WHO yaufungua mkutano wake wa 78 mjini Geneva
19 Mei 2025Kwenye ufunguzi rasmi wa baraza hilo la 78, viongozi wa ngazi ya juu walianza na uteuzi wa wajumbe wakuu hususan naibu mkurugenzi mkuu wa WHO kwa eneo la Afrika, Profesa Mohamed Janabi kutoka Tanzania, aliyekabidhiwa rasmi majukumu ya naibu mkurugenzi na kuahidi kuwa atawajibika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus aliwapongeza waliopewa majukumu mapya na kuwakumbusha kuwa shirika hilo linahudumu katika kipindi kigumu cha kupunguziwa bajeti, kwani wafadhili wa mataifa ya magharibi sasa wanawekeza hela zaidi katika ulinzi na wala sio msaada wa kibinadamu.
Mkutano wa mwaka wa WHO umeanza mjini Geneva
Kongamano hilo la siku 9 linajadili masuala mazito yakiwemo kuimarisha uwezo wake wa kifedha na jinsi ulimwengu utakavyoweza kuhimili athari za majanga yanayoibuka. Nchi wanachama zinatarajiwa kuridhia mpango wa kuongeza kiwango cha fedha wanachochangia kila mwaka kwa asilimia 20 kuunga mkono miradi ya WHO na kupunguza utegemezi kwa michango ya hiari ya serikali za nchi wanachama ambayo inafadhili nusu ya bajeti yake.
Mkutano unalenga kupitisha mikataba ya kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza
Wataalamu wamesema mpango mwengine unaotarajiwa kuridhiwa ni pamoja na kuwa na mkataba maalum wa jinsi ya kupambana na majanga ili kuepusha madhara kama ilivyotokea wakati wa COVID -19.
Wakati huohuo, ajenda hiyo itawawezesha kubadilishana sampuli za virusi kwa lengo la kuimarisha vipimo na hatimaye utengezaji wa chanjo mahsusi kwa mataifa masikini. Kulingana na mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros, mkataba huo utawawezesha kuwa na umoja na ushirikiano.
Marekani yatakiwa kutafakari upya uamuzi wake kuhusu WHO
Mkataba huo utapata kukubaliwa rasmi na kuanza kutumika siku ya Jumanne.Hata hivyo vikwazo vipo.Baraza hilo linawaleta pamoja wajumbe kutoka nchi 194 wanachama na ndicho chombo cha kupitisha maamuzi muhimu. Tayari WHO imetangaza mbinu za kubana matumizi.Ujerumani kwa upande wake imeahidi kuongeza mchango wake kwa euro milioni 10 ili kujaliza pengo lililoachwa na Marekani iliyotangaza kujiondoa.
Lengo la mkutano huo ni kupitisha rasmi mkataba wa kimataifa uliotarajiwa kwa muda mrefu kuhusu namna ya kukabiliana na kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza yanayosababisha majanga duniani.