Wito wa kiongozi wa PKK wapokelewa tofauti
28 Februari 2025Wachambuzi nchini humo wanasema wito huo unaweza kuwa ndio chanzo cha kuwepo ukomo wa mihula anayoweza kutawala rais wa Uturuki.
Kumekuwepo na muitikio tofauti kufuatia wito huo. Baadhi wameukaribisha, wengine wameutaja kama hatua kuelekea amani, wengine wameukosoa wakisema ni kosa kubwa na wengine, wameukataa kabisa.
Soma Pia: Wito wa Ocalan wa kukivunja chama chake cha PKK wapongezwa
Mehmet Kaya mwenye miaka 54 amesema ni hatua nzuri na muhimu. Mfanya biashara huyu wa duka anayeishi kwenye jimbo la Batman anasema watu wana matumaini baada ya wito huu, kutafuata amani. Akasisitiza kwamba wanataka amani na utulivu.
Mstaafu Sadullah Bazyigit mwenye miaka 58, yeye anauelezea wito huo kwa mtizamo mpana wa kikanda. Amesema ujumbe huu sio tu kwa ajili ya Wakurdi na Waturuki, bali ni kwa ajili ya watu wa Mashariki ya Kati.
Mustafa Ogut, mkaazi wa jimbo la Nevsehir katikati mwa Uturuki amelikataa katakata pendekezo hilo akisema miaka iliyopita, waliwahi kuweka silaha chini lakini baadae wakaimarika tena. Akasema, hatua hii si sahihi.
Lakini Terkin Erturk, anayefanya biashara ya bima, huko Istanbul, kwenye wilaya ya Kadikoy amesema wito huu una mashaka makubwa, ingawa alikiri kwamba wanatamani kuwa na amani, utulivu, umoja na undugu na kutoa rai ya ugaidi kupingwa kwa kila hali nchini humo.
Wachambuzi wa siasa wana mashaka kuhusuana na nia ya serikali
Na wachambuzi wa masuala ya siasa kwa ujumla wao bado wanaonyesha mashaka kuhusiana na nia ya serikali ya Uturuki.
Ocalan ametoa wito huo wa kihistoria wa amani, lakini bado haiko wazi ikiwa Ankara ina dhamira ya dhati ya kupata makubaliano ama inataka tu kujinufaisha kisiasa, amesema Wolfango Piccoli, rais mwenza wa shirika linaloshauri juu ya hatari za kisiasa la Teneo.
Amesema, Rais Recep Tayyip Erdogan anakabiliwa na vizingiti vikubwa, katika wakati ambapo anahitaji kuungwa mkono na Chama cha DEM kinachowaunga mkono Wakurdi ili kupata kura za kutosha kwa ajili ya marekebisho ya katiba na kugombea tena kwenye uchaguzi ujao.
Emre Peker, mkurugenzi wa taasisi ya Eurasia inayomulika masuala ya Uturuki, ameandika kwenye barua yake kwamba Erdogan anaweza kuutumia wito huo wa Ocalan kuwashirikisha Wakurdi kwenye mchakato wa marekebisho ya katiba. Na kwa upande mwingine kulinda Haki za kitamaduni na lugha za Kikurdi.
Amesema ikiwa mazungumzo na Wakurdi yatakwama, kama ilivyotokea mwaka 2012-15, pengine Erdogan anaweza kuzidisha ukandamizaji wa kisiasa dhidi ya chama cha DEM, kinachounga mkono Wakurdi na kuanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya chama cha PKK, kilichopigwa marafuku nchini Uturuki ili kujiimarisha yeye mwenyewe.