Wirtz kukosa mechi ya ligi ya mabingwa na Bayern
10 Machi 2025Nyota wa Bayer Leverkusen Florian Wirtz atakaa nje ya uwanja kwa wiki kadhaa baada ya kupata jeraha la kwenye mkano wa kifundo cha guu la kulia, mabingwa hao wa Bundesliga wamesema Jumatatu katika taarifa.
Kiungo huyo kwa hiyo atakosa pambano la duru ya pili ya ligi ya mabingwa Ulaya, Champions, la hatua ya mtoano ya timu 16 bora dhidi ya Bayern Munich siku ya Jumanne, jambo ambalo ni pigo kubwa kwa Leverkusen.
Mabingwa hao wa Ujerumani wako nyuma goli 3-0 baada ya mechi ya duru ya kwanza wiki iliyopita. Wirtz aliingizwa uwanjani katika kipindi cha pili wakati Leverkusen walipocharazwa 2-0 na Werder Bremen Jumamosi iliyopita, lakini akachechemea nje ya uwanja baada ya dakika nane tu kufuatia madhambi aliyofanyiwa na Mitchell Weiser.
"Kukosekana kwa Florian Wirtz bila shaka kunatuathiri kwa kiwango kikubwa katika awamu hii ya msimu lakini nafasi yake tutaijaza na kikosi kilicho imara sana," alisema mkurugenzi wa michezo wa Leverkusen, Simon Rolfes.
"Tunamfahamu Florian na pia tunafahamu atarejea haraka iwezekanavyo. Kila mtu atamuunga mkono katika hilo. Tunachukulia kwamba atapona na kuwa tayari tena kucheza mechi za sehemu ya mwisho wa msimu," Rolfes aliongeza.