Wimbi la joto lasababisha maafa Ulaya
13 Agosti 2025Moto na moshi mweusi ulishuhudiwa katika kiwandakimoja cha simiti kilichoteketezwa na moto wa nyika katika mji wa Patras huko Ugiriki magharibi mwa Mji Mkuu Athens.
"Inaonekana kama siku ya kiama, Mungu atusaidie na awasaidie watu wa hapa," alisema Giorgos Karvanis, mkaazi wa Athens aliyesafiri hadi mji wa Patras kusaidia.
Mamlaka ziliwaamrisha wakaazi wa mji mmoja wenye wakaazi 7,700 karibu na Patras kuondoka sehemu hiyo na wakatoa onyo zaidi Jumatano wakiwashauri raia wa vijiji vingine viwili wayahame makao yao.
Katika visiwa vya Ugiriki vya Chios magharibi mwa nchi hiyo na Cephalonia katika eneo la magharibi, maeneo yote hayo yakiwa yanapendwa na watalii, mamlaka zimewataka wakaazi kukimbilia sehemu salama kwa kuwa moto unaendelea kusambaa.
Huko Uhispania, mtu mmoja aliyekuwa anajaribu kuzima moto alifariki dunia baada ya kuungua huku watu kadhaa wakijeruhiwa na kulazwa hospitali.
Mtu huyo mwenye umri wa miaka 35 alikuwa anajaribu kuzima moto katika mji wa Nogarejas eneo la Leon, ndipo aliponasa katika moto huo.
Haya yanafanyika wakati ambapo shirika la hali ya hewa nchini humo AEMET limetahadharisha kwamba karibu nchi nzima ya Uhispania iko katika hatari ya kukabiliwa na moto kutokana na joto kali.