumuisha kuruhusu baadhi ya wanachama kujiondoa kwenye maamuzi fulani na kuruhusu makundi ya nchi chache kusonga mbele na mazungumzo hata kama hakuna makubaliano ya jumla.
"Mfumo wa pande nyingi wa baada ya vita kama tunavyoufahamu umefifia,” alisema Roberto Azevedo, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa WTO kati ya 2013 hadi 2020, akionya kuwa majadiliano ya sasa ni suala la "kuwa au kutokuwa” kwa shirika hilo.
Kwa mujibu wa hati ya ndani ya WTO, Mkurugenzi Mkuu wa sasa, Ngozi Okonjo-Iweala, aliwasilisha msimamo wa Marekani kwa wanachama, akieleza kuwa njia ya "mageuzi kwa vitendo vidogo vidogo” ni "tupu” na haitatatua matatizo ya msingi ya kimfumo.
Katika ajenda yake ya biashara ya mwaka 2025, Marekani ilionya kuwa uvumilivu wake "umekuwa mdogo”na haitarajii mafanikio yoyote iwapo China na nchi nyingine kubwa – ikiwemo India – hazitakubali kupunguzwa kwa upendeleo wao.
China, kwa upande wake, mwezi Juni ilieleza kuwa imesikia "kila neno” kutoka Marekani na iko tayari kujadili suala hilo la upendeleo, pamoja na masuala ya ushuru na sera za viwanda. India haikujibu maombi ya maoni kutoka kwa Reuters.
Mazungumzo ya sasa hayajagusa bado mfumo wa utatuzi wa migogoro, ambao unatarajiwa kujadiliwa baadaye, kwa mujibu wa mojawapo ya nyaraka hizo.
WTO ilikataa kutoa maoni rasmi kuhusu makala hii, na Balozi Olberg hakuwa na tamko la ziada alipotafutwa na Reuters.